Pages

Wednesday, August 19, 2020

MATATIZO YA KIUCHUMI (ECONOMIC PROBLEM)

Nchi zote duniani hufanya juhudi kubwa katika kujenga uchumi imara na maendeleo kwa watu wake. Nimeeleza katika makala iliyopita mitazamo miwili tofauti kuhusu suala la maendeleo. Kujenga uchumi imara na kuleta maendeleo iwe kwa misingi ya kiislam au vinginevyo ni kazi ngumu na yenye kuhitaji umakini mkubwa kwa upande wa viongozi na wanaoongozwa. Si jambo la viongozi pekee kusema hiki na hiki tunachofanya ndio maendeleo au ndio ukuaji wa uchumi. Ikitokeya hivyo, wananchi wana kila sababu ya kuhoji aina hiyo ya maendeleo inayosemwa na viongozi wao. Na jambo hili limekuwa likijitokeza mara kadhaa kwa sababu mbili; Ya kwanza, kukosekana ushirikishwaji wa wananchi katika majadiliano ya maendeleo wayatakayo na uchumi imara wanaoutaka (lack of public participation). Je watendaji wa serikali wanakusanya maoni yetu na kuyafanyia kazi? Ya pili, tabiya ya viongozi na wanasiasa kuhodhi maamuzi ya matumizi ya rasilimali mbalimbali katika maeneo yao (dominance of political elite in decision making on resource utilization). Mambo haya yanahitaji kusahihishwa. Ili kufanikiwa katika usahihishaji wa mambo haya, tunahitaji kujiuliza tatizo au matatizo ya kiuchumi yanayowakabili watu wetu ni ya sampuli gani? Wachumi kama Lionel Robins waona kuwa tatizo la kiuchumi la watu wetu chanzo chake ni uhaba wa rasilimali (scarcity of resources). Wanamahitaji mengi lakini rasilimali ni chache ili kukidhi mahitaji hayo. Kwa upande wa wachumi wa Kiislam, tatizo la kiuchumi linalowakabili watu wetu linachukuwa sura zifuatazo: 1. KUKOSEKANA KWA FURSA SAWA (EQUAL OPPORTUNITIES). Binadamu ni viumbe vya Allah na wote wanahadhi kwa ubinadamu wao. Wote wana mahitaji sawa ya msingi katika kuendesha maisha yao ya kila siku. Wanahitaji kula, kunywa, kupata elimu, kupata ajira, kupata matibabu, kupata fursa za kujiongezeya mapato, kugombeya nafasi za uongozi, kutowa maoni na ushauri, kudai haki katika vyombo vya sheria n.k. Tatizo la kiuchumi kwa watu wetu hujitokeza pale mamlaka fulani haitowi fursa sawa kwa watu wote kujipatia mahitaji yao. Tulieleza wiki iliyopita mifano kadhaa kuhusu fursa za mikopo kutoka Baraza la Uwezeshaji Kiuchumi ambazo haziwapi fursa waislam kunufaika kutokana na uwepo wa Riba katika mikopo hiyo pamoja na kuwa sehemu ya fedha zao ndio zinazoendesha mifuko hiyo kwa kupitiya kodi mbalimbali. Katika fursa za ajira serikalini, sauti za waislam wamekuwa zinalalamika kuwa ni waislam wachache mno wanaopewa fursa hizo. Kadhalika katika fursa za elimu ya juu, kuna malalamiko kuwa waislam ni mdogo kuliko wa dini nyingine. Kwa ujumla inapotokeya kuwa watu hawana fursa sawa za kujipatiya mahitaji yao, hili ni tatizo ambalo linahitaji umakini mkubwa kulitatuwa na inawezekana. Sio mambo ya kupuuza bali kuyafanyia kazi kwa umakini mkubwa. 2. UBORA WA MAISHA ( QUALITY OF LIFE). Binadamu kwa uhalisia wake ni mjumuiko wa kiwiliwili na roho. Hivyo, ubora wa maisha ya binadamu upo katika kujengewa uwezo wa kiimani (spiritual) na uwezo wa kuyamudu mazingira yake (materials). Tatizo la kiuchumi lipo katika kutafuta njia maridhawa zenye kuweka uwiano baina ya mambo haya mawili ili binadamu huyu aweze kufikiya kilele cha kuwa na utu na vitu. Sera za kiuchumi zenye kujenga fursa za kuwa na vitu zinapelekeya watu kuwa mtu-vitu (materialist). Athari yake ni kuwa na ongezeko la wizi, ongezeko la rushwa, ongezeko la dhuluma n.k Na sera zenye kujenga fursa za kuwa na imani zinapelekeya kuwa na watu waliojitenga na ulimwengu wao (spiritualist). Athari yake ni kuwa na watu wanaojitenga na kufanya kazi n.k Mambo haya mawili yanahitajika kwa binadamu ili kuwa kamilifu kama alivyoumbwa na Mola wake, awe na utu na vitu kwa ustawi wa ubinadamu na mahitaji yake. 3. UADILIFU NA HAKI. Tatizo la mwisho la kiuchumi kwa mtazamo wa Kiislamu ni namna gani ya kumlinda mtu mwenye rasilimali yake iwe kipawa, maarifa au kitu dhidi ya wale ambao wanataka kumnyonya au kumpokonya au kumdhulumu jambo ambalo mwisho wako litaathiri ubora wa maisha yake na kukosekana kwa fursa baina ya wananchi. Kwa mfano, kuna wananchi wengi mno ambao wanamiliki ardhi lakini hawana hati miliki za viwanja hivyo. Wapo katika hali ya hatari inayoweza kupelekeya kupoteza mali zao kwa kudhulumiwa na wananchi wenzao au hata na watumishi wa serikali wasiokuwa waadilifu. Mfano wa pili ni utaratibu wa kuwa ardhi yote ni ya serikali na mwenye hati amekodi tu (leasehold) unaweza kuwaweka wananchi wengi katika hatari ya kupoteza mali zao baada ya muda wa kukodi kuisha (lease) na ikawa yule aliyekodishwa au mwenye hati hiyo hakuomba kuendeleya kuikodisha ardhi hiyo (lease renewal) ndani ya muda uliowekwa. Jambo hili sio la kufikirika bali yametokeya kwa baadhi ya wananchi wa Kenya ambao walijikuta nyumba zao zikibomolewa katika mji wa Nairobi na wamiliki wapya kwa kuwa hawakurenew hati zao! Wakati huo huo baadhi ya wananchi wenzao hati zao ni za kudumu na sio kukodishwa (freehold). Kwa upande wa pili, ni tatizo la kiuchumi na kijamii iwapo sheria zetu hazikidhi aina mbalimbali za miamala au ufanyaji wa biashara. Kwa mfano biashara ya bima ya Kiislam, sheria na kanuni zilizopo hazikidhi matakwa ya biashara hiyo na kuwa kanuni mpya zinahitajika. Ukosefu wa kanunni hizo mpya zimepelekeya kukosekana bima ya kiislam nchini Tanzania. Hivyo baadhi ya wananchi wananufaika na huduma za bima na kulipwa fidia wakati wa majanga na sehemu ya wananchi wanakoseshwa kupata huduma hiyo kwa sababu ya msingi-nayo ni kuwa bima zilizopo zinaenda kinyume na mafunzo ya dini yao! Kwa upande mwingine, sheria zenye kuingiliya haki ya umiliki mali zinahitaji mabadiliko. Kwa upande wa vyombo vya mahakama lazima viwe uwezo mkubwa wa kusikiliza kesi kwa wakati na haraka ili kila mwenye haki yake aweze kuipata na kunufaika. Hivyo, ni suala la msingi kuwa sera, sheria na vyombo vya mahakama vinasimama katika uadilifu na haki. Mwenyezi Mungu anasema "Enyi mlio amini! Kuweni wenye kusimamisha uadilifu...(4:135). Kwa kuhitimisha, matatizo yetu ya kiuchumi si uhaba wa rasilimali peke na wingi wa mahitaji peke yake bali pia ukosefu wa fursa sawa, ubora wa maisha yenye uwiano baina ya utu na vitu na ukosefu wa uadilifu na haki.

No comments:

Post a Comment