Pages

Monday, September 14, 2020

ILANI ZA VYAMA KWA JICHO LA UCHUMI WA KIISLAMU- SEHEMU YA KWANZA

Wiki iliyomalizika vyama mbalimbali vimezinduwa kampeni na ilani zao. Ilani ni maandiko muhimu. Katika siasa, ilani ndio mkataba unaotumiwa na chama cha siasa na kujifunga na wananchi katika kipindi fulani. Vyama vilivyozinduwa ilani hizo ni pamoja na CCM, CHADEMA, ACT WAZALENDO na vinginevyo japokuwa havitajwi sana na vyombo vya habari nchini. Kama wananchi na waislamu tunatakiwa tusome ilani hizo na kuzichambuwa iwapo zinakidhi mahitajio yetu na zinatupeleka katika kujenga nchi ambayo wananchi wake wanafursa sawa za kiuchumi, kijamii na kadhalika. Kubwa zaidi ni kutazama iwapo vyama husika vinalenga kutumikiya wananchi bila ya kumuudhi Muumba wetu kwa yale ambayo inakusudiya kuyafanya au kutoyafanya katika kipindi cha miaka mitano ijayo (2020-2025). Wanasiasa na watu kwa kawaida wanaona kuwa ilani nzuri ni ile inayokelezwa na ilani mbaya ni ile ambayo haikutekelezwa. Hatahivyo, katika mizani ya Uchumi wa Kiislamu, ilani nzuri ni ile ambayo vipaumbele vyake vya kiuchumi na sera zake za fedha zinazingatia uadilifu na kutovunja amri za Muumba wetu. ILANI YA CCM NA VIPAUMBELE VYAKE. Kwa kuanzia na ilani ya CCM ambayo ndio chama kinachoongoza serikali kwa sasa kuna maandiko mawili yanayoelezeya ilani yao. Andiko la kwanza ni ilani yenyewe yenye kurasa 308 na la pili ni muhtasari wa ilani wenye kurasa 19. Katika ilani kuna mengi ambayo yanastahili kuchambuliwa lakini makala haya yanalenga katika kutazama ilani hii inasemaje kuhusu Uchumi wa fedha au sekta ya fedha (Financial Economy or Sector) kwa mtazamo wa uchumi wa Kiislamu. Ifahamike uchumi wa nchi una mambo mengi ndani yake ikiwemo suala la Uzalishaji kupitia Kilimo, Viwanda na Utoaji huduma za msingi nakadhalika. Hivyo sekta ya fedha ni eneo dogo kwa uchambuzi lakini ni muhimu mno katika maendeleo ya uchumi wa nchi. Katika vipaumbele sita vya CCM vilivyoainishwa katika Muhtasari wa ilani, suala la uchumi linachukuwa 50% ya vipaumbele vyote kama vifuatavyo; 1. Kukuza uchumi wa kisasa, fungamanishi, jumuishi na shindani uliojengwa katika msingi wa viwanda, huduma za kiuchumi na miundombinu wezeshi; 2. Kuleta mageuzi ya kilimo, mifugo na uvuvi ili kuwa na uhakika wa chakula na kujitegemea kwa chakula wakati wote na kuchangia kikamilifu katika maendeleo ya uchumi; 3. Kutengeneza ajira zisizopungua 8,000,000 (milioni nane) katika sekta rasmi na isiyo rasmi kwa ajili ya vijana. Kwa vipaumbele hivi, inaweza kusemwa kuwa ilani hii ni ya kukuza uchumi na maendeleo ya uchumi. SEKTA YA FEDHA Katika ukurasa wa 19 wa ilani, umuhimu wa sekta hii unatambuliwa. Ilani inasema "Kutokana na umuhimu wa sekta ya fedha katika kuchochea shughuli za kijamii na kiuchumi, katika kipindi cha mwaka 2015 hadi 2020, Chama kiliendelea kuisimamia Serikali kuchukua hatua mbalimbali za kuboresha huduma za fedha kwa wananchi." Kadhalika katika ukurasa wa 213, ilani inasema "Huduma za fedha, ikiwemo za kibenki na mifumo ya malipo, masoko ya mitaji, bima, hifadhi za jamii, na huduma ndogo ndogo za fedha (microfinance), ndio mlizamu wa kuimarisha uchumi." Hivyo, huduma za fedha ni muhimu katika kuimarisha na kuharakisha miamala ya kiuchumi Katika awamu ijayo, Ilani imebainisha baadhi ya hatuwa ambazo zinastahili pongezi, nazo ni: Mosi, kuongeza upatikanaji wa huduma za kifedha kwa gharama nafuu kwa kupanua wigo wa matumizi ya TEHAMA katika utoaji wa huduma za kifedha ili kuongeza huduma jumuishi za fedha nchini, kuchochea uwekezaji wa ndani na kukidhi mahitaji halisi ya wananchi hususan wa kipato cha chini na waishio vijijini. Pili, Kupunguza vikwazo vya ushirikishwaji wa Watanzania kwenye mfumo rasmi wa fedha, ikiwemo kuimarisha ulinzi wa watumiaji wa huduma za kifedha (consumer protection) kwa kukamilisha na kutekeleza Mpango Kabambe wa Taifa wa Maendeleo ya Sekta ya Fedha 2019/20 - 2029/30. Tatu, Kuboresha na kuimarisha huduma za kifedha zikiwemo benki, masoko ya mitaji, bima na huduma ndogondogo za kifedha na utendaji wa taasisi za sekta ya fedha na kodi ili ziendelee kutoa mchango mkubwa katika ukuzaji wa uchumi wa Taifa. Taasisi hizo ni pamoja na Benki kuu ya Tanzania (BoT), Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA). Nne, hususani kwa upande wa Zanzibar, ilani ya CCM ukurasa wa 214 (F) inaelekeza SMZ "Kuimarisha huduma za kifedha kwa mfumo wa uchumi wa Kiislam." Kwa upande wa pili, zipo hatuwa ambazo zinachukiza. Hatuwa hiyo ni ile ambayo imetajwa katika muhtasari wa ilani ukurasa wa 18 F (ii) kuwa katika kutengeneza ajira Milioni 8, mambo ambayo chama kinaahidi kufanya ni pamoja na " Kuwawezesha vijana kushiriki katika shughuli za ujasiriamali, ikiwemo kuwapatia mafunzo na kuwaunganisha na taasisi na asasi za utoaji mikopo yenye riba na masharti nafuu;" Ujasiriamali sawa, kupata mafunzo sawa lakini kuunganisha vijana wakiwemo vijana wa kiislam na taasisi za utoaji mikopo yenye riba, hili ni baya mno! Uislam unakataza kujihusisha na riba kwa kuwa ni dhambi kubwa na yenye kuangamiza duniani na akhera. Hii inatia doa ilani hii. MAPENDEKEZO. Kwa ujumla, napendekeza mambo yafuatayo yazingatiwe iwapo chama cha CCM kitaendeleya kuongoza serikali: 1. Kusahihisha dosari hii iliyopo katika muhtasari huu kwa kuahidi ya kwamba "itawaunganisha na asasi za utoaji mikopo yenye riba na ambayo haina riba!" Ni wajibu wa serikali, kuhakikisha taasisi na asasi zake kama mabenki ya serikali yanayohuduma ya mikopo bila riba kwa njia ya kufanya mauziano au kukodisha au ushirika katika faida na hasara na wateja wake. 2. Izingatiwe na watunga sera na mipango ya nchi kuwa kikwazo kikubwa cha ushirikishwaji wa Watanzannia kwenye mfumo rasmi wa fedha sio kukosekana ulinzi wa watumiaji wa huduma za kifedha (consumer protection) pekee bali kuachwa huduma za kibenki kutowa mikopo kwa njia ya RIBA, kuachwa taasisi za mikopo midogo kutoza RIBA, kuachwa huduma za bima kufanya shughuli zake kama mashirika ya kamari na kuwekeza kwa njia za RIBA, kukosekana ushirikishwaji wa taasisi za kijamii zenye wataalamu Waislam kutoka Bara kama vile CIFCA na kutoka Zanzibar kama vile UKUEM katika uandaaji wa Mipango ya Maendeleo ya Sekta ya Fedha. Kukosekana ushirikishwaji huu kumepelekeya watunga mipango kutozingatia desturi, mila na dini za wananchi ambao ndio walengwa wa mipango husika. Jambo hili linapaswa kusahihishwa haraka iwezekanavyo. 3. Ilani iweke wazi zaidi kile kinachokusidiwa kufanywa. Kwa mfano ilani inasema "Kuweka mazingira wezeshi kwa sekta ya bima kukua zaidi, kuwanufaisha wananchi wengi na kuchangia katika uchumi kwa kiwango kikubwa zaidi;" Ni mazingira gani hayo ambayo kwa sasa hayapo na hivyo yatawekwa ili sekta hii ikue zaidi? Ndani ya muda gani mazingira hayo yatakuwa yameshawekwa? Hivyo ni muhimu watunga ilani watusaidie kujibu maswali hayo bila kusahau kilio cha muda mrefu cha kuwa na bima ya Kiislamu (Takaful) ambayo kwa takribani miaka 5 yote imekosekana idhini ya waziri wa fedha bila kuwepo kwa sababu zozote zinazofahamika. 4. Kama ambavyo imeoneana umuhimu kwa upande wa Zanzibar kuimarisha huduma za kifedha kwa mfumo wa uchumi wa Kiislamu, kadhalika kwa upande wa bara umuhimu huo ni mkubwa zaidi ukinzingatia kuwa Waislam waliopo bara ni wengi zaidi ya waislam wote wa Zanzibar. Na mahala mnasaba pa kuanzia ni mpango kabambe wa maendeleo ya sekta ya fedha utambue mfumo wa fedha wa Kiislamu na taasisi za fedha zote za serikali na zile ambazo serikali ni mmiliki wa hisa nyingi, kuwe na mipango ya makusudi ya kuanzishwa huduma za kifedha zinazokidhi mfumo wa uchumi wa Kiislamu. Iwapo dosari hizi zitarekebishwa na kutekelezwa, ni matumaini yangu serikali itafanikiwa katika vipaumbele vyake vitatu vya kiuchumi vilivyoainishwa hapo juu kwa maslahi ya wote na sio kwa maslahi ya wachache.

No comments:

Post a Comment