Pages

Monday, November 20, 2023

RIBA, DINI NA SIASA.

Moja katika mambo makubwa ya kiuchumi ambayo baadhi ya waislam hawajaweza kufahamu ni iwapo suala la riba ni suala la dini au sio la kidini? Je ni suala la kisiasa tu ambalo halifungamani na dini yoyote? Hivi kukubali uwepo wa riba katika uendeshaji wa uchumi Tanzania ni suala la kisiasa tu bila mfungamano na dini? Mara kadhaa tumewasikia baadhi ya Waislam pale tunapoinasihi na kuiomba serikali itazame mbadala wa kutoza na kukopa kwa riba na taasisi zake zitazame mbadala wa kukopesha kwa riba, ndugu zetu wanatujibu kuwa serikali haina dini. Wakimaanisha kuwa kutoza riba sio suala la kidini bali la kisiasa na uchumi tu. Kadhalika siasa zote ulimwenguni hufuata dini kwa kiwango tofauti na kwa utambulisho tofauti hata hiyo ambayo yasemwa kuwa serikali ya kisekula, lakini ndani yake kuna mambo kadhaa ambayo yametokana au yanafuata dini fulani. Sasa ukitazama mafunzo ya dini mbili kuu duniani; Uislam na Ukiristo utaona kuwa jambo la kuwepo au kutokuwepo kwa riba katika uendeshaji wa nchi sio suala ka usekula bali kuna kila tashwishi ya msukumo wa mafunzo ya dini. RIBA KATIKA UKRISTO. Katika ukristo riba inakubalika kwa ujumla wake. Kwa undani, kuna namna mbili ya kuitazama riba: 1. Riba katika mkopo wa masikini. Agano la kale lina maandiko kadhaa ambayo wataalamu wa biblia wanakubaliana kuwa riba imekatazwa kwa ndugu yako katika Imani ambaye ni masikini. Katika kitabu cha Kutoka 22:25 “Ukimkopesha mtu aliye maskini, katika watu wangu walio pamoja nawe; usiwe kwake mfano wa mwenye kumdai; wala hutamwandikia riba.” Kemeo juu ya watu wanaowatoza riba masikini linabainishwa katika Mithali 28:8 “Yeye azidishaye mali yake kwa riba na ujambazi, Humkusanyia mtu awahurumiaye maskini.” Ikimaanisha kuwa hamna manufaa yoyote ayapatayo na mwisho wake mali hiyo itarudi kwa masikini. Lakini akikopesha bila riba malipo yake yapo kwa Mungu. Hata hivyo, katika Nehemia 15: 10 inasema "Na mimi pia, na ndugu zangu, na watumishi wangu, twawakopesha fedha na ngano ili kupata faida? Tafadhali na tuliache jambo hili la riba." Kwa mujibu wa biblia, watu watendao haki na kutenda ya halali wanasifa kadhaa na moja wapo "ambaye hakumkopesha mtu ili apate faida, wala hakupokea ziada ya namna yo yote; naye ameuepusha mkono wake na uovu, na kufanya hukumu ya haki kati ya mtu na mwenzake;" Ezakiel: 18: 8. Ukiondoa sehemu chache zinazohusu masikini, vitabu vingine vya biblia havioneshi kuwa kutoza riba kusifanywe kwa masikini bali kwa wanaisraili wote. Kwa mujibu wa agano la kale, wale wote walioshindwa kulipa watapaswa kusamehewa kila mwaka baada ya miaka saba. Kumbukumbu la Torati 15:1-2 “Kila miaka saba, mwisho wake, fanya maachilio.Na jinsi ya maachilio ni hii, kila mkopeshaji na akiache alichomkopesha mwenziwe, wala asimlipize mwenziwe wala nduguye; kwa kuwa imepigwa mbiu ya maachilio ya Bwana.” 2. Riba katika mkopo wa asiyekuwa masikini. Kwa upande wa agano jipya, tunakutana na maandiko ambayo yanadaiwa kuwa yanaashiria kufaa kutoza na kupokea riba japokuwa haioneshi wazi kama ni kwa wenye uwezo tu au hata masikini pia. Kwa mfano; katika kisa cha talanta katika Mathayo 25:27 au Luka 19:11-19 ambacho watetezi wa riba wanapenda kutumia, Yesu anakisimulia kuwa “Akaja na yule aliyepokea talanta moja, akasema, Bwana, nalitambua ya kuwa wewe umtu mgumu, wavuna usipopanda, wakusanya usipotawanya, basi nikaogopa, nikaenda nikaificha talanta yako katika ardhi; tazama, unayo iliyo yako. Bwana wake akajibu, akamwambia, Wewe mtumwa mbaya na mlegevu, ulijua ya kuwa navuna nisipopanda, nakusanya nisipotawanya; basi, ilikupasa kuiweka fedha yangu kwa watoao riba; nami nikija ningalipata iliyo yangu na faida yake.” Kwa kupitia maneno haya, wakiristo wengi wamesimama kuwa unaweza kupokea na kutoza riba kwa kuwa Yesu katika kisa hiki hakukemea riba. Hatahivyo, wasomi wengine wa wabiblia hawaoni kuwa kisa hiki kinatoa uhalali wa riba kwa sababu katika Luka 6: 34-36 unakutana na maneno ya Yesu akiagiza wafuasi wake kuwa wakikopesha wasitake kupata ziada / riba; “Na mkiwakopesha watu huku mkitumaini kupata kitu kwao, mwaonyesha fadhili gani? Hata wenye dhambi huwakopesha wenye dhambi, ili warudishiwe vile vile. Bali wapendeni adui zenu, tendeni mema, na kukopesha msitumaini kupata malipo, na thawabu yenu itakuwa nyingi; nanyi mtakuwa wana wa Aliye juu, kwa kuwa yeye ni mwema kwa wasiomshukuru, na waovu. Basi, iweni na huruma, kama Baba yenu alivyo na huruma.” Pamoja na kuwepo tafsiri na uelewe tofauti, kwa uhalisia ni jambo dhahiri kuwa wakristo wengi wanapokea na kutoza riba katika mikopo kwa kutegemea Mathayo kuliko Luka. Na wengine wanaona kuwa tatizo lililopo ni suala la kiwango gani kinafaa? Lakini sio riba yenyewe. RIBA KATIKA UISLAM. Katika Uislam, katazo la riba lipo wazi zaidi katika Quran na katika Hadithi za Mtume Muhammad saw. Wanazuoni wa Uislam wanakubaliana kuwa Riba yenyewe bila kujali masikini au tajiri ni chukizo mbele ya Mungu na ni dhambi yenye kuangamiza. Katika Quran, amri inatolewa kwa waumini “ Enyi mlioamini, Muogopeni Allah na wacheni chochote katika riba ikiwa ni waumini wa kweli” (Baqara: 278). HITIMISHO. Kwa kumalizia makala haya, pamoja na kuwepo kwa tofauti ya wanazuoni wa biblia kuhusu msimamo wa biblia kuhusu Riba, uhalisia ni kuwa wakristo wengi wanaona kuwa riba inakubalika na sio tatizo katika Imani yao. Uislam na wanazuoni wake wanakubaliana kuwa Riba katika aina zake zote iwe katika mkopo au nyingine haifa, ni dhambi kubwa. Baina ya Imani hizi mbili, siasa ya mataifa mbalimbali ukiondoa nchi kama ya Sudan na Iran ambazo zinafuata uchumi wa Kiislamu na hivyo kuharamisha riba, nchi nyingi zinaruhusu miamala ya riba. Kuna sababu mbalimbali zinazopelekea nchi za waislam wengi kuwa na mfumo wa riba, kubwa katika sababu hizo ni kukosekana uhuru kamili wa sera za kifedha (monetary sovereignity), athari za fikra za kimagharibi na ukoloni, kutofahamika ipasavyo mafunzo ya Uislam, Sheria zinazozuia dola kufuata mafunzo ya dini kama vile Uturuki nakadhalika. Kwa upande wa nchi za magharibi na kikristo, ni dhahiri kuwa msimamo wa ukristo kuruhusu riba ni moja ya sababu za kuwa na mfumo huo katika nchi zao. Sioni kwa sababu gani ndani ya dola ya Vatican na benki ya Vatikan inatoza riba iwapo Kanisa katoliki lingekuwa na mafunzo ya uharamu wa riba. Sioni kwa sababu gani benki za kanisa Tanzania au kwingine na benki kadhaa zinazomilikiwa na wakristo zingetoza riba iwapo msimamo wa kanisa ungekuwa mmoja kuwa riba ni haramu. Sioni kwa sababu gani Kanisa na viongozi wake wangekaa kimya kuona serikali au taasisi zake za uwezeshaji zinakopesha kwa Riba kwa wananchi wakati mafunzo ya Kanisa hayaruhusu wakristo kukopa au kukopesha kwa njia ya Riba? Hivyo, kutoza au kuacha kutoza riba sio suala ambalo halifungamani na dini au utamaduni bali ni sehemu ya dini zetu pamoja na kuwepo tafsiri tofauti za uhalali wa riba katika biblia.Jambo linaloleta matumaini ni kuwa dini zote mbili zinaweza kuungana katika kukataza Riba na kushirikiana katika njia mbadala ili watu wote waishi katika mafunzo ya Mwenyezi Mungu. Hivyo, siasa safi na jumuishi, inapaswa kusimama katika msimamo wa riba / dini ambao unatujumuisha sote kuliko kutugawa. Hivyo, siasa safi na jumuishi, inapaswa kusimama katika sera za Kiuchumi na kifedha ambazo zinatujumuisha sote kuliko kutugawa.