Pages

Friday, April 2, 2021

BARUA KWA WAZIRI MPYA WA FEDHA NA NAIBU WAKE.

Napenda kutanguliza pongezi za dhati kwa Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano, Ndugu Samia Suluhu Hassan na Makamu wa Rais Dr. Philip Mpango kwa kuwa viongozi wetu katika kipindi hiki kigumu cha maombolezo na changamoto zinazotokana mbalimbali. Kwa hakika tumewabebesha mzigo mzito wa Uongozi wa Taifa zuri la Tanzania. Lakini tunaimani kuwa kwa sifa na taaluma zenu na aina ya viongozi ambao wapo na mtakaowateua siku zijazo, mtaweza kuipekeka mbele Tanzania ili kuwa ni mwangaza na mfano wa kusifika katika bara la afrika kama ambavyo kwa utashi wa Mola, nchi yetu imebarikiwa kuwa na mengi ya kusifika nayo. Kadhalika pongezi zangu za dhati kwa Mh. Mwigulu Nchemba na Mh. Hamad Masauni, kwa kuaminiwa na kuteuliwa na Mh. Raisi kuongoza Wizara ya Fedha na Mipango ya nchi. Kwa maneno ya Rais, uteuzi wenu umezingatia sifa zenu na rekodi zenu za utendaji wa muda mrefu katika utumishi wa Umma. Kwa hili, hatuna mashaka kuwa mtaishi katika kutimiza matarajio ya aliyewateua kwa manufaa yetu sote wananchi wa Tanzania. Wakati mnaapishwa, Rais na Makamu wa Raisi wamewapa kazi ya kwanza na kwamba hilo liwe katika kipaumbele chenu. Bila shaka jambo hilo ni muhimu katika kutimiza matakwa ya katiba ya JMT, kuondoa kero na hivyo kuudumisha Muungano wetu. Kwa bahati nzuri jambo lenyewe linahusiana na masuala ya fedha ili kudumisha Muungano wetu, na mimi barua yangu hii inajikita katika eneo la sekta ya fedha lakini kwa maslahi ya muungano wetu na wananchi wote. Tangu nchi yetu pate uhuru wake imekuwa ikifuata sera mbalimbali za fedha na kiuchumi. Kutoka katika mfumo sera za kiuchumi wa kijamaa mpaka mfumo wa sera za soko huria. Katika safari yetu ya maendeleo, tumekabiliana na dhoruba mbalimbali katika sera zetu za kifedha na kiuchumi. Yapo mafanikio na yapo maeneo ambayo kwa hakika tunapaswa kuyafanyia kazi haraka iwezekanavyo ili kwenda sambamba na kasi ya mabadiliko ya sekta ya fedha ulimwenguni ambazo zitawawewesha wananchi wote kunufaika na fursa za kiuchumi bila kikwazo chochote. Katika eneo ambalo nakuomba Waziri wetu mpya na Naibu wake walipe kipaumbele kinachostahili na ambalo huenda hawatolisikia ndani ya Wizara zao kutoka kwa makatibu na wakurugenzi wao ni maeneo mawili. Hata hivyo kwa leo nitalieleza jambo la kwanza na la pili wakati mwingine iwapo tutajaaliwa ili nisiirefushe barua hii nalo ni; kuhakikisha sera zetu na mikakati yetu katika sekta ya fedha (financial sector policies) inatambua na kuweka mazingira rafiki kwa watoa huduma mbalimbali za kifedha (financial services providers) iwe taasisi za serikali kama mifuko ya uwezeshaji ya serikali na taasisi zake na taasisi za kifedha za binafsi zinakidhi mahitaji yao ya jamii yote ya watanzania (whole-society approach). Tumezoea kusoma na kusikia kuwa tunao mkakati wa mfumo wa fedha jumuishi (Inclusive Financial Sector Strategy) lakini suali la msingi ni kweli jumuishi? Naomba nitoe mifano michache ili idhihirike kuwa mkakati wetu bado haujatambua mahitaji ya baadhi ya wanajamii yetu ambao idadi yao sihaba na hivyo bado hatujawa jumuishi. Mikopo ya watumishi serikalini na Taasisi zake. Serikali yetu inawatumishi wa Imani tofauti kama ilivyo jamii ya watanzania, hata kupelekea viongozi wetu mnapotusalimia mnasema “As Salaam Alaykum” na pia “Bwana Yesu asifiwe”. Kadhalika, madhehebu hizi mbili zimekuwa zikishiriki kuliombea taifa nyakati tofauti na katika hafla tofauti za kiserikali. Hatahivyo, mikopo kwa watumishi wa serikali na taasisi za wizara zinazotoa mikopo hiyo inafuata utaratibu mmoja tu wa kukopesha kwa RIBA kama vile wananchi wote ni wa dini moja ambao wanaamini kuwa kukopesha kwa riba ni halali! Hili si kweli Mh. Waziri. Ni jambo linalofahamika kwa waislamu wote, hata Naibu wako anaweza kukuthibitishia kuwa ni HARAMU muislamu kukopa au kukopesha kwa njia za RIBA kwa mujibu wa Imani yake. Muislamu anayekopa au kukopeshwa kwa RIBA inawezekana kwa kutojuwa mafunzo hayo au kupuuzia na hivyo kujiweka katika laana ya Muumba wake. Mtume Muhammad s.a.w amesema “ Mwenyezi Mungu amemlaani mwenye kutoa riba, kupokea riba na kushuhudia miamala ya riba.” Qurani inasema “Amehalalisha Mwenyezi Mungu biashara na ameiharamisha RIBA” ( Sura ya 2: aya ya 275). Ukilizingatia mafunzo haya utafahamu kwa nini Waislamu wengi hawatumii huduma za mikopo ya kibenki, ya vyama vya kuweka akiba na kukopa, za taasisi za mikopo ya serikali bali hata mikopo ya bodi ya elimu ya juu! Vilevile, Waislam hawawekezi katika hati fungani za serikali (treasury bills and treasury bonds) au kuwekeza katika mifuko ya uwekezaji (UTT) ambayo njia zao kuu za mapato ni RIBA. Kutokana na bidhaa za kifedha zisizokidhi matakwa yao, Waislam wanaepuka BIMA sio kwa sababu BIMA ni kitu kibaya bali muundo wa huduma za BIMA zilizopo haukidhi vigezo vya kibiashara au mashirikiano kwa misingi ya uadilifu. Tumeunguliwa na rasimali zetu na mashule yetu kadhaa mwaka 2020 kwa kukosa bima inayofuata misingi ya ushirikiano katika kusaidiana wakati wa hatari (TAKAFUL) badala ya bima ya mauziano kwa kitu ambacho hakipo wakati wa mauziano hayo. Mifano hii michache itoshe kukuonesha ni kwa kiasi gani Serikali katika kuijenga sekta ya kifedha “jumuishi” na kutoa huduma za kifedha za mifuko ya serikali ya uwezeshaji kama vile SELF MF, SIDO, Presidential Trust Fund, Youth and Women development Fund, NEDF, UTT zimewaacha 98% ya matakwa ya Wazanzibari na asilimia takribani 50% ya waislam wa Tanzania bara. Hali hiyo ipo hivyohivyo katika sekta binafsi ya fedha. OMBI KWA WAZIRI WETU JUU YA NINI KIFANYIKE La kwanza, ni kutambuwa uwepo wa kundi hili maalum katika jamii yetu ambalo linahitaji kujumuishwa katika kupata huduma za kifedha na kiuchumi nchini kwa kupita utoaji wa huduma za kifedha zinazozingatia uchumi wa kiislam. Kwa hakika jambo hili, limetambuliwa vyema na ilani ya CCM (2020-2025) paragrafu ya 159 (f) inayoahidi“Kuimarisha utoaji wa huduma za kifedha kwa mfumo wa uchumi wa kiislam” kwa upande wa Zanzibar. Hatahivyo, hilo ni hitajio tena kubwa zaidi kwa upande wa Tanzania bara. Bahati mbaya sana kuwa mpango wa maendeleo wa tatu wa miaka mitano ijayo (FYDPIII) unaoandaliwa haujazingatia mahitaji ya kundi hili wala ahadi ya Ilani ya CCM. La pili, maandalizi mbalimbali yameshachukuliwa katika makaratasi na baadhi ya taasisi zilizopo chini ya wizara yako ili hatua zingine zifuate. Hatahivyo, hamna taarifa yoyote mpaka sasa juu ya hatuwa zilizofutwa au zitakazofuatwa. Kwa mfano, Benki Kuu kwa kushirikiana na wataalamu wa benki ya dunia ilishafanya uchambuzi wa mambo ambayo yanapaswa yafanyike kuhusu sera za kibenki na kisheria na kikanuni ili kuweka mazingira rafiki kwa benki za kiislam kufanya shughuli zake bila bughudha au hofu (Islamic banking supervisory and regulatory framework) kutoka kwa mamlaka nyingine za serikali kama vile Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na kadhalika. Mfano wa pili, ni kanuni za bima ya Kiislam (Takaful) ambazo zimekuwa tayari tangu mwaka 2017 na mtangulizi wako ambaye kwa sasa ni Makamu wa Raisi katika mkutano na wadau wa BIMA nchini uliofanyika mkoani Tanga aliahidi kuwa atachukuwa hatuwa za haraka (ministerial interventions) ili zipitishwe na kuanza kutimika. Lakini hakujaaliwa, na hivyo nakuomba ulipokee suala hili ili kufanikisha ahadi ya Makamu wa Raisi kwa wadau. Nikuhakikishie kuwa iwapo kanuni hizo zitakapopitishwa, tutapata uwekezaji katika katika eneo hili na hivyo kuchangia kukuwa kwa sekta ya bima nchini, kutoa ajira na kuingiza mapato mapya serikalini. La mwisho, kwa kuwa kuna mengi ya kujifunza, kubadilishana mawazo na kusahihisha sintofahamu zinazoweza kuwa ni kikwazo cha utekelezaji, nikuombe Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Naibu wako mkutane na taasisi inayoitwa CENTRE FOR ISLAMIC FINANCE, COMPLIANCE AND ADVISE (CIFCA) ya hapa nchini Tanzania ambayo inalengo la kuisaidia na kushirikiana na serikali na sekta binafsi ili kukidhi mahitaji ya kundi hili katika jamii yetu. Nimaombi yangu kwa Mungu kuwa ushauri wa barua hii utaupokea ukiwa na furaha ya katika siku hizi za mapumziko ya kitaifa na utaufanyia kazi kwa kasi na hatimaye mfumo wa huduma zetu za kifedha nchini ziweze kusema “As salaam Alaykum” na “Bwana Yesu Asifiwe” kama ambavyo viongozi wetu mmekuwa mkitusalimia kwa kuzingatia umajumui wa jamii ya watanzania wote. Shukrani.

No comments:

Post a Comment