Pages

Friday, November 7, 2025

HUKUMU YA KIISLAMU KUHUSU KUENDESHA BODA BODA YA BIASHARA: MKATABA, DHUMUNI NA MAADILI YAKE.

Uislamu ni dini inayothamini kazi halali na juhudi za binadamu katika kujitafutia riziki. Mwenyezi Mungu (S.W.) amewataka Waislamu kufanya kazi kwa bidii, kwa kuzingatia maadili yake na kwa njia zinazokubalika kisheria. Moja ya kazi zinazopatikana sana katika jamii ya leo ni kazi ya kuendesha boda boda kwa ajili ya biashara. Kazi hii imekuwa chanzo kikuu cha mapato kwa vijana wengi. Hata hivyo, ni muhimu kuelewa hukumu yake katika Uislamu, pamoja na misingi ya mkataba, dhumuni, na maadili yanayohusiana nayo.


Hukumu ya Kiislamu Kuhusu Kuendesha Boda Boda
Kwa mujibu wa mafundisho ya Kiislamu, biashara ya kuendesha boda boda ni halali (ḥalāl) iwapo kanuni za mkataba wake na maadili yake yatazingatiwa. Hii ni kwa sababu ni njia ya kupata riziki kwa jasho la halali, bila dhuluma wala uovu. Uislamu unakataza kazi zinazohusiana na haramu kama vile usafirishaji wa pombe, madawa ya kulevya, au kushiriki katika wizi na udanganyifu.

Aliulizwa Mtume wa Allah (swallah llahu alayhi wasallam) kuhusu chumo lililobora (njia bora ya kuchuma mali) akasema: Kazi anayoifanya mtu kwa mikono yake na kila biashara nzuri. (Bazaar, Al Hakim, Tabarani. Hadith sahih). Hivyo basi, kuendesha boda boda ni kazi ya staha na yenye heshima, mradi inafanywa kwa uadilifu na kwa kufuata sheria za nchi na dini.

Mkataba katika Uendeshaji wa Boda Boda

Katika Uislamu, mkataba (ʿaqd) ni makubaliano ya msingi katika shughuli za kibiashara baina ya pande mbili. Makubaliano hayo yanapaswa kuzingatia Shariah na kutimizwa ipaswavyo. Mwenyezi Mungu anasema katika Qur’an:
“Enyi mlioamini! Timizeni makubaliano yetu.” (Al-Mā’idah 5:1)
Kazi ya boda boda mara nyingi huendeshwa kwa makubaliano kati ya dereva na mmiliki wa pikipiki na kati ya dereva na abiria. Mkataba baina ya mmiliki na dereva inaweza kuwa ya aina tofauti:
1. Mkataba wa ajira (ʿaqd al-ijārah shakhsiyya) — ambapo dereva anaajiriwa na hulipwa mshahara kwa kufanya kazi iliyobainishwa.
2. Mkataba wa Ijarah Al Manafiy - mmiliki anamkodisha dereva pikipiki kwa malipo kwa siku au wiki au mwezi.
3. Mkataba wa Mudharaba (ushirikiano)- ambapo dereva hugawana na mmiliki mapato yaliyopatikana kwa siku au kwa wiki au kwa mwezi kwa kigawanyo walichokubaliana.
4. Mkataba wa Ijarah Muntahia BiTamleek — ambapo dereva anakodishwa pikipiki na analipa kiasi fulani kwa muda maalum. Baada ya muda kumalizika, anapewa pikipiki kama zawadi au kuuziwa kwa bei nafuu.

Mkataba baina ya dereva na abiria huwa ni mkataba wa ajira, ambapo dereva huajiriwa na abiria kufanya shughuli ya kumsafirisha kutoka sehemu moja kwenda sehemu nyingine kwa malipo maalumu waliyokubaliana.
Uislamu unasisitiza mkataba uwe wa wazi, wa ridhaa kwa pande mbili, na usiokuwa na udanganyifu (gharar) katika malipo au muda au aina ya kazi. Hivyo, pande zote mbili zinapaswa kuelewana vizuri kuhusu malipo, majukumu, na matengenezo ( baina ya mmiliki na dereva) ili kuepuka migogoro.


Dhumuni la Kuendesha Boda Boda

Dhumuni la Kiislamu na nia ya Muislam katika kazi ni kutafuta riziki ya halali kwa ajili ya kujitegemea, kujitosheleza na kuisaidia jamii. Dereva wa boda boda anapofanya kazi kwa nia njema — yaani, kutafuta riziki halali, kuepuka omba omba, na kuwahudumia watu — basi matendo yake yanakuwa ibada. Nia njema (niyyah) inayofungamana na matendo mema ndiyo inayoamua malipo mema mbele ya Mwenyezi Mungu.

Maadili ya Kiislamu Katika Kazi ya Boda Boda


Uislamu umeweka maadili ambayo kila Muislamu anapaswa kuyafuata katika kazi yake. Dereva wa boda boda anapaswa kuwa mfano wa maadili haya katika jamii. Baadhi ya maadili hayo ni:
1. Uaminifu (Amānah): Kuwa mwaminifu na kutoiba mali ya abiria au kuficha mapato halisi ili kuzuia haki ya mwaajiri katika mapato hayo (chini ya mkataba wa Mudharaba). Mtume (swallah llahu alayhi wasallam) alisema: “Mfanyabiashara mwaminifu na mkweli atakuwa pamoja na manabii, wakweli na mashahidi.” (Tirmidhi)
2. Uadilifu (ʿAdl): Kutozidisha nauli au kumdhulumu mteja kwa kufanya udanganyifu wa bei. Ni nguzo katika mkataba wa ajira, dereva na abiria wakubaliane bei ya kazi kabla ya kuanza kazi husika ili kuwa na uwazi na kuepuka migogoro.
3. Utii wa sheria (Ṭāʿah): Kufuata kanuni za usalama barabarani kama vile taa za barabarani, kuvaa helmet, kupakia abiria idadi inayoruhusiwa, kuwa na leseni, kuwa na bima ya chombo (third party insurance) na kadhalika.
4. Nidhamu: Kuvaa mavazi safi na yanayositiri mapaja, kuwa na lugha ya heshima, na kuzungumza na abiria kwa adabu. kadhalika kuendesha pikipiki katika njia yake na sio katika njia ya watembea kwa miguu.
5. Kuepuka madhambi: Kuepuka kugusana na abiria wa jinsia ya kike na ikiwa hakuna budi kuepuka kupakia abiria wa jinsia tofauti. Mtume (swallah llahu alayhi wasallam) amesema: Mmoja wenu kugongwa na chuma kichwani kwake ni bora kwake kuliko kumgusa mwanamke ambaye si halali yake. (Imepokewa na Tabarani, Hadith Hasan). Kadhalika abiria ambaye dhumuni la safari yake ni kwenda kufanya maasi na ikawa imebainika kwa dereva dhumuni hilo, utapaswa kukataa kutoa huduma hiyo ili kuepuka kusaidia katika uovu.

Kwa mujibu wa mafundisho ya Kiislamu, kuendesha boda boda ya biashara ni kazi halali, yenye staha na yenye baraka, mradi inafanywa kwa haya tuliyoyaeleza. Mikataba inapaswa kuwa ya haki na ya wazi, dhumuni la kazi liwe ni kutafuta riziki halali, na maadili ya Kiislamu yazingatiwe wakati wote. Uislamu haukatazi kazi yoyote halali, bali unasisitiza uaminifu, uadilifu na nidhamu katika utekelezaji wake. Kwa hivyo, dereva wa boda boda anayefuata misingi hii tunatarajia atapata baraka katika riziki yake, amani katika maisha yake, na thawabu mbele ya Mwenyezi Mungu (S.W.).

No comments:

Post a Comment