Pages

Monday, June 16, 2014

KITABU: KINGA YA RIBA KATIKA UISLAMU NA PROF. FADHILULLAH.


Mwaka 2011 kilichapwa kitabu chenye maudhui juu ya Riba ambacho hakikupatapo kuwepo kabla yake kwa wasomaji wa lugha ya Kiswahili. Kitabu hicho ni tarjuma ya kitabu ambacho asili yake ni katika lugha ya kiarabu ikiwa ni tasnifu iliyoletwa kwa madhumuni ya kupata shahada ya Uzamivu (PhD) iliyofanywa na mwanazuoni Professa Fadhilullah na kufasiriwa na Sheikh Suleiman Amran Kilemile, mola awajaze kheri.

Nimepata bahati ya kukisoma kitabu hiki mwanzo hadi mwisho katika siku zake za mwanzo baada ya kuarifiwa na msanifu wa kitabu hicho ndugu yangu Bw. Iddi S. Kikong'ona. Leo nimeoneleya nikitaje kitabu hiki na kuwaomba kila mmoja wetu atafute nakala ya kitabu hiki ambacho kimebainisha Riba kikamilifu na kuijadili kwa mapana na kisomi.

Kitabu hiki kina milango miwili; Mlango wa kwanza ni kuhusiana na Riba-Ufahamu wake, Hukumu yake na Madhara yake katika jamii. Mlango wa pili unahusina na taratibu zenye kukinga na Riba.

Naweza kusema kwa kinywa kipana kuwa kwa Mswahili na wengineo,(neno Mswahili si tusi bali ni jina la kila mtu ambaye enzi hizo kabla ya mabomba ya maji alikuwa anenda chooni na kopo la maji na kwa sasa anapojisaidiya haja kubwa au ndogo lazima atumiye maji),kitabu hiki ni chenye kukusanya kila linalopaswa kusemwa juu ya njia halali za kuchuma mali na njia zilizoharamu katika kuchuma mali. Haya mambo mawili, yampasa kila mtu na si muislamu tu ayajue kindaki ndaki na mfasiri ameyabainisha kwa lugha tamu ya kiswahili na kwa njia ambayo mtu wa darja yeyote ya kielimu anaweza kuelewa yaliyomo.

Mwandishi kwa namna ya kipekee amemaliza kitabu chake kwa ombi linalopaswa kuzingatiwa aliposema "Mtafiti anatumia nafasi hii kuomba wanazuoni, walinganiaji wa dini, matajiri Waislamu, wenye haja katika wanaoongoza dola za Kiislamu, wanasaikolojia na watafiti wa Kiislamu kusimamia wajibu wao kwa ajili ya kuokoa watu na janga la Riba ambalo ni kubwa sana."

Kitabu hiki kinapatikana katika maduka ya dini ya kiislamu karibu na Masjid Mtoro, Kariakoo Dar es salaam.

Mola atufanyie wepesi kutimiza wajibu wetu na ombi zuri la ndugu yetu. Ameen.

No comments:

Post a Comment