The primary purpose of this blog is to share latest information, opinions, exchange knowledge and expertise on the field of Islamic Finance from different perspectives. The secondary purpose is to share opinions and key development of Islamic Banking and Islamic insurance in Tanzania.
Tuesday, August 12, 2014
AHMED EL NAGGAR: MWANZILISHI WA BENKI ZA KIISLAMU KWA MSAADA WA WAJERUMANI.
Jina la Ahmed el Naggar ni maarufu mno katika taaluma ya benki za Kiislamu au ulimwengu wa benki za Kiislamu. Jina hili ndilo pekee linalohusishwa na uanzilishwaji wa benki ya Kiislam pale Mit Ghamr nchini Misri miaka ya 1960's. Lakini pamoja na kazi na mafanikio makubwa aliyoyapata msomi huyu katika nyanja ya masuala ya fedha, machache yanafahamika kumhusu yeye hata miongoni mwa wale waliobobea katika masuala ya fedha ya Kiislamu. Ni swali zito ukumuuliza leo mtu aliyesomea masuala ya fedha ya Kiislamu kuwa ilikuwaje mtoto wa Abdul Aziz el Naggar, profesa wa masuala ya kiislamu katika jiji la mishemishe la Cairo, alikuwa ni mmoja katika watu wenye ushawishi mkubwa katika ulimwengu wa fedha wa Kiislamu. Unaweza usipate jawabu au wachache sana wenye kufahamu maisha ya msomi huyu.
Kutokana na upungufu huu, hususani kwa wazungumzaji wa lugha ya Kiswahili nimeonelea nifunguke kidogo kwa kuwaeleza yanayofahamika kumhusu msomi huyu na namna alivyofanikiwa kuanzisha benki ya kuweka akiba chini ya misingi ya Kiislamu katika kipindi ambacho watawala wa nchi ya Misri walikuwa wanakabiliana na ushawishi wa vikundi vyenye mlengo wa Kiislamu nchini humo.
WAKULIMA WA MISRI-FALLAHEEN.
Ahmed Naggar, ni msomi aliyehitimu mafunzo yake ya uchumi katika mji wa Cologne nchini Ujerumani alijifunza mambo mengi pamoja na kujuana na watu wengi ambao walikuwa na msaada mkubwa katika mpango wake wa kuwa na utaratibu wa kibenki wenye kuzingatia Sharia ya Kiislamu kwa ajili ya kuwasaidia wanyonge na wakulima masikini wa Misri ambao hadi leo wanajulikana kwa jina maarufu la Fallaheen. Wakulima hawa na wafanya biashara ndogo ndogo kama ilivyo leo hawakuwa na dhamana ya maana ya kuweka benki ili waweze kupata mikopo. Benki za Misri hazikuwa kwa ajili yao na hata kufukuzwa wanaposogelea majengo ya benki hizo. Njia pekee ya wao kuweza kupata mikopo ni kwa kupitiya watu wajanja na wanyonyaji ambao walikuwa tayari kuwapa mikopo lakini kwa riba kubwa sana kuliko iliyopo katika mabenki. Wanaokubali kukopa hawakuweza kujikwamua kutoka katika mzunguko wa madeni ya kila mara.
Naggar alichukizwa sana na riba na unyonyaji huu uliokuwa ukifanywa na wakopeshaji binafsi na kuhamasika kudidimiza utaratibu wao wa kinyonyaji kwa kuja na utaratibu ambao utawawezesha wakulima si tu kukopa bila riba bali kuweka akiba kama sharti la msingi la kukopa.Dhamira yake ilikuwa kuanzisha benki kwa ajili ya wakulima na watu masikini.
Hakukuwa na namna ya kuanzisha benki isiyojishughulisha na riba, yenye kuhimiza kuweka akiba ili kukopa (Saving Bank) na kuwajali masikini wakati huo katika nchi ya Misri na wala hakukuwa na mfano wa kuiga wa kuanzisha na kuendesha benki ya Kiislamu katika miaka hiyo ya 1950's. Bahati nzuri, mahali pekee pa kujifunza uendeshaji wa benki za kuweka akiba ilikuwa nchini Ujerumani kwa kuwa benki hizo zilishatimiza miaka mia moja katika shughuli zake na kwa mafanikio katika nchi ya Ujerumani. Kujifunza taratibu za benki hizi haikuwa jambo gumu kwa Naggar kwa kuwa alishawahi kufanya kazi katika moja ya benki yenye utaratibu huo iliyokuwa ikifahamika kwa jina la German Kreissparkasse Koln au Cologne Saving Bank.Alikuwa amehamasika na benki hizi kwa kuwa zilikuwa zinajihusisha na watu wa vijijini mahala ambapo yeye alikusudia benki yake ihudumu katika nchi ya Misri.
Nchi ya Misri ni yenye wakulima wengi wadogowadogo na wakiishi vijijini wasiokuwa na mitaji na hivyo Naggar alikusudia kuwasaidia watu hawa masikini kwa njia ya kuwa na benki ambayo itahimiza uwekaji wa akiba na kisha benki kuziwekeza katika miradi yenye faida, kisha faida hiyo itagawiwa kwa wakulima na hivyo kuweza kunyanyua kiwango cha maisha yao.
Naggar alikuwa ni mtu mcheshi na mchangamfu sana na mweye uwezo mkubwa wa kushawishi watu ili wamsaidie katika mipango yake. Mmoja katika watu waliovutika na mpango wake huu alikuwa ni msomi Bw.Gunter Klower, akifundisha uchumi. Haikuchukuwa muda bwana huyu alikuwa rafiki mkubwa na Naggar akimtembelea nyumbani kwake kama sehemu ya familia. Mipango mingi na majadiliano juu ya uwanzishwaji wa benki ya kiislamu ilikuwa ikifanyika hadi usiku wa manane katika meza ya chakula jikoni, katika nyumba ya Bw. Gunter. Wakati mwingi marafiki wa familia ya Gunter kama vile Bw. Haider Dewar-alipata kuwa waziri wa fedha wa Afghanistan,Bw. Wolfgang Hohmeyer na Bw.Martin Gester walikuwa wakishiriki majadiliano haya.
Urafiki wake na Bw.Klower ulikuwa wa kushibana sana na bwana huyu ndiye aliyekuwa mfadhili wa fikra ya kimapinduzi katika benki ya kutoa huduma za benki katika gari aina ya VW (VolksWagen). Fikra hii ya kutumia gari ilikuja kufaa sana katika uendeshaji wa benki ya kiislamu kwa kuwa ilimuwezesha Naggar kufika sehemu mbalimbali za vijijini na kutoa huduma ya kibenki. Hiki kilikuwa kipindi ambacho mambo yote ya kibenki kama vile mikopo ilikuwa lazima ruhusa itoke Cairo, mji mkuu tena kwa kutoa rushwa( Bakhshees). Naggar ilibuni utaratibu wa kuwapa mamlaka na maamuzi wakuu wa kamati za vijiji (decentralized system), mkulima mwenye shida ya pesa atasema mbele ya kikako cha kijiji na wazee wa kijiji wataamua nani apewe mkopo.
PESA ZA KUANZISHA ZILITOKA WAPI?
Ili uwe na benki ni lazima uwe na fedha za kuanzisha na wakati huo kuwa na ushawishi wa kisiasa. Kwa uhodari wake wa kujieleza na uaminifu wake alikwisha jijengea akiwa ujerumani, aliweza kupata fedha kutoka katika jumuiya ya mabenki ya akiba ya ujerumani na serikali ya shirikisho ya ujerumani. Wajerumani walichukulia majaribio ya kuanzisha benki ya akiba nchini Misri kuwa ni jambo la kimapinduzi na zuri kama sehemu ya utoaji wa msaada wa kifedha. Msaada huu waliuchukulia kuwa ni mradi kabambe wa kufikishwa fikra na ushawishi wa ujerumani katika nchi ya kiarabu. Hivyo waliuita mpango wao kuwa ni “Development of a regional savings
bank sector in Egypt”. Kwa kweli haijulikani ni kwa namna gani siasa za ujerumani zilipelekea kufanya maamuzi ya kuupa pesa mpango wa Naggar katika kipindi kigumu cha vita baridi iliyokuwa ikiendelea katika siasa za kimataifa. Pamoja ha hiyo, serikali ya ujerumani ilikubali kuwapa mafunzo ya kiufundi wafanyakazi 20 katika benki hii chini ya Naggar na kupeleka wataalamu watatu wa masuala ya benki za akiba kwa ajili ya ushauri na usaidizi.
Sasa kuishawishi serikali ya Misri ilikuwa ni jambo zito sana ili mradi huu uweze kuanza. Naggar aliepuka sana kutumia jina la Uislamu katika kuelezea mradi huu ukizingatia kuwa wanasiasa wa ngazi za juu wakishughulika kupunguza ushawishi wa uislamu katika siasa za nchi hiyo hususani baada ya kukoswa kuuliwa kwa Gamal Abdi Nasser katika miaka hiyo ya 1954 lawama zikiwaendea wafuasi wa udugu wa Kiislamu (Muslim Brotherhood). Mambo yalikuja kusonga mbele baada ya kutumia wanafamilia wa Naggar ambao walikuwa na ushawishi kwa Mkuu wa Idara ya Upelelezi ya nchi hiyo maarufu kwa jina la Mukhabaraat ambaye alikuja kumtambuslisha Naggar kwa maafisa wa ngazi za juu katika wizara ya mambo ya uchumi. Baada ya muda, fikra na mradi wa Naggar ulipata ruhusa na serikali ya Misri ilichangia paund za misri elf 60 kwa ajili ya mradi huu.
Kwa hakika kabla ya kupewa fedha na umoja wa mabenki ya akiba nchini ya ujerumani Bw. Walter Quade, mwenyekiti wa benki ya akiba ya Frankfurt aliuuliza swali la wazi; kuweka akiba bila ya riba, tueleze namna inavyofanya kazi? Kwa mara nyingine Naggar aliweza kuwashawishi hata wale waliokuwa wakimkosoa kwa kuelezea utaratibu wa kugawana faida au hasara katika Sharia na kuwa huo ndio msingi wa uendeshaji wake. Akiba zote ni vyema zikawekezwa katika benki za vitenga uchumi au miradi ambayo itaamuliwa na wanachama wa kijiji husika. Faida itakayopatikana itagawiwa kwa wale walioweka fedha zao na ikitokea hasara itabebwa na wanachama wa kijiji husika. Kwa hakika maelezo yake yaliweza kuungwa mkono na serikali ya ujerumani na jjumuiya ya benki za akiba za ujerumani kwa kupewa kasoro robo milioni DM (DEUSTCHMARKS).
KUANZA KWA BENKI NA KUFA KWAKE.
Baada ya kupata fedha na kuungwa mkono na wanasiasa wa Misri, Naggar na marafiki zake wa ujerumani wa walifika Cairo mwaka 1963. Naggar alichagua sehemu iitwayo Mit Ghamr, karibu na Nile Delta kaskazini mwa Cairo na kuwaendea wakulima na wakuu wa vitongoji pamoja na maimamu ili kuwaelezea mpango wake.
Kwa mara nyingine, ucheshi wake na ushawishi wake mzuri ulimuwezesha si tu kuanzisha benki lakini mpaka kuiendesha. Aliwashirikisha sana maimamu wa sehemu za vijijini kuitangaza benki yake isiyotoza au kutoa riba. Maimamu walikuwa na kazi ya kuishauri benki na kuhamasisha watu wajiunge kwa wingi. Njia hii iliwezesha ndani ya mwaka mmoja kuwa na akaunti 25,000 zenye amana za wateja zifikazo nusu milioni DM. Benki ilianza kukua kwa kasi na kufungua matawi sehemu nyingine kama vile Dakahlia, Zifta na Cairo, lakini kukua huku kulileta changamoto kubwa. Wafanyakazi wa benki walikabiliwa na amana nyingi za wateja lakini wakiwa na uhaba wa miradi ya kuekeza ili kuleta faida.
Changamoto ya pili ilitokana na waendesha benki za riba na wanasiana kuingiwa na woga. Waendesha benki za riba waliona mafanikio ya benki hii yanaweza kupelekea kupigwa marufuku kwa riba. Wanasiasa wakihofia watu kuvutiwa na utaratibu huu na kutaka taratibu za kiislamu zitumike kuendesha mambo ya nchi. Matokeo yake mwaka 1969, matawi yaliokuwa yakifanya vizuri yalilazimishwa kuungana na benki ya serikali iitwayo Nasser Social Bank na hapa ndio ikawa mwisho wa jaribio la kwanza la kuanzisha benki ya Kiislamu nchini Misri.
HAIKUWA MWISHO WA NAGGAR.
Kufa kwa jaribio hili halikuwa mwisho wa Naggar. Kwa hakika alikuwa amekifanya kitu ambacho hajafanya mtu mwingine kabla yake na fikra na jaribio hilo likawa ndio chachu ya kuibuka kwa benki za Kiislamu. Alionesha kwa vitendo kuwa kuna njia nyingine ya kuweza kuhamasisha uwekaji wa amana (mobilisation of deposit) chini ya utaratibu Kiislamu wa kugawana faida na hasara. Jambo hili lilipelekeya kuonekana kwa uwazi kuwa ipo namna ya kuepuka benki za riba.
Naggar aliendelea na fikra yake hii na kumshawishi tajiri Prince Mohammad Faisal Al Saudi na Sheikh Saleh Kamel kuanzisha benki ya Kiislamu. Price Mohammad Faisal chini ya msaada wa Naggar aliweza kuanzisha benki ya kiislamu nchini Misri mwaka 1975. Ushawishi wa Naggar uliweza kumpatia uungwaji mkono na Waziri wa masuala ya dini na wakfu wa nchi ya Misri Sheikh Shaarawi, ambaye kwa wadhifa wake aliweza kushawishi kupitishwa kwa sheria mpya katika bunge la nchi hiyo. Hizo sheria mpya ndiyo ziliwezesha kustawi kwa Faisal Islamic Bank. Utaratibu wa kiislamu uliweza kuvutiya serikali nyingine ulimwenguni na Naggar na Price Faisal wakaweza kuanzisha benki hii katika nchi ya Sudan, Pakistan, Switzerland, Bahrain na Cyprus.
Wawili hawa waliungana kwa ajili ya kuanzisha benki za kiislamu na piya walikuja kuwa marafiki wakubwa na kuongozana pamoja katika safari muhimu hadi kuja kufanikiwa kuanzisha Islamic Development Bank (IDB), benki iliyochini ya umoja wa nchi za kiislamu duniani (OIC) na ambayo ilipata fedha nyingi kutoka kwa familia ya Al-faisal.
Vilevile, Naggar alisimamia uanzishwaji wa taasisi ya ushauri juu ya uchumi na benki za kiislamu iitwayo, International Association of Islamic Banks (IAIB) hapo mwaka 1977 ambayo alihudumu kama Katibu Mkuu. Kazi kubwa ya taasisi hii ilikuwa kushawishi viongozi wa kisiasa na kijamii kuunga mkono benki za kiislamu na kutoa ufumbuzi wa changamoto za kiutendaji zinazozikabili benki za kiislamu.
Kwa hiyo leo hii wakati tukishuhudia mafanikio makubwa katika masuala ya kibenki ya kiislamu, ni muhimu kukumbuka mchango mkubwa wa bwana huyu ambao unaenda mbali zaidi ya benki za kiislamu, na kufikiya kuwa ndiye mwanzilishi wa Islamic micro-finance na kwa kuzibadilisha jamii za waislamu kuja kuwa ni jamii zinazotumia huduma za kibenki. Naggar atakumbukwa daima kwa juhudi hizi baada ya miaka mingi tangu alipofariki mwaka 1994.
Chanzo.
Makala hii ni tafsiri isiyorasmi ya makala ya Bi Rebecca Schonenbach na Gerd klower yenye anuani 'Ahmed Naggar-the pioneer of Islamic Banking.'iliyochapwa katika "Bulletin" ya The European Association for Banking and Financial History mwaka 2014.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment