Pages

Wednesday, June 18, 2014

Serikali Kulipa Riba Sh5 Bilioni Deni la Miezi Sita.


Gazeti la leo na Mwananchi limepambwa na habari ya kuhuzunisha. Gazeti limeandika "Serikali italazimika kulipa hasara ya zaidi ya Sh5.2 bilioni (Dola za Marekani milioni 3.1) ambazo ni riba ya malimbikizo ya malipo ya miezi sita kwa Kampuni ya Jacobsen Elekron AS inayotekeleza awamu ya kwanza ya mradi wa umeme wa Kinyerezi, Dar es Salaam.

Gazeti hili limebaini kuwa kampuni hiyo ya Norway inaidai Serikali Dola 48.8 milioni (Sh80.52 bilioni), yakiwa ni malimbikizo ya malipo kuanzia Novemba mwaka jana na Mei mwaka huu.

Laibuka bungeni

Juzi jioni, suala hilo liliibuliwa na Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe ambaye alisema Serikali imekuwa ikipata hasara ya mabilioni ya fedha kutokana na kupanga utekelezaji wa miradi mikubwa pasipokuwa na uhakika wa fedha.

Akichangia hoja ya Bajeti ya Serikali, Mbowe ambaye pia ni Mbunge wa Hai (Chadema) alisema: “Wakati Serikali ikitafuta fedha za kutekeleza miradi ya maendeleo, tumekuwa tukiingia kwenye madeni ya ajabu ambayo kama tungekuwa makini yangeweza kuepukwa.

“Ninao mfano halisi hapa ambao unaonyesha jinsi Serikali itakavyolazimika kulipa riba ya zaidi ya Sh5 bilioni kutokana na kushindwa kulipa fedha za Kampuni ya Jacobsen inayojenga mradi wa Kinyerezi One, hii ni aibu kubwa maana tumelimbikiza madeni ya miezi sita na wanatudai Dola za Marekani 48 milioni.”

Mradi wa awamu ya kwanza Kinyerezi unakusudia kutumia gesi kutoka Mtwara ukiwa na uwezo wa kuzalisha Megawati 150 za umeme.

Mradi huo uliopangwa kukamilika mwishoni mwa mwaka huu, unagharimiwa na Serikali ya Tanzania kwa Sh293.28 billion, lakini gharama hizo tayari zimeongezeka kutokana na riba inayotokana na ucheleweshaji wa malipo.

Hii si mara ya kwanza Jacobsen kulalamikia ucheleweshaji wa malipo, Novemba mwaka jana, Meneja Mkazi wa Mradi, Shaun Moore aliuambia ujumbe wa Serikali na nchi wadau wa maendeleo waliotembelea miradi ya umeme na gesi kwamba: “Ucheleweshaji wa malipo ni tatizo kubwa." Mwisho wa kunukuu.

Riba Kongwe na iliyosambaa.

Aina hii ya riba ni kongwe sana na katika zama zetu imesambaa katika mikataba mingi ya kibiashara na kifedha. Wakati wa Mtume s.a.w, mtu alikuwa anakopeshwa pesa na anatakiwa arejeshe ndani ya muda maalumu. Siku ya malipo ikifika anaambiwa alipe deni au aongezewe muda na kulipa ziyada. Wanazuoni wameiita riba aina hii, Riba Al Jahiliyyah au Riba ya Qur'ani kwa kuwa wakati Qur'ani inateremshwa riba hii ilikuwa imeenea sehemu kubwa ya bara Arab.

Hivi sasa riba aina hii imechukuwa sura ile ile ya kuchelewa kufanya malipo kwa wakati na hivyo mdaiwa analazimishwa kwa mujibu wa mkataba kulipa ziyada. Bila shaka riba hii inaweza kuepukwa iwapo serikali itakuwa makini na vyanzo vyake vya mapato na kusimimia vizuri wajibu wake wa kulipa madeni yake kwa wakati. Ni wazi kuwa serikali haijashindwa kulipa lakini wale waliopewa jukumu la usimamizi wa miradi na malipo yake hawawajibiki ipasavyo. Wakati umefika sasa badala ya kusikia tu kuwa hasara kama hii inajitokeza, wale wote waliohusika na usimamizi mbovu wa miradi na malipo yake wawajibike au wawajibishwe ili liwe funzo kwa watumishi wengine. Wananchi na kodi zao si za kulipiya uzembe unaofanywa na wachache kwa kuwa hasara hii haikubaliki!

Napongeza gazeti la Mwananchi na Bw. Mbowe kwa kuoneshwa kukerwa na uozo huu. Watanzania tuamke na kuishinikiza serikali kwa kupitia wawakilishi wetu suala hili na mengineyo yenye sura hii yakome na tuone wazembe wote wanaosababisha hasara na ubadhirifu wa fedha za umma wanachukuliwa hatua za kisheria.



No comments:

Post a Comment