Imeandika na Sheikh Tawakkal Juma.
1. ✨ MAANA YA ZAKATUL-FITRI
Ni zaka maalumu inayotolewa baada ya kumalizika mfungo wa mwezi wa ramadhan.
- imeitwa hivyo kwa sababu inawajibika kwa kuingia siku ya idd-el-fitri.
- Piah inaitwa zaka ya viwiliwili na kufungua miili kwa sababu inawajibika kwa kila nafsi na sio katika Mali.
- Zama hii imefaradhishwa mwaka wa pili Hijiria baada ya kufaradhisha funga ya ramadhan.
2. HUKUMU YAKE
Ni wajibu kwa kila muislamu mwanaume na mwanamke, mdogo na mkubwa, aliyehuru au mtumwa anapaswa kuitoa baada ya funga ya Ramadhani kabla ya kuswali swala ya Iddil-Fitri.
- Watoto, wanawake, wazee n.k wasio na uwezo wa kulipa Zakatul-Fitri watalipiwa na mawalii wao (wasimamizi wao).
- Kwamfano katika familia baba atamtolea mkewe na watoto wake ikiwa hawawezi kujitolea, pia atawatolea wazazi wake kama nao pia hawana uwezo wa kujitolea, vilevile baba atalazimika kuwatolea Zakatul-Fitri wale wote wengine ambao ni waislamu walio chini ya uangalizi wake na hawawezi kutoa Zakatul-Fitri.
- Hata mtoto mchanga aliyezaliwa dakika chache kabla ya kuandama kwa mwezi naye pia atatolewa Zakatul-Fitri.
3. WANAOPASWA KUTOA ZAKATUL FITRI
- Zakatul Fitri inamlazimu yeyote yule mwenye kupata chakula cha kumtosha yeye na wale waliochini ya uangalizi wake kwa mchana wa siku ya Iddi na usiku wake na akawa na ziada.
- Ziada hiyo ataitoa Zakatul-Fitri kwa viwango vinavyostahiki.
4. KIWANGO CHA ZAKATUL FITRI
- (Imekuja katika mafundisho ya mtume kuwa kiwango ni Swaa’ moja) ambayo ni makadirio sawa na Kilo mbili na nusu au mchoto wa chakula wa ujazo wa viganja viwili vya mkono vya mtu wa wastani vilivyojaa mara nne.
- Kinachotolewa ni chakula Kinachotumika na watu Katika nchi hiyo
- (mfano mchele) au pia mtu anaweza kutoa kiasi cha pesa chenye thamani sawa na kiasi hicho cha chakula (kisichopungua,ni bora hata ikizidi kdg),
- mfano kilo 2 na nusu ya mchele mzuri katika eneo fulani inaweza kuwa ni Tsh 7000/= (Itategemea na eneo)
5. JINSI YA KUTOA ZAKATUL FITRI
- kwa urahisi zaidi Zakatul Fitri hukusanywa pamoja katika sehemu zenye kuaminika kama misikitini au katika taasisi za kidini na kisha kuwafikishia wahusika hivyo pia ukipata ugumu wa kumfikia mhusika wa kupewa Zakatul Fitri unaweza ukaiwasilisha sehemu hizo.
NB: Kama ukiweza ni vizuri zaidi kutoa chakula na kumfikishia mhusika moja kwa moja kama ilivyokuja kiasili katika hadith ya mtume(s.a.w), licha ya watu kuona kuwa pesa ndiyo rahisi na inapendeza zaidi hata kwa mhusika mwenyewe anayepewa Zakatul Fitri ili kupata na mahitaji mengine lakini tambua pia unaweza kutoa chakula hicho kama Zakatul Fitri kisha na pesa hiyo ya mahitaji mengine kama Sadaqa ya kawaida ambayo ni bora pia.
- Kiasi chini ya kiwango cha Zakatul Fitri na au kutoa kitu kingine tofauti na lengo la Zakatul Fitri hiyo sio Zakatul Fitri ni Sadaqa ya kawaida.
6. UMUHIMU WA ZAKATUL-FITRI
Zakatul-Fitri ni kwa ajili ya kuitakasa funga ya muislamu kutokana na maneno machafu na mambo ya upuuzi wakati alipokuwa katika swaum kwa kuwalisha maskini chakula ili nao wapate chakula kizuri siku ya Iddi na ndio maana kutolewa kwake kunakuwa kabla ya kusali sala ya Iddil-Fitri ili kuendana na maandalizi.
7 . MUDA WA KUTOA ZAKATUL-FITRI
- Muda mzuri zaidi ni wakati kuanzia Magharibi ya siku ya mwisho ya Ramadhani hadi asubuhi kabla ya Sala ya Iddil-Fitri.
- Inaweza pia kutolewa siku mbili au tatu hivi kabla (Chamsingi iwe kabla ya sala ya Iddil-Fitri).
- Kulipa Zakatul-Fitri mapema kabla ya kusali lddi au mapema zaidi ya hapo kutawawezesha maskini na mafakiri kufurahia lddi pamoja na waislamu wengine.
- Ikitokea sababu ya msingi kama vile kusahau na mtu akachelewa kutoa Zakatul-Fitri mpaka lddi ikasaliwa, basi hana budi kuitoa baada ya sala lakini jambo la kuzingatia ni kwamba amri ya kutoa Zakatul-Fitri kabla ya sala imetolewa na mtume (s.a.w) hivyo mtu akiivunja amri hii kwa makusudi au kwa uzembe ajue kuwa atakuwa amefanya makosa.
8 . WANAOSTAHILI KUPEWA ZAKATUL-FITRI
- Wanaostahiki ni maskini na wale wote wasioweza kujipatia chakula pamoja na wale walio chini ya uangalizi wa hao maskini na wasiojiweza ili nao wafurahie Iddi pamoja na waislamu wenzao wenye uwezo.
- Kama pia ilivyo katika Zakatul-Mal akipewa Zakatul-Fitri mtu asiyestahiki itakuwa ni kudhulumu haki ya wale wanaostahiki,
- hivyo mtoaji na mpokeaji wa Zakatul-Fitri hiyo wote watakuwa ni madhalimu.
- Ili kuhakikisha kuwa katika jamii au katika mtaa wa waislamu kila anayestahiki kupewa Zakatul-Fitri anapata na kuzuia uwezekano wa mtu mmoja kulundikiwa Zakatul-Fitri kiasi kikubwa sana na mwingine kukosa au kupata kiasi kidogo sana kisichotosheleza mahitaji yake ya siku ya Iddi,
- basi ni vyema waislamu wa sehemu hiyo waikusanye Zakatul-Fitri kwa pamoja na kisha waigawanye kwa wote wanaostahiki katika mtaa au sehemu hiyo wakizingatia mahitajio yao kulingana nao majukumu ya kifamilia waliyonayo.
- Piah inajuzu kumpa mtu mmoja zaidi ya pishi moja
- Muislamu inampasa achukue juhudi ya kuwatafuta wanaostahiki kupewa zaka hii.
NB:Watu unaowajibika kuwatolea Zakatul-Fitri haihesabiki kuwa unawapa Zakatul Fitri, mfano kuwapa wazazi wako sio Zakatul-Fitri kwani wao ni wajibu wako kuwahudumia.