The primary purpose of this blog is to share latest information, opinions, exchange knowledge and expertise on the field of Islamic Finance from different perspectives. The secondary purpose is to share opinions and key development of Islamic Banking and Islamic insurance in Tanzania.
Thursday, May 21, 2020
KUDHIBITI BEI (TAS'IR) KATIKA UISLAM
Kwa muda mrefu tumekuwa tukisikiya juu ya serikali kuwataka wafanyabiashara wauze bidhaa fulani za chakula kwa bei elekezi. Vile vile kuna bidhaa ambazo tangu kuingizwa kwake sokoni bei huwa imeshapangwa na serikali kama vile mafuta ya petroli n.k. Bidhaa nyingine bei hupangwa na nguvu ya soko (market forces).
Mwanzoni wa mwezi huu tumesikiya juu ya kuadimika kwa sukari jambo ambalo serikali imelikanusha kuwa sukari ipo lakini kuna watu wemeihodhi kwa manufaa yao binafsi. Na upande mwingine kuna taarifa kuwa viwanda kadhaa vipo katika kurekebisha mitambo yao na pia kutokana na mvua kubwa zinazoendeleya nchini Tanzania kumepelekeya miwa kutokuwa na sukari ya kutosha. Ili kukabiliana na uhaba huo hatuwa zifuatazo zimechukuliwa:
1. Serikali imeagiza sukari kutoka nchi ya jirani ya Uganda.
2. Serikali kuwataka wafanya biashara wauze kwa bei elekezi ya serikali. Bei za sukari ni kama ifuatavyo, Iringa (2900), Mbeya (3,000), Rukwa, Katavi, Ruvuma (3,200), Njombe (2,900), Lindi, Mtwara (2,800), Arusha, Kilimanjaro, Manyara, Tanga (2,700), Dar (2,600), Pwani, Morogoro (2,700), Kagera, Mwanza, Shinyanga,Simiyu, Geita (2,900), Mara (3,000), Kigoma (3,200), Singida, Tabora, Dodoma (2,900), Songwe (3,000). Wale waliokutwa wakiuza bei ya juu, hatuwa kadhaa zimechukuliwa ikiwemo:
a. Kufunga maduka ya wafanya biashara waliokiuka bei hiyo elekezi. Huko Kigoma, Mkuu wa Mkoa aliwafungia wafanya biashara watano kwa kuuza bei zaidi ya iliyoelekezwa.
b. Kupigwa faini au adhabu ya kupokonywa leseni na kupigwa faini.
Utetezi wa wafanyabiashara waliokamatwa ni kuwa sukari imeadimika na kuwalazimu kuinunuwa kwa bei ya juu ili kuweza kuisambaza bidhaa hiyo kwa wananchi na wao kupata faida kidogo (bei elekezi 3200 wao wanauza 3700 kwa Kigoma). Ikumbukwe kuwa tatizo hili sio mara ya kwanza kujitokeza. Mwaka 2014 jambo hili lilijitokeza tena na pia miaka ya nyuma.
Suala la kudhibiti bei ni nyeti, la kiuchumi na kidini. Uislam unasemaje kuhusu kudhibiti bei kupitiya vyombo vya dola / serikali? Uislam haujaliwacha suala hili bila muongozo wake. Kimsingi, bei hupatikana kwa njia mbili.
1. Nguvu ya Soko (market/ natural forces). Allah s.w.t ndie mwenye nguvu ya kufanya bidhaa fulani iwepo au isiwepo na pia ndie mwenye uwezo wa kufanya watu wahitaji bidhaa fulani au wasihitaji, kwa kuwa anadhibiti nyoyo za viumbe vyake na anafanya anavyokataka. Hivyo yeye Mola ndio anayedhibiti bei za bidhaa kwa kupitia uwezo wake wa kuruhusu bidhaa iwepo au isiwepo (supply side) na pia kudhibiti uhitaji wa bidhaa hiyo sokoni (demand side). Hivyo, pande mbili hizi zinapokutana na kuwafikiana bei wenyewe bila mtu yoyote wa tatu kuingilia.
2. Kupitia bei elekezi za serikali kwa ajili ya kulinda maslahi ya ummah. Hivyo serikali inaweza kutowa maelekezo ya bei kwa bidhaa au huduma fulani. Njia hii ya serikali kupanga bei ni suala lenye ikhtilafu wa wanazuoni. Wapo wanaowafiki kwa masharti na wanakaotaa kuwa serikali isiingilie bei ya soko.
Serikali huingilia bei ya soko ( intervene) kwa kutowa maelekezo ya bei ya bidhaa au huduma husika kwa lengo la kumlinda mnunuzi wa mwisho. Hamna ambaye anamashaka na nia njema ya serikali katika kupanga bei. Njia hii ndio inaitwa Taasir. Imam Shafii anaeleza kuwa Tas'ir ni hali ambayo serikali inatowa amri ya kuuza bidhaa kwa bei kadhaa katika soko.
Baadhi ya wanachuoni wanaona kuwa moja ya wajibu wa serikali ni kupanga bei ya bidhaa muhimu inapokuwa kuna haja ya kufanya hivyo. Na wapo wanaoona kuwa kimsingi, katika suala la kuendesha uchumi, wajibu wa serikali sio kupanga bei bali kuhakikisha hamna mwenye kuhodhi bidhaa au wenye kufanya ubabaishaji na kuhakikisha kuwa bei za sokoni zinaenda kwa mujibu wa nguvu ya soko bila ya kuwepo haja ya serikali kutowa bei elekezi. Kwa sababu Mtume s.a.w amesema kuwa "...bei hupangwa na Mungu, ndie mwenye kuzuia na kukunjuwa rizki kwa waja wake..." [Hadithi Sahih]
Hadithi hiyo huchukuliwa kama hoja dhidi ya serikali kupanga bei. Hata hivyo, wapo wanao ona kuwa muktadha wa hadithi hiyo ni kuwa katika hali ya kawaida hamna haja ya kuingilia na kuelekeza bei ya bidhaa sokoni. Lakini hadithi hii haizuii serikali kuingilia kati pale inapodhihiri kuwa kuna kuhodhi soko (monopoly) kwa wazalishaji au wauzaji wachache kwa manufaa binafsi. Ikibainika jambo hilo ndipo inadhihiri haja ya serikali kupanga bei kwa:
-----Kuunda mamlaka maalumu yenye wajuzi wa masuala ya bidhaa na masoko ili kusimamia bei za bidhaa husika sokoni. Wajuzi hawa watafanya tafiti zao kubaini chanzo cha bei kupanda au kushuka isivyokawaida na baada ya kubaini visababishi vyote vya hali hiyo wataweka bei ya sawa na haki inayozingatiya gharama (cost) na faida (profit). Bei hiyo iwe ni ya uadilifu na haki, pia iwafikiwe na wahusika-wazalishaji na wanunuzi. Katika kufanikisha hili pande zote zizingatie kuheshimiana, kuhurumiana na kuvumiliana.
Izingatiwe kuwa kuhodhi bidhaa ni kinyume na Sharia pale mtu anapohifadhi ghalani bidhaa inayohitajika ili kutengeza upungufu na kunyanyuwa bei ya soko kwa makusudi. Hata hivyo, mkulima hatakiwi kushurutishwa kuuza bidhaa zake sokoni. Kazalisha mwenyewe na hivyo anahaki auze au la. Vilevile watengezaji wa bidhaa za ubunifu, wana haki ya kuamuwa wauze au la na muda gani. Ni haki yao hiyo. Lakini wazalishaji wa viwandani (producers) au wafanyabiashara (traders) hawatakiwi kuzuia ghalani bidhaa zao kwa sababu ya kutaka kupata faida kubwa.
Fikra za wanazuoni kuhusu Taasir.
Kimsingi, kati hali ya kawaida ni haramu serikali kuweka bei elekezi za bidhaa na huduma bila ya kuwepo haja yoyote ya kufanya hivyo. Huu ni mtazamo wa maimam wanne, pia Ziaidiya na Imamiyah. Hii ni kwa sababu, suala la mauziano ni mawafikiano ya pande mbili kwa hiari yao. Haifai pande moja kushurutishwa kuuza au kununuwa kwa bei fulani.
Katika zama za Mtume iliwahi kutokeya watu kumfuata ili apange bei. Hali iliyokuwepo ni kuwa bidhaa iliadimika sokoni na mahitaji yaliongezeka. Hapakuwa na makubaliano ya kibinafsi ya wauzaji wala kuhodhi mali. Kwa hali ya kawaida ni kuwa, kunapokuwa na ongezeko la mahitaji na uchache wa bidhaa, bei hupanda. Mtume s.a.w alikataa kupanga bei ilipotokeya bei kwenda juu akisema "bei hupangwa na Mungu, ndie mwenye kuzuia na kukunjuwa riziki kwa waja wake. Mimi nataka nikutane na Mola wangu nikiwa sina haki ya mtu mwingine iwe katika damu yake au mali yake!"
Pamoja na msimamo huo, wanazuoni wametofautiana kuhusu wajibu wa serikali kupanga bei katika hali isiyokuwa ya kawaida (exceptional cases) ili kuhifadhi maslahi ya ummah. Kuna makundi matatu au rai tatu katika jambo hili:
1. Imam Abi Hanafa, anachukulia kuwa ni Makruh Tahrimi (jambo lisilopendeza linaloekeya katika katazo).
2. Imam Shafii, anachukuliya kuwa ni haramu kupanga bei iwe kuzipandisha au kuzishusha katika hali yoyote iwayo.
3. Imam Hanbali, wao wanatofautisha aina mbili za kupanga bei- kwa haki na kwa dhulma. Kupanga bei kwa haki kunaruhusiwa na kwa dhulma ni haramu.
Imam Shawkani, anaona kuwa tas'ir ni haramu kutokana na matumizi ya nguvu na ubabe unaotumika ndani yake. Hii ni kwa sababu kila mtu anahaki na mali yake na hivyo kupanga bei ni kuingiliya haki hiyo. Kadhalika Imam Ibn Hazm na Al Mawardi, wanapinga kabisa kupanga bei za bidhaa kwa hali yoyote ile na kwa bidhaa yoyote ile, iwe bei imepanda au imeshuka.
Hivyo, wale wanaokataa kupanga bei wanafuata maana ya hadithi iliyotajwa hapo juu na wale wanaoona kuwa kuna mazingira yafaa na wakati mwingine haifai, imetokana na Ijtihadi zao kwa kuzingatia hali ilivyo. Wao wanaona kuwa Mtume s.a.w hakupanga bei kwa sababu masoko yaliendeshwa kwa uadilifu. Wauzaji hawakufanya hila yoyote katika kupanda kwa bei na hivyo basi iwapo itaonekana kuwa kuna hila ya wauzaji basi mtawala anaweza kuingiliya kati ili kulinda maslahi mapana ya umma. Lakini ikiwa ni kutokana na kuadimika kwa bidhaa husika sokoni bila kufichwa na wauzaji au kuongezeka kwa hitajio la watumiaji ni haramu kupanga bei katika hali hiyo.
Hivyo kuna hoja tatu za wanaopinga kupanga bei.
1. Haifai kumlazimisha muuzaji kuuza kwa bei asiyokuwa radhi nayo. Mtume s.a.w amesema "Haifai kula mali ya Muislam ila kwa kuridhiya mwenyewe kwa nafsi yake.
2. Mtume s.a.w aliombwa apange bei na alikataa kufanya hivyo.
3. Ni dhulma kumlazimisha mtu mwenye mali yake kuuza kwa bei asiyoridhiya.
4. Inaweza kuchangiya kuibuka kwa soko la kificho (black market) kwa sababu ya kuminya uhuru wa wazalishaji au wauzaji kuuza kwa bei waitakayo.
Kwa upande wa wanachuoni wanaona kuwa inafaa kupanga bei, wameweka masharti katika kufanya hivyo. Ibn Taymiyyah anawafiki kupanga bei ya haki iwapo jambo hilo litapelekeya kusimamisha haki hasa pale iwapo watu hawatoweza kupata mahitaji yao ya msingi isipokuwa kwa njia ya kupanga bei ya haki (fair price) na inapokuwa imethibiti kuwa wafanya biashara wanafanya hila kwa ajili ya kujinufaisha. Hatahivyo, mpangilio uliowekwa na wanachuoni hawa ni kuwa ipatikane jopo la wataalamu watakaotazama chanzo cha mtikisiko wa bei na kuja na ufumbuzi kwa njia ya mashauriano na sio kwa njia ya kulazimisha na ubabe (by force and tyranny).
Hivyo basi iwapo fikra ya kupanga bei haina budi kufuatwa, mashauriano ya kina (public and private dialogue) katika kutafuta chanzo na suluhisho ni muhimu kabla ya watumishi wa serikali kufika katika maduka ya watu na kutowa adhabu na kuwaharibia heshima zao wafanyabiashara hao kwa kuwatuhumu na kuwaadhibu kwa wakati mmoja. Watumishi wa serikali wakiwa na mashaka na wafanyabiashara ambao wanahodhi, njia nzuri ni kuwapeleka mahkamani. Adhabu ibaki kuwa ni eneo la mahkama kuamuwa. Muuza duka mtaani kutofuata bei elekezi ya serikali haipendezi lakini je ni haki kufuata bei elekezi yenye kumpatia hasara au kumfungiya mlango wake wa riziki? Pia imedhihirika kuwa serikali inazo njia nyingine za kukabiliana na upungufu wa bidhaa iwe kutokana na kuhodhi kwa wafanya biashara au kwa kuwepo ongezeko la mahitaji, nayo ni njia ya kuagiza bidhaa hiyo kwa wingi kutoka nchi nyingine.
Kwa kuhitimisha, natarajiya kuwa watendaji wa serikali wamche Mungu zaidi wakijuwa kuwa suala la kupanga bei sio jepesi, kuingiliya mali ya mtu binafsi sio jambo jepesi. Muhimu zaidi ni kuwa njia yakuagiza kutoka nje, kuwadhibiti wanaohodhi na kuwa na jopo la wataalamu kwa ajili ya mashauriano inapaswa kuzingatiwa sio kwa bidhaa za mafuta pekee bali hata kwa mazao mbalimbali inaodhihiri haja ya kufanya hivyo.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment