Pages

Wednesday, August 26, 2020

JENGA UCHUMI WAKO BINAFSI

Tumezoea kusikia kuhusu kujenga uchumi wa nchi na kuleta maendeleo. Tunaambiwa kuwa uchumi unakuwa kila mwaka na hivyo maisha ya watu yanaimarika. Hali hiyo inaweza kuwa sahihi iwapo wewe na mimi tunajizatiti kujenga uchumi wetu binafsi. Na abadan ukuaji huo wa uchumi hautomnufaisha yule ambaye amekaa maskani asubuhi na jioni akizungumza kuhusu mechi au wanayosema wanasiasa majukwaani au wanayofanya wasanii au amekaa nyumbani na kutazama filamu mbalimbali au kucheza games za kieletroniki n.k Hivyo, ili uchumi wako binafsi uimarike lazima kila mmoja wetu ajizatiti katika mambo yafuatayo muda wote wa uhai wake. 1. Ajifunze misingi ya elimu ya biashara. Iwe mfanyabiashara au mfanyakazi, elimu ya biashara ni elimu muhimu sana kwa kila mmoja wetu. Unatakiwa ujuwe biashara ni nini? Namna ya kuweka mahesabu, namna ya kuuza bidhaa au huduma, namna ya kuzungumza na wateja, namna ya kupata mitaji, namna ya kujitangaza na namna ya kuibuwa mawazo ya kibiashara ambayo yatatatuwa tatizo la mtu au watu kwa njia ambayo watu hao watakauwa tayari kulipiya ili kupata ufumbuzi wako. Somo la biashara hufunzwa katika elimu sekondari kupitiya somo la commerce na book keeping. Kwa bahati mbaya, watu wanahiyari ya kuyawacha masomo hayo wanapoingiya kidato cha tatu. Kwa maoni yangu, ilipaswa kuwe na somo moja mjumuiko wa masomo haya ambayo iwe mtu ni wa arts au science ataendeleya kusoma ili kumjenga kujuwa namna biashara inavyopaswa kufanywa. Umuhimu wa somo hili ni kuhakikisha ya kwamba anayemaliza kidato cha nne awe anayomsingi imara wa kuweza kujiajiri na kujenga uchumi wake na wa familiya yake. Biashara tunazofanya kimazoea na kupitia ushauri wa rafiki badala ya wataalamu, hautoshi kukuimarisha kiuchumi. Hata ikiwa ulipitwa na masomo hayo, sasa hivi katika umri ulionao tenga muda wa kusoma maudhui fulani za somo la biashara na ufanyie kazi. Hatuwa hizi zitakuweka katika mstari wa kujenga uchumi wako. Soma sana vitabu au sikiza mazungumzo yanyolenga kukuongozea maarifa katika ufanyaji biashara iweya vitu au ya kutoa huduma (mwajiriwa) 2.Tumia muda wako vizuri. Muda ndio rasilimali kubwa aliyopewa mwanadamu na neema kubwa kabisa ni kuwa na imani/ tawheed. Kama muislam, ushapewa neema ya tawheed na kinachofuata ni kutumia rasilimali ya wakati vizuri. Wakati ndio uhai wenyewe. Ukitoka kazini au ukishafunga biashara yako jioni, jiulize maswali yafuatayo; kitu gani napaswa kufanya ili kuboresha utendaji wangu kazini au kuboresha biashara yangu? Watu wengi huwa hawana jawabu ya swali hili. Hiyo sio dosari. Dosari ni kuridhika kwa kukosa jawabu! Dosari ni kudhani kuwa hamna anayejuwa jawabu! Dosari ni kuifungiya ndani ya fikra zako na ukawacha mlango wa kutafuta ushauri kwa wengine. Imesemwa "washauri wenye ujuzi, utapata nuru ya maarifa yao." Hivyo badala ya kupoteza muda wako wa jioni ukishafunga kazi au kupoteza muda siku za week end, tumiya muda huo kujumuika na familiya yako na piya kukusanya maarifa mapya ili kuboresha zaidi. Hili ni jukumu lako la kila siku ili kujenga uchumi wako ambao utakuwa imara. 3. Weka malengo yako na ujilazimishe kuyatimiza. Ni muhimu uwe na malengo ya kukuza kipato chako kila mwaka. Iwe kwa kupitiya ajira au kwa kulima au kwa kuzalisha au kwa kufanya biashara ambazo zinaboresha maisha ya watu wengine. Tunaishi wakati ambo taarifa za watu wengine ni nyingi mno katika magazeti, mitandaoni na mitangazo. Taarifa hizi nyingine zinaweza kukupa maarifa na nyingine zinaweza kukutowa katika malengo yako. Hivyo ni muhimu ujilazimishe kuyafikiya malengo yako kila mwaka na usikubali kuondoka katika malengo uliyojiwekeya na kuishi katika malengo ya wengine. Sasa tupo katika mwaka mpya wa Kiislam, chukuwa kalamu na karatazi uandike kipato ambacho ungependa ukifikiye ifikapo mwisho wa mwaka na nini unapaswa kufanya ili kufikiya malengo hayo. Usipofanya hivyo, usilalamike pale gharama za maisha zinapoongezeka na wewe miaka nenda rudi umejifunga katika kipato cha miaka ya nyuma! Kila siku zinavyoenda unatakiwa ujenge uchumi wako au hali ya kiuchumi itakuwa na changamoto ya kutegemeya wengine. Weka malengo na kisha tekeleza peke yako au pamoja na wengine!

No comments:

Post a Comment