Pages

Friday, November 14, 2014

MIFUKO YA PENSHENI KATIKA MIZANI YA SHARIA YA KIISLAM.

UTANGULIZI.

Baada ya hayo, nchini Tanzania kuna mifuko sita ya pension kwa ajili ya watumishi wa mashirika ya serikali, wafanyakazi wa serikali pamoja na wafanyakazi wa mashirika ya watu binafsi. Mashirika haya yameundwa kwa sheria maalum zilizopitishwa na bunge. Sheria husika zinayapa nguvu mifuko hiyo katika shughuli zake za kila siku china ya wizara husika ambazo zinasimamia mifuko hii. Chini ya wizara ya fedha kuna mfuko wa PSPF, PPF, GEPF, na ZSSF, china ya wizara ya kazi, ajira na maendeleo ya vijana upo mfuko wa NSSF na chini ya wizara ya serikali za mitaa upo mfuko wa LAPF.

Makala hii inalenga kuangalia nadharia ya mifuko ya pension, jinsi mifuko hii inavyofanya shughuli zake, umuhimu wake katika jamii, na uhalali au uharamu wa mifuko hii katika mizani ya Sharia tukufu ya kiislamu.

NADHARIA YA MIFUKO YA PENSION.

Mifuko ya pension ya wafanyakazi ilianzishwa mnamo karne ya 20, kufuatia hali ya wasiwasi waliyokuwa nayo wafanyakazi juu ya maisha yao ya baadae na familia zao inayoweza kusababishwa na mabadiliko mbalimbali kama vile kifo, kustaafu, kupata ajali kazini n.k hali ambazo zikijitokeza huziweka familia za mfanyakazi katika wakati mgumu kifedha kumudu mahitaji yao ya kila siku. (Gross 2000).

Serikali mbalimbali katika nchi za kibepari zikaona njia bora ya kupunguza wasiwasi huu ni kuwa na mifuko maalum ambayo mfanyakazi ataweka fedha kutoka katika mshahara wake na serikali au mwajiri atamwongezea ili iweze kumfaa siku za mbele yeye binafsi na/au familia yake pamoja na faida atakayogawiwa kutoka katika vitega uchumi vya mfuko husika.

Kulipa nguvu jambo hili, serikali mbalimbali zimeweka sheria maalum ili kuhalalisha na kuhakikisha kuwa wafanyakazi wanakuwa wanachama wa mifuko hii na kukatwa sehemu ya mishahara yao (kati ya 5% au 10%) na kuwalazimisha waajiri kuwachangia wafanya kazi wao (kati ya 10% au 15% kulingana na sheria ya mfuko husika). Kadhalika, sheria hizo zinawahakikishia wanachama kupata mafao yao na huduma mbalimbali chini ya taratibu zilizowekwa. Kwa mfano, NSSF imeundwa chini ya sheria namba 30 mwaka 1997, PPF chini ya mswada wa PPF no 14 (1978) na sheria namba 25 (2001), PSPF chini ya Public Service Retirement Benefits Act No.2 of 1999 na kadhalika.

SHUGHULI ZA MIFUKO YA PENSION.

Mifuko yote ya pension inategemea sana michango ya wanachama na waajiri wao katika kukuza mitaji kwa shughuli za uwekezaji na kuwa na fedha za mara moja ili kuwalipa wanachama walio chini ya mifuko hii chini ya utaratibu wa kuchukua michango ya wale wanaojiunga sasa kulipia mafao ya wale waliojiunga zamani. Kwa ufupi, mstaafu analipwa kile alichoweka kama mchango wake na mwajiri wake pamoja na ‘faida’ iliyotokana na uwekezaji wa fedha hizo katika miradi ya mfuko husika ndani ya muda wote alipokuwa kazini. (Spiceland et al)

Pamoja na hayo, mifuko hii imekuwa ikibuni taratibu mbalimbali za kinga ya jamii kufuatana na mabadiliko yanayojitokeza na kukabiliana na ushindani ili kuweza kuwavutia watu kuweka fedha za akiba chini ya bidhaa mbalimbali za mifuko hii.

Ukiacha michango ya wanachama, mifuko hii inatumia njia mbalimbali za uwekezaji ili kupata faida ambayo itatumika kujiendesha na kuwalipa wanachama chini ya taratibu mbalimbali za pension ( pension plans). Mifuko yetu hapa Tanzania, yote ina sera zake za uwekezaji (Investment policies) ambazo zinafanana hususan katika maeneo ya uwekezaji au vitega uchumi (investment portfolio).

Maeneo makuu matatu ya uwekezaji yanayotumiwa sana na mifuko hii;

1. Miradi yenye kipato maalum (Fixed Income assets).
Mifuko hii hununua dhamana za serikali (T/Bills na T/Bonds), dhamana za makampuni (corporate bonds), kuweka katika mabenki mbalimbali katika akaunti za muda (Fixed deposit account or call account), kukopesha makampuni makubwa (Corporate loans), wafanyakazi wake nakadhalika. Sifa kubwa ya uwekezaji huu ni kuwa makubaliano huwa chini ya mikataba ya riba. Hali halisi inaonyesha kuwa zaidi ya asilimia 68 ya fedha zote za mifuko hii huwekezwa katika utaratibu huu. (PSPF 65%, ZSSF 85%, PPF 54%, LAPF haikowazi, NSSF haikowazi, GEPT haikowazi). Katika hiyo asilimia 68, Bw. Peter Mhando anasema asilimia 41% ya fedha zote huwekezwa katika mabenki na dhamana za serikali.

2. Miradi ya Ujenzi, (Properties), mifuko hii huwekeza katika ujenzi wa nyumba za kuishi na za biashara (Residential and commercial buildings). Uwekezaji katika sekta ya ujenzi au majengo inachukua hadi asilimia 25%.(inategemea aina ya mfuko husika, kwa mfano ZSSF ni 3.36%). Uhalali wa kipato kinachotokana na uwekezaji huu inategemea kampuni au biashara za wale waliopangishwa na muundo wa mitaji (Capital structure) wa kampuni hizo. Kwa mfano, baadhi ya ofisi za majengo ya PPF na NSSF wamepangishwa benki za riba, makampuni ya bima, na makampuni yanayoendeshwa kwa mikopo ya riba n.k

3. Kuwekeza katika hisa za makampuni ya umma yalioorodheshwa katika soko la hisa (DSE). Mifuko ya pension nchini yamejiwekea kima maalum cha kuwekeza katika hisa za makampuni imara na yenye kuleta faida ambayo yameorodheshwa katika siko la hisa la DSM. Hata hivyo, kiwango cha uwekezaji katika hisa ni kidogo sana ukilinganisha na maeneo mengine. ( Kila kampuni inayosera yake ya uwekezaji inayoelekeza kiwango cha kuwekeza katika eneo hili.) Kama ilivyo uwekezaji katika ujenzi wa majengo ya biashara, uhalali wa faida itokanayo na hisa za makampuni inategemea aina ya kampuni husika na muundo wa mtaji wake. Kwa mfano, mifuko hii hununua hisa katika mabenki ya riba, makampuni ya bia, makampuni ya bima, sigara, nakadhalika. Bahati mbaya, sehemu kubwa ya uwekezaji katika hisa huwa katika hisa za makampuni haya.

Kwa ujumla hizi ndio njia kuu za kupata mapato au faida ambayo hugawiwa kwa wanachama au mapato haya ndio yanayolipia gharama mbalimbali za huduma itolewayo. Kadhalika, mifuko hii imeruhusiwa kukopa katika taasisi za fedha ili kumudu mahitaji ya shughuli zake mbalimbali.

Wachunguzi na wachambuzi wa mifuko ya pension nchini wanaona kuwa mifuko hii imekabiliwa na upungufu mkubwa katika njia za uwekezaji inazozitumia na namna ya uendeshaji. Bw. Philip Mpango, mchumi wa benki ya dunia, katika mahojiano yake na gazeti la EastAfrican amesema kunahitajika mabadiliko makubwa katika sheria ya mifuko hii hasa katika eneo la uwekezaji na miradi inayokubaliwa na mifuko ya pension. Hatahivyo, upungufu mkubwa unaoonekana ni ile hali ya mifuko hii kuhatarisha amana za wafanyakazi kwa kuamua kuwekeza katika sekta ya ujenzi na majengo ya kibiashara, miradi ambayo matunda yake huchukua muda mrefu na kuifanya mifuko ikose fedha kulipa mafao(Liquidity problems). Kwa mfano, NSSF na PPF imewekeza mabilioni ya shilingi katika miradi ya ujenzi wa nyumba Dar es salaam, Arusha, Dodoma na Mwanza. Waziri wa fedha, Mr. Mkulo amenukuliwa akisema kuwa mifuko mikubwa ya pension ipo katika matatizo makubwa kifedha. Ameitaja mifuko hiyo kuwa ni PPF, PSPF na LAPF, jambo ambalo litailazimu “... serikali kufidia hasara inayotokana na matatizo ya kifedha.” Ameongeza kusema “hali hii inaenda kinyume na dhamira ya serikali. Lengo la serikali ni kuhakikisha mifuko hii inakuwa na uwezo wa kifedha endelevu.”

Kadhalika, mifuko hii inalaumiwa kwa kutoa mikopo kwa wafanya biashara fulani na wanasiasa au hata vyama vya siasa. Baya zaidi ni kukaa na Tsh 622 billioni za wanachama bila kuwekezwa katika miradi (idle funds) hali inayopelekea manung’uniko na wanachama kupata faida ndogo wakati wa kuchukua mafao yao.

Mwisho, mifuko hii inahitaji kufanya mabadiliko ili kuwawezesha wafanyakazi kutumia amana walizoweka kama dhamana katika kupata mikopo kutoka katika taasisi za fedha. Vilevile, kuunda utaratibu maalum ambapo utawawezesha wachangiaji kuwa na uchaguzi wa maeneo ambayo wangependa mifuko hii iwekeze fedha zao na wao kupata gawio ambalo linawiana na imani zao pamoja na kuwa na uwazi kwa wanachama juu ya mwenendo wa mifuko husika.

FAIDA ZAKE KATIKA NCHI.

Utafiti wa kina na kisayansi unahitajika katika kutathmni mchango wa mifuko ya pension katika maendeleo ya Tanzania. Kinadharia, inaweza kusemwa kuwa mifuko hii ina faida kubwa katika kujenga uchumi wa nchi kwa kuwa ni inafanya shughuli ya kukusanya fedha ambazo zinaweza kutumika kama mtaji (Formation of capital) kwa taasisi na miradi mbalimbali ya kimaendeleo. Mifuko hii inatoa ajira kwa watu mbalimbali wanofanya kazi katika mifuko hii kadhalika watu wanopata ajira kutokana na miradi inayowezeshwa na mifuko ya pension. Kwa mwanachama, zipo faida mbalimbali kulingana na mfuko husika, kwa mfano mafao ya kustaafu kazini, mafao ya kuumia kazini, msaada wa mazishi (funeral grant), msaada wa huduma za afya (medical benefits), mafao ya uzazi (maternity benefits), na kadhalika. Bila shaka, mafao haya yanainufaisha jamii na kupunguza makali ya maisha pindi wanapostahili mafao hayo.

Hata hivyo, ulazima uliowekwa katika kuhakikisha kila muajiriwa (formal sectors) anakuwa mwanachama wa mifuko hii kwa kuchangia kima maalum moja kwa moja kutoka katika mshahara wake kunamkosesha muajiriwa manufaa ya jasho lake katika muda husika, uhuru wa maamuzi na matumizi ya kipato chake, kunapunguza uwezo wa kuyamudu mahitaji ya kila siku (purchasing power), kupunguza mori wa wafanyakazi na mzunguko wa fedha katika uchumi wa nchi

MIZANI YA SHARIA YA KIISLAMU JUU YA MIFUKO YA PENSION.

Ili kujua mtazamo wa sharia ya kiislamu juu ya mifuko ya pension, hatuna budi kuanzia katika kuangalia nadharia ya mifuko hii na lengo la sharia ya kiislamu. Sharia ya kiislamu ina malengo (maqasid sharia) makuu mawili, moja kuleta manufaa na la pili, kuondosha madhara. Lengo kuu katika haya malengo mawili ni kuondosha madhara (Relieving hardship takes precedence over promoting benefit). Kwa kuwa nadharia ya mifuko yote ya pension ni kumnufaisha mwanachama wake na kumkinga na hali ya wasiwasi juu ya matatizo yanayoweza kujitokeza kwa kukosa kipato wakati akiwa hana nguvu ya kufanya kazi au akiwa hana kazi, au akipata ajali kazini, au akifiwa na watu wa karibĂș na kadhalika. Hivyo, sharia ya kiislamu haina kipingamizi katika nadharia ya mifuko ya pension.

Pamoja na kuwa sharia inaunga mkono dhamira njema ya mifuko hii, mambo yafuatayo ni vyema yakazingatiwa ili uhalali wa mapato au faida itokanayo na mifuko hii kwa wanachama wake upatikane.

1. Wasilazimishwe wafanyakazi kuwa wanachama wa mifuko hii. Mwenyezi Mungu, amekataza watu kuwalazimisha wenzao kufuata dini yake seuze kufuata utaratibu huu? Juhudi ifanyike kuwaelimisha wafanyakazi umuhimu wake na yule atakayeridhika ajiunge na mfuko husika kwa hiyari yake. Kumlazimisha mtu aache sehemu ya ujira halali utokanao na jasho lake (forsake his current needs for unforeseable future needs) bila ridhaa yake kwa kisingizio kuwa kipato hicho kinahifadhiwa kimfae baadaye ni dhulma kubwa.

2. Waajiri wasilazimishwe kuchangia kwa ajili ya wafanyakazi wao. Waelimishwe umuhimu na uzuri wa kufanya hivyo na atakayekuwa na uwezo awe anawapa wafanyakazi wake kiasi anachoweza kama motisha ya juhudi au kazi nzuri inayofanywa na wafanyakazi wake. Kuwalazimisha waajiri watoe kiasi fulani kwa ajili ya wafanyakazi zaidi ya kile walichokubaliana na muaajiriwa ni kuwadhulumu waajiri hawo na kuwakatisha tamaa kwa kuwa sheria iliyopo haitambui uwezo wa muajiri kufanya hivyo.

3. Wafanyakazi wawe ni wawekezaji au wanahisa (Shareholders)katika mfuko wa pension husika. Na kila mmoja anapochangia iwe ni sawa na mtu anayenunua hisa katika shirika la biashara chini ya mkataba wa mudharaba.

4. Njia za uwekezaji (investment avenues) ziwe zinakidhi mahitajio ya sharia ya kiislamu kwa wale wanaotaka kipato chao kitokane na vyanzo halali kwa mujibu wa Sharia.

5. Hiyo basi, kuhakikisha jambo hili, iundwe bodi au kamati ya wataalamu wa sharia ya kiislamu wenye dhima ya kuelekeza na kuidhinisha uwekezaji wa amana za wanachama katika vitega uchumi halali na kwa uwazi.

SWALI LA MSINGI JUU YA KIPATO CHA MIFUKO HII YA PENSION ILIYOPO.

Ni muhimu kujiuliza, je? kipato apatacho mwanachama wa mifuko hii kutokana na kulazimika kuchangia kutoka katika mshahara wake na kile anachopewa na mwajiri na riba itokanayo na fedha hizo ni halali kwa matumizi yake?

Wanazuoni wa india wamejibu swali hili ya kwamba, kipato hicho ni sehemu ya mshahara wake na anaweza kutumia kwa matumizi yake na matumizi ya neno riba si sahihi katika jambo hili . Hata hivyo, fatwa hii haina uzito ukitazama vitega uchumi vya mifuko ya pension ya Tanzania na hata sehemu nyingine ulimwenguni. Kwa sababu hiyo, wanazuoni mahiri, wamekataza kuchukua ile riba kwa matumizi binafsi na hii ndio fatwa yenye nguvu kisharia ukizingatia aina ya mikataba inayotumika na chanzo cha faida inayotolewa. Hivyo, riba inayotolewa na mifuko hii, itolewe katika shughuli za jamii (charitable social activities).

Mwisho, wanazuoni wote wanakubaliana juu ya wajibu alionao mwanachama atakayekuwa anachukua mafao yake kutoa zakat wakati anapopokea fao lake iwapo mafao yake yamefikia kima cha nisaab ya fedha taslimu (Value of 85gram of Gold) na kutimiza mwaka mmoja.Wajibu huu wakutoa zakah ni pale atakapokuwa anachukua mafao yake na si kwa muda ambao fedha yake imekaa katika mfuko husika.


CHANGAMOTO NA NINI KIFANYIKE.

Ni wazi ya kuwa sisi kama waislamu nchini Tanzania tunalazimishwa na sheria zilizopo kushiriki katika mifuko hii na ni wajibu wetu ushiriki wetu uishie hapo. (yaani kwa kulazimishwa). Lakini je nini wajibu wetu katika mazingira haya? Kuacha hali hii iendelee au kufanya juhudi kuepukana na mfumo huu au kuanzisha mifuko ya kiislamu?

Mafunzo ya kiislamu yanamtaka Muislamu popote asiwe katika upande wa kuacha jambo baya liendelee hali yakuwa ni muislamu mwenye kufahamu wajibu na mwenye uwezo wa kubadilisha hali hiyo. Mtume s.a.w ametueleza wazi ya kuwa “atakayeona mmoja wenu jambo baya, alizuie kwa mikono yake akishindwa, kwa ulimi wake, akishindwa achukie kwelikweli moyoni mwake na (jambo hili la kuchukia tu) ni dalili ya udhaifu wa imani.” Historia ya kiislamu na muda wote wa kuwepo Uislamu haijapata kukosa watu waliotekeleza kauli hii kivitendo. Mfano uliodhahiri katika zama zetu, ni juhudi ya kuepukana na riba katika taasisi za fedha. Wanazuoni wa kiislamu na wataalamu wa masuala ya fedha wa kiislamu, wameweza kuonesha njia mbadala ya kuendesha shughuli taasisi za fedha bila riba,kufuatana na muongozo wa Sharia. Hivyo, wito wa kisharia kwa waislamu ni kutambua wajibu huu na kuutekeleza kivitendo kwa kuwa na mkakati.

Kwanza, kuwa na wajuzi waislamu wa kusimamia mifuko hii kwa kufuata sharia ya kiislamu, baada ya utafiti makini (feasibility study) juu ya vyanzo endelevu ambavyo vitaupa nguvu mfuko wa jamii au pension wa kiislamu (Islamic social security or pension fund), kuulinda kisheria na ndani ya jamii ili uweze kudumu bidhnillah.

Wamepata kusema wanazuoni ya kuwa muislamu anaruhusiwa tu kuishi katika mazingira yasiyo ya kiislamu (yenye dhulma mbalimbali) iwapo anatafuta namna bora ya kuhamia nchi ya kiislamu au anapambana na mfumo dhalimu uliopo ili kubadilisha mazingira hayo na kumfanya atekeleze Uislamu wake bila kizuizi katika kila nyanja ya maisha. Asipofanya moja kati ya haya basi anastahili kupata adhabu ya mola wake, kwa kauli ya Mtume s.a.w “Yule atakayejifananisha na watu fulani naye ni miongoni mwao.”

Wajibu wa muislamu katika kupambana na uovu au dhulma ameueleza kwa ufupi mmoja wa wanafikra wetu, Prof. Hamza Njozi katika moja ya maandiko yake pale aliposema, “It is socially and morally wrong to acquiesce to injustice. Muslims have the moral and political responsibility to expose and to fight against all forms of social injustice and discrimination even if their efforts would always end in failure. Heroic failure in fighting injustice is far better than success in entrenching an unjust order.” Maana yake ni kwamba “ kwa hakika ni jambo baya kimaadili na kijamii kushikamana na dhuluma. Waislamu wana wajibu kimaadili na kisiasa kudhihirisha na kupambana na aina zote za dhuluma katika jamii na ubaguzi hata ikiwa juhudi zao hazitofanikiwa. Kushindwa kishujaa katika kupambana na dhuluma ni jambo lililo bora sana kuliko kufanikiwa kwa kuimarisha mfumo dhalimu.”

Mwisho, tutahadhari na haya yafuatayo katika harakati dhidi ya uovu na dhulma kama alivyosema Mtume s.a.w katika hadithi mbalimbali;
• kutafuta maslahi binafsi badala ya maslahi ya ummah kwa ujumla,
• kuacha malengo kwa kughafilika baada ya kuwa na ujuzi,
• kuwa na tamaa iliyopindukia katika yale ambayo hatuna uwezo nayo kwa sasa,
• kujiepusha na unafiki na wanafiki miongoni mwetu,
• kubweteka,
• kuwa katika usingizini mzito (kufikiri bila kutenda) na
• Udhaifu wa imani.




No comments:

Post a Comment