The primary purpose of this blog is to share latest information, opinions, exchange knowledge and expertise on the field of Islamic Finance from different perspectives. The secondary purpose is to share opinions and key development of Islamic Banking and Islamic insurance in Tanzania.
Wednesday, August 5, 2020
UCHUMI JUMUISHI
Maendeleo ya kiuchumi ni eneo muhimu baada ya yale ambayo tuliyaeleza wiki iliyopita. Katika hotuba ya bajeti ya wizara ya fedha mwaka huu, Waziri wa Fedha alibainisha dhamira ya serikali kuwaleteya wananchi maendeleo ya kiuchumi na kuwajumuisha wananchi katika maendeleo ya kiuchumi.
Mikakati kadhaa kila mwaka huwekwa ili kufikiya azma hii. Katika yale ambayo Waziri alibainisha kwa mfano ni kufutwa kwa ada na tozo za kero ili kuboresha mazingira ya kufanya biashara na kuwekeza hapa nchini. Uwekezaji katika miundombinu wezeshi kwa shughuli za uzalishaji mali na biashara ili kukuza uchumi, kuendelea kuorodhesha Hatifungani zake katika Soko la Hisa la Dar es Salaam; na kutoa elimu kwa umma ili kuhamasisha ushiriki wao katika kuwekeza kwenye Hatifungani na Dhamana za Serikali, kusimamia na kuboresha sekta ya fedha; kuongeza upatikanaji wa huduma za msingi kama vile afya, elimu, maji na umeme hususan maeneo ya vijijini; na kuendelea kutekeleza Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini kupitia Mfuko wa Maendeleo ya jamii (TASAF) ili kuongeza kipato chao na kuwawezesha kupata mahitaji ya msingi na kadhalika.
Je mikakati hii inawapa fursa sawa wananchi kujumuika kwa katika kuziendea fursa za uchumi? Jawabu ni ndio na hapana! Ili kufahamu hoja za jawabu hii kwanza tujiulize ni nini uchumi jumuishi ambao wachumi katika karne hii wanaona kuwa ni njia muwafaka ya kuhakikisha uchumi unakuwa vizuri na kuwa imara.
UCHUMI JUMUISHI (INCLUSIVE ECONOMY).
Ukiwauliza watu wa kawaida nini uchumi jumuishi watakuwa na jawabu tofauti na hilo pia lipo kwa upande wa wachumi. Wapo wanaona kuwa uchumi jumuishi ni ule ambao watu wanafursa sawa ya kupata ajira yenye hadhi na kipato halali. Ni uchumi ambao kila mwananchi anahusishwa katika fursa zilizopo za kupata kipato na anaweza kuziendeya fursa hizo bila kikwazo chochote iwe dini au kabila au eneo alilopo na kadhilika. Ni uchumi ambao fursa haziwapendelei watu fulani tu iwe kwa utajiri wao au kwa dini zao au kwa uanachama wao nakadhalika bali kila mtu anaweza kunufaika kikamilifu na fursa zilizopo.
Tafsiri moja wapo ambayo inanivutiya zaidi ni ile inayosema kuwa uchumi jumuishi ni ule ambao unawajali watu wote kwa mujibu wa mitazamo yao ya kiuchumi ( inclusive economy as the one that support all people from their economic standpoint).
Baada ya kufahamu maana ya uchumi jumuishi, je hatuwa hizi zilizoainishwa na Waziri ni hatuwa zenye kujenga uchumi jumuishi?
SIFA YA UCHUMI JUMUISHI NA HALI YETU.
Wachumi wamebainisha vigezo au sifa kadhaa za uchumi jumuishi kama vile; ushiriki wa wananchi (participation), usawa wa fursa mbalimbali (equity), kuongezeka kwa mapato (growth), endelevu (sustainable) na imara (stability).
Ukitazama sifa hizi na ukilinganisha na hatuwa ambazo waziri amezibainisha utaona kuwa zipo ambazo zimekidhi sifa hizo kama vile kufuta ada na tozo zenye kero, kuwekeza katika miundombinu, upatikanaji wa huduma za msingi,kunusuru kaya masikini na kadhalika. Na kwa upande mwingine, kwa mtazamo wa kiuchumi wa kiislamu, baadhi ya hatuwa zilizotajwa sio jumuishi kikamilifu na hazitowi fursa sawa kwa wote. Kwa mfano, kuoridhesha hatifungani na dhamana za serikali zinazolipa riba.
HATIFUNGANI NA DHAMANA ZA SERIKALI.
Waziri amesisitiza kuwa serikali itatowa elimu kwa umma ili kuhamasisha ushiriki wao katika au kununuwa au kuwekeza kwenye Hatifungani na Dhamana za Serikali. Kimsingi, serikali huhitaji fedha kwa ajili ya shughuli zake mbalimbali za kuwatumikiya wananchi. Na njia moja maridhawa ni kufanya biashara na wananchi wao, kwa maana ya kuwataka wawekeze katika hatifungani na dhamana zake ili wapate faida na kuongeza kipato chao na huku fedha hizo zinaenda katika kuimarisha miundombinu au huduma muhimu kwa wananchi. Hivyo wananchi wananufaika pande zote mbili.
Dosari iliyopo kwa mtazamo wa Uchumi wa Kiislamu ni kuwa hatifungani na dhamana za serikali zimetengezwa katika muundo ambao serikali wanauza hela kwa hela au kitaalamu inakopa kwa wananchi wake na kuwalipa na riba (interest). Hapa kuna tatizo la muundo (structural fault). Nini tatizo? Muundo huu unawanyima na kuwakosesha fursa sawa sehemu ya wananchi hususani waislamu katika kushiriki katika kufanya uwekezaji kwa kupitiya serikali yao kwa kuwa wao, HAWARUHUSIWI kukopa au kukopesha kwa riba au kuuza hela au kukodisha hela kwa hela!
Riba ni dhambi kubwa sana katika Uislamu. Ubaya wake umefananishwa na kutangaza vita na Mwenyezi Mungu au kufanya tendo la ndoa na mama yako mzazi. Anayekula riba ataingiya motoni isipokuwa atakapo tubiya na kuachana na riba. Kwa kutolifahamu jambo hili, serikali sio tu haitoweza kupata fedha za kutosha kutoka Waislam wanaofuata dini yao na Waislamu hawatoweza kupata kipato cha ziada. Hivyo, serikali inaumiya na wananchi hawa wanakosa fursa ambayo wenzao wengine wanaipata!
Lakini baya zaidi ni kuwa, serikali inapolipa riba kwa wale ambao watawekeza katika hatifungani na dhamana hizo kwa kuwa dini zao haziwazuii kukopesha kwa riba itakuwa inatumiya kodi zetu sote kuwanufaisha kwa malipo ya riba baadhi tu ya wananchi! Hali hii inadhihirisha wazi kuwa muundo wa serikali wa kukopa kwa riba kwa kuuza hatifungani na dhamana (Treasury bills and treasury bonds), sio jumuishi kwa wananchi wote. Ni muundo unaowabaguwa waislamu kwa kuwafanya wasishiriki katika kufanya 'biashara' serikali na kupata faida ya halali. Ni muundo ambao inahitaji kufikiriwa upya ili kutafuta muundo mwingine ambao utaiwezesha serikali kupata hela au kukidhi mahitaji yake na wananchi kuwekeza na kupata faida halali. je ipo njia mbadala?
NINI CHA KUFANYA?
Njia tulioieleza hapo awali ya kukopa kwa riba ni kongwe na imekuwa ni ya mazoeya lakini ukweli ni kuwa sio shirikishi kwa wananchi wote na ni yenye kubaguwa waislamu. Wachumi wa Kiislamu, wameshapendekeza miundo mengine ambayo serikali inaweza kupata hela au ukidhi mahitaji yake bila ya kutumiya mkataba wa kukopa kwa riba na badala yake kutumiya mikataba mingine kama vile ya mauziano (sales) au kukodisha (leasing) au kushirikiana katika faida na hasara (partnership). Jina maarufu la njia zenye kufuata mikataba hii ni Sukuk. Zipo Sukuk aina nyingi na zenye kuundwa kwa mikataba mbalimbali lakini sio mkataba wa kukopa (loans contract). Njia hii y Sukuk, imeshatumika nchi kadhaa ikiwemo Afrika Kusini, Nigeria, Gambia, Senegal, Sudan na nchi nyingine.
Miundo hii (Sukuk) inayowafikiana na kanuni za kibiashara za Kiislamu hazibagui watu wa dini nyingine kwa kuwa hazipingani na mafunzo ya dini hizo. Waislamu na wasiokuwa waislamu wanaweza kushiriki kwa usawa.
Je njia hizo zinawezesha wananchi kupata faida? Ndio. Kwa mfano, serikali inataka fedha kwa ajili ya kununuwa mitambo ya Umeme wa Stigler's Gorge ili kuzalisha umeme nchini. Ili kukidhi haja hii serikali kwa kupitiya bank kuu inakaribisha wananchi kuchanga fedha ambazo zitatumika kununuwa mitambo hiyo kwa bilioni 100 kwa mfano, na serikali itaahidi kununuwa mitambo hiyo kutoka kwa wananchi kwa Bil 105 na wananchi hao watalipwa ndani ya mwaka au miaka mitatu na kadhalika kulingana na kila mmoja alivyochangiya na gawio la faida. Kwa utaratibu huu, haya ni mauziano kwa faida na sio kukopeshana. Hii ni biashara halali ya mali kwa fedha na sio biashara haramu ya fedha kwa fedha. Hii ni njia moja tu katika njia nyingi zilizobuniwa na wachumi waislam katika kuiwezesha serikali kupata mahitaji yake (financing government deficit budget) ambayo waislam na wananchi wote kwa usawa wanaweza kushiriki na kuhimizana kushiriki kikamilifu na kuiondoleya serikali kazi ya ziada katika kuhamasisha.
Hivyo, jambo hili linawezekana na wapo wataalamu wa kutosha duniani wa kuishauri serikali katika kuweka muundo ambao unaepukana na riba. Kinyume na hivi, waislam wanasikitika mno kuona matangazo ya serikali yanahamasisha kununuwa hatifungani na dhamana zake kwa njia ya riba ilhali zipo njia mbadala zisizo na riba ambazo na wao wanaweza kushiriki bila kuvunja kanuni za dini yao. Waislamu wanahuzunika kuona serikali itatumiya kodi zao kulipa riba kwa baadhi ya wananchi na kuwanufaisha watu wachache tu. Ili kutuondoleya masikitiko haya na huzuni hizi, tunaiomba kwa heshima kubwa serikali yetu sikivu ione kuwa kuna haja sasa ya kubuni njia mbadala ambazo zitawapa wananchi wote fursa sawa ya kushiriki katika kuiwezesha serikali kupata mahitaji yake na wananchi kupata fursa ya kupata kipato cha halali.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment