Pages

Tuesday, March 25, 2025

SUKUK NI WIZI NA UTAPELI?

Nimeona katika mitandao ya kijamii maneno ambayo hayapaswi kukaliwa kimya hususani na wadau wa sekta ya fedha ya Kiislam. Maneno hayo anuani yake ni "SUKUK NI WIZI NA UTAPELI, BENKI KUU TOENI TAHADHARI" ukiwa "unaonekana" kuingiza Sukuk katika kinyang'anyiro cha mashindano ya Kisiasa visiwani Zanzibar lakini pia huenda waandaaji wake wana malengo ya kutia hofu wananchi dhidi ya hatua kubwa iliyofikiwa nchini ya kuwa na Sukuk iliyotolewa na SMZ. Tunajiuliza dhamira gani waliyonayo wale walioandaa ujumbe huo? Kwa nini katika mikopo yote ya serikali ya Zanzibar hatujasikia kunasibishwa na Wizi na Utapeli isipokuwa Sukuk?


Waingereza wanamsemo wao "If you want to kill a dog, give it a bad name (ukitaka kumuua mbwa, mpe jina baya)." Kuinasibisha sukuk na wizi na utapeli ni katika mkakati mbaya sana na haunabudi kukemewa vikali na wadau wote wa maendeleo jumuishi katika nchi yetu. Nakemea kitendo hicho ambacho sio cha kistaarabu wala uungwana, huku nikiwa na matumaini kuwa vyombo vya usalama vitakuwa mbioni kuwatafuta watu waliopo nyuma ya ujumbe huo na kuwachukulia hatua stahiki.


Sitoingia katika ujumbe wa kisiasa uliovikwa tu ndani ya ujumbe huo, bali ninachokiona ni mashambulizi dhidi ya Sukuk kama njia mbadala na jumuishi kwa maendeleo ya nchi yetu. Hivyo, niseme kuwa kwa mujibu wa mpango wa maendeleo wa miaka mitano (FYDP), Sukuk inatambulika na mamlaka za nchi kama njia mbadala wa kuwezesha maendeleo ya nchi yetu. Zanzibar Sukuk ni hatua kubwa katika kutekeleza mpango huo na inatambulika na Benki Kuu na Mamlaka ya Masoko ya Fedha na Mitaji nchini. Hivi karibuni, tumeona Gavana wa Benki Kuu akiwa na Waziri wa Fedha wa Zanzibar akipendekeza wananchi wawekeze katika Sukuk hiyo. Hivyo, ni hujuma mbaya sana kutumia upotoshaji kwa lengo si tu la kupata kiki ya kisiasa bali kuichafua Sukuk kama njia jumuishi na inayotambulika nchini. Wale walionyuma ya ujumbe huo, waache mwenendo huo ambao unaathari mbaya sana katika kujenga jamii ya watu wastaarabu, maendeleo endelevu na utoaji wa huduma jumuishi za kifedha nchini.


Kwa upande mwingine, ujumbe huo umedhihirisha na kutukumbusha kiasi gani Siasa inavyoweza kuathiri huduma za kifedha za Kiislam ktk nchi zetu. Binafsi, imenikumbusha kitabu cha Prof Rodney Wilson, The Politics of Islamic Finance akionesha namna gani Siasa za nchi zinaweza kuathiri vizuri au vibaya maendeleo ya Islamic Finance. Kwa muktadha huo, hatupaswi kukaa kimya pale tunapoona watu wachahe wanataka "kutumia siasa chafu" katika jambo muhimu kama hili lenye kujumuisha na kuwapa watu fursa kushiriki katika maendeleo ya nchi yao na kukuza vipato vyao kwa njia Halali bila Riba!


Kwa kuhitimisha, mara zote tumeona athari chanya ya utashi mzuri wa kisiasa kupitia ilani za vyama vya Siasa na utekelezaji wake katika kuwezesha huduma za kifedha za Kiislam nchini kustawi na kunufaisha wananchi. Wote walionyuma ya utashi huo mzuri, tunawapongeza na kuwataka wasikatishwe tamaa kwa hali yoyote iwayo. Hii ni mara ya kwanza natumai itakuwa ya mwisho, kuona watu kupitia "mlango wa kisiasa", wakihusisha Sukuk na wizi au utapeli. Waislam na hususani wataalamu wa masuala ya kifedha ya Kiislam, hatuwezi kukaa kimya na kukubali upotoshaji huo kwa kupitia mlango wa Kisiasa ambao unahujumu au kurejesha nyuma juhudi za miongo kadhaa zenye dhamira ya kutoa fursa kwa Waislam na wananchi wengine kushirikiana na Mamlaka za nchi yao katika upatikanaji wa huduma jumuishi za kifedha nchini.

No comments:

Post a Comment