The primary purpose of this blog is to share latest information, opinions, exchange knowledge and expertise on the field of Islamic Finance from different perspectives. The secondary purpose is to share opinions and key development of Islamic Banking and Islamic insurance in Tanzania.
Monday, July 13, 2015
KITABU "KOSA LA BWANA MSA" NA WASHAURI WA BENKI ZA KIISLAMU.
Wiki moja iliyopita nilisoma kitabu cha riwaya nzuri kikiitwa 'KOSA LA BWANA MSA' na katika kufikiria mkasa wa riwaya hiyo na kosa halisi la bwana Msa, nimeona ni vyema mafunzo ya kisa hiki yakaelezwa na kuzingatiwa na washauri wa benki za Kiislamu na hata washauri wa katika maeneo mengine.
Kwa ufupi sana, mwandishi wa riwaya hiyo alionesha kwa uhodari mkubwa kuwa kosa moja la Kisharia ( Sheria za Muumba kwa watu), linaweza kusababisha makosa mengi na hiliki kwa mhusika au jamii kwa ujumla. Bwana Msa ambaye ni mpelelezi alijitwika Usheikh na kutoa fatwa ambayo ilisababisha mke wa mtu, kuolewa na mwanaume mwingine, akazaa naye na kurithi mali ya mwanaume huyo ilihali yeye alikuwa bado ni mke halali wa mtu mwingine. Zaidi ya hayo, ni kuwa mwenye mke alidhurika sana na hata karibu kuwa mwendawazimu kwa kupotelewa na mkewe aliyempenda kwa dhati. Kosa la Bwana Msa, ni kuwa alisema kuwa iwapo mwanamke kaolewa na mwanaume kwa jina ambalo sio la kusajiliwa au ajulikanalo kwalo, basi ndoa hiyo si sahihi. Na kwa msimamo wake huo, ilimpelekea mke baada ya mizonge ya kifamilia ya mume wake huyo aliyemuoa kwa jina tofauti, aliamua bora aolewe na mwanaume mwingine, akazaa na yeye na kuja kurithi mali yake. Uzuri ni kuwa mwishowe Bwana Msa anakumbuka kosa lake na kuomba radhi na msamaha kwa wote waliodhurika kwa kosa lake ili aweze kupata msamaha kwa mola wake.
Funzo kubwa linalopatikana katika kitabu hiki ni kuwa, washauri wowote wanatakiwa kuwa na ujuzi wa kile wakisemacho kuwambia wengine hususani linapokuwa suala hilo linahusu Sharia ya Mola Mtukufu. Iwapo hili halitozingatiwa, mshauri ajue si tu kuwa ni mtu mmoja anayeweza kuathirika na kosa lake bali watu wengi au jamii nzima. Hivyo ni muhimu sana tena sana, washauri wa masuala ya Kisharia katika benki za kiislamu au idhaa na taasisi za Kiislamu, kuwa waangalifu sana na makosa yanayoweza kutokana na ushauri wao na ikawa ni muhali sana kuweza kurekebisha kosa hilo baadaye hata ikiwa ni kwa kuomba radhi. Waswahili wamehadharisha " Maji yamkishamwagika hayazoleki" Tena ikiwa maji hayo ni masuala ya pesa na kuchuma mali, ni jambo gumu sana kurekebishika.
Pamoja na ukweli huu kuwa kusahihisha makosa katika uchumaji wa mali nakadhalika ni jambo zito, mshauri asione aibu kukiri kosa lake kwa wale aliowashauri na kutafuta namna ya kurekebisha athari ya ushauri wake, ili kuwaongoza waathirika namna ya kurejea katika njia sahihi. Jambo hili ni muhimu si tu kwa kujivua dhimma juu ya yale yaliyochumwa, bali ili kupatikana msamaha wa Mola. Akumbuke mshauri kuwa, watu wa motoni (mola atuhifadhi nao), watasema na kumuomba Mola awaongezee adhabu wale waliowapoteza katika kufanya maamuzi.
Hivyo ni wajibu kwa washauri, kuwa waangalifu mno katika kazi zao na kumuogopa Mwenyezi Mungu wasije wakatokwa na machozi ya damu siku ya kuhesabiwa na haitomfaa mtu majuto yake. Mola atufanyie wepesi na azinyooshe kalamu zetu na maneno yetu, katika kuandika na kusema yaliosawa na haki. Ameen.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
Ndugu, nashukuru sana! Kazi yako imenifaa katika Taaluma yangu ninayoifanya ya FASIHI YA KISWAHILI
ReplyDeleteMOLA AKUJAALIE HERI!