The primary purpose of this blog is to share latest information, opinions, exchange knowledge and expertise on the field of Islamic Finance from different perspectives. The secondary purpose is to share opinions and key development of Islamic Banking and Islamic insurance in Tanzania.
Wednesday, August 12, 2020
UCHUMI JUMUISHI NA MCHANGO WA CIFCA
Wiki iliyopita tulitowa mfano mmoja unaonesha upungufu wetu katika kujenga uchumi jumuishi. Makala haya yataeleza mifano mingine michache na kueleza mchango wa CIFCA katika masuala ya fedha na kuwa na uchumi jumuishi.
Mikopo wa wafanyakazi serikalini.
Serikali kama taasisi nyingine hutowa mikopo nafuu kwa watumishi wake. Mikopo hiyo huelezwa kuwa haina riba lakini kwa jicho la Uislam ipo riba iliyojificha au kufichwa chini ya kile kinachoitwa tozo mbalimbali za mkopo huo. Wanachuoni wanaona kuwa mkopo wowote ambao unatozo au unamnufaisha mkopeshaji isipokuwa tozo halisi tu ambazo hulipwa kwa watowa huduma wengine. Kwa mfano tozo ya kutuma mkopo kwenye simu au kwenye bank yako inaweza kukusanywa na mkopeshaji kama gharama halisi ya mkopo unaotolewa. Gharama au tozo ambazo hazifungamani moja kwa moja na gharama halisi za mkopo.
Baraza la Taifa la uwezeshaji wananachi Kiuchumi (NEEC).
Baraza la taifa ambalo limeundwa na kuanza shughuli zake mwaka 2005 lina dhima ifuatayo "Kuongoza Watanzania kuelekea katika uchumi thabiti wa taifa kwa kutengeneza mazingira rafiki ya biashara na ushiriki sawa katika kiuchumi." Ni dhima inayoleta matumaini na baraza lina program nzuri za kuwawezesha watanzania kujiimarisha kiuchumi. Hatahivyo, yapo maeneo machache yanayopaswa kufanyiwa kazi ili kuwapa waislamu fursa sawa na wananchi wengine.
Tovuti ya baraza inaeleza kuwa kuna mifuko ya Serikali na Programu za uwezeshaji wananchi kiuchumi 45 ambazo zinaratibiwa na Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi. Makala haya haitoweza kuangalia mifuko yote hiyo bali tutatazama mifuko inayohusiana na utoaji mikopo moja kwa moja kwa wajasiriamali kwa mfano;
1. Mfuko wa Rais wa Kujitegemea (Presidetial Trust Fund –PTF). Mfuko unatowa mafunzo, mikopo na kufanya tafiti. Ni wazo zuri sana kuwa na mfuko namna hii hata hivyo huduma yake ya mikopo inaweza ikawa sio jumuishi au rafiki kwa waislam iwapo kuna riba ndani yake. Tovuti ya mfuko kwa sasa inaonesha aina za mikopo, masharti na kiwango cha mikopo lakini ipo kimya kuhusu tozo au riba yoyote inayotozwa na mfuko. Suali muhimu ni je mfuko huu unatozza riba kwa mikopo yake au la? Ikiwa inatoza basi ni wazi kuwa sio rafiki kwa waislam kwa kuwa kwa waislam riba imekatazwa. Ikiwa hamna riba, hii itakuwa ni mfano mmoja unaodhihirisha kuwa inawezekana kutowa mikopo bila riba na hivyo harakati za mfuko zinahitaji kupongezwa kwa kuwa jumuishi.
2. Mfuko wa Maendeleo ya Vijana (Youth Development Fund –YDF), Mfuko wa Maendeleo ya Wanawake (Women Development Fund –WDF) na Mfuko wa Taifa wa Kuendeleza Wajasiriamali Wananchi(National Entrepreneurship Development Fund –NEDF). Kimsingi fikra ya kuwa na mifuko hii ni nzuri mno. Hatahivyo, mikopo yake hutolewa bila riba? Ikiwa ni mikopo yenye riba au tozo, hiyo ni mushkeli mkubwa kwa waislam na hivyo kutonufaika ipasavyo na mifuko hiyo.
Changamoto na tatizo la riba lipo katika mifuko mingine inayoratibiwa na baraza. Kadhalika, baraza katika utekelezaji wa majukumu yake linaweza kutowa mkopo kwa mtu au shirika kwa mujibu wa masharti waliyojiwekeya. Je mikopo hiyo ina riba au la?
Kimsingi, baraza katika kutekeleza majukumu yake ni muhimu mno kuzingatia ujumuishi wa taratibu za mikopo ili baraza hili liwe na manufaa wa watu wote.
MCHANGO WA CIFCA
Waislam baada ya kutambuwa changamoto zilizopo katika sekta ya fedha na uchumi, waliaamuwa kuanzisha chombo chao chenye lengo la kushauri na kufunza yoyote yule ambaye angependeleya kufuata mfumo wa fedha na uchumi usiohusisha suala la riba. Kadhalika, chombo hicho kinaendeleya kutowa elimu kwa waislam juu ya tatizo la riba katika mikopo mbalimbali ikiwa na lengo la kuhadharisha na kuonesha njia mbadala.
Hivyo, ni muhimu sana hususani sekta ya umma kushirikiana na chombo hiki nchini ili mikopo inayotolewa na taasisi za serikali na mifuko ya baraza la taifa iweze kunufaika na wataalamu bobezi wa masuala ya fedha na uchumi waliopo katika chombo hicho na hivyo kuongeza kasi juhudi za baraza. Itambulike ya kwamba, taratibu zisizo na riba ni jumuishi kwa kila mtanzania na sio kwa manufaa ya waislam peke yao.
Kadhalika nitoe wito kwa taasisi binafsi za fedha na utoaji mikopo, kutambuwa kuwa lipo kundi kubwa la watanzania ambao hawafurahishwi na hawaridhii miamala ya riba kabisa na sio suala la riba kubwa au ndogo. Riba yote iwe ndogo au kubwa, haifai. Kwa rehema zake Mola ametuwekeya njia nyingi ambazo zinaiwezesha taasisi kufanya biashara na kupata faida isiyokuwa riba. Hivyo, wachukuwe fursa inayopatikana kwa kuwepo kwa CIFCA nchini ili kuweza kushauriwa namna ya kufanya ili waweze miamala sahahi na kutowa huduma zisizokuwa na riba kwa manufaa ya watanzania wote. Jambo hili linawezekana iwapo taasisi husika itakuwa na utashi thabiti na kufuata maelekezo ya wataalamu wa CIFCA katika kuepukana na Riba pamoja na vipengele vingine ambavyo ni vya kinyonyaji.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment