Pages

Wednesday, August 26, 2020

JENGA UCHUMI WAKO BINAFSI

Tumezoea kusikia kuhusu kujenga uchumi wa nchi na kuleta maendeleo. Tunaambiwa kuwa uchumi unakuwa kila mwaka na hivyo maisha ya watu yanaimarika. Hali hiyo inaweza kuwa sahihi iwapo wewe na mimi tunajizatiti kujenga uchumi wetu binafsi. Na abadan ukuaji huo wa uchumi hautomnufaisha yule ambaye amekaa maskani asubuhi na jioni akizungumza kuhusu mechi au wanayosema wanasiasa majukwaani au wanayofanya wasanii au amekaa nyumbani na kutazama filamu mbalimbali au kucheza games za kieletroniki n.k Hivyo, ili uchumi wako binafsi uimarike lazima kila mmoja wetu ajizatiti katika mambo yafuatayo muda wote wa uhai wake. 1. Ajifunze misingi ya elimu ya biashara. Iwe mfanyabiashara au mfanyakazi, elimu ya biashara ni elimu muhimu sana kwa kila mmoja wetu. Unatakiwa ujuwe biashara ni nini? Namna ya kuweka mahesabu, namna ya kuuza bidhaa au huduma, namna ya kuzungumza na wateja, namna ya kupata mitaji, namna ya kujitangaza na namna ya kuibuwa mawazo ya kibiashara ambayo yatatatuwa tatizo la mtu au watu kwa njia ambayo watu hao watakauwa tayari kulipiya ili kupata ufumbuzi wako. Somo la biashara hufunzwa katika elimu sekondari kupitiya somo la commerce na book keeping. Kwa bahati mbaya, watu wanahiyari ya kuyawacha masomo hayo wanapoingiya kidato cha tatu. Kwa maoni yangu, ilipaswa kuwe na somo moja mjumuiko wa masomo haya ambayo iwe mtu ni wa arts au science ataendeleya kusoma ili kumjenga kujuwa namna biashara inavyopaswa kufanywa. Umuhimu wa somo hili ni kuhakikisha ya kwamba anayemaliza kidato cha nne awe anayomsingi imara wa kuweza kujiajiri na kujenga uchumi wake na wa familiya yake. Biashara tunazofanya kimazoea na kupitia ushauri wa rafiki badala ya wataalamu, hautoshi kukuimarisha kiuchumi. Hata ikiwa ulipitwa na masomo hayo, sasa hivi katika umri ulionao tenga muda wa kusoma maudhui fulani za somo la biashara na ufanyie kazi. Hatuwa hizi zitakuweka katika mstari wa kujenga uchumi wako. Soma sana vitabu au sikiza mazungumzo yanyolenga kukuongozea maarifa katika ufanyaji biashara iweya vitu au ya kutoa huduma (mwajiriwa) 2.Tumia muda wako vizuri. Muda ndio rasilimali kubwa aliyopewa mwanadamu na neema kubwa kabisa ni kuwa na imani/ tawheed. Kama muislam, ushapewa neema ya tawheed na kinachofuata ni kutumia rasilimali ya wakati vizuri. Wakati ndio uhai wenyewe. Ukitoka kazini au ukishafunga biashara yako jioni, jiulize maswali yafuatayo; kitu gani napaswa kufanya ili kuboresha utendaji wangu kazini au kuboresha biashara yangu? Watu wengi huwa hawana jawabu ya swali hili. Hiyo sio dosari. Dosari ni kuridhika kwa kukosa jawabu! Dosari ni kudhani kuwa hamna anayejuwa jawabu! Dosari ni kuifungiya ndani ya fikra zako na ukawacha mlango wa kutafuta ushauri kwa wengine. Imesemwa "washauri wenye ujuzi, utapata nuru ya maarifa yao." Hivyo badala ya kupoteza muda wako wa jioni ukishafunga kazi au kupoteza muda siku za week end, tumiya muda huo kujumuika na familiya yako na piya kukusanya maarifa mapya ili kuboresha zaidi. Hili ni jukumu lako la kila siku ili kujenga uchumi wako ambao utakuwa imara. 3. Weka malengo yako na ujilazimishe kuyatimiza. Ni muhimu uwe na malengo ya kukuza kipato chako kila mwaka. Iwe kwa kupitiya ajira au kwa kulima au kwa kuzalisha au kwa kufanya biashara ambazo zinaboresha maisha ya watu wengine. Tunaishi wakati ambo taarifa za watu wengine ni nyingi mno katika magazeti, mitandaoni na mitangazo. Taarifa hizi nyingine zinaweza kukupa maarifa na nyingine zinaweza kukutowa katika malengo yako. Hivyo ni muhimu ujilazimishe kuyafikiya malengo yako kila mwaka na usikubali kuondoka katika malengo uliyojiwekeya na kuishi katika malengo ya wengine. Sasa tupo katika mwaka mpya wa Kiislam, chukuwa kalamu na karatazi uandike kipato ambacho ungependa ukifikiye ifikapo mwisho wa mwaka na nini unapaswa kufanya ili kufikiya malengo hayo. Usipofanya hivyo, usilalamike pale gharama za maisha zinapoongezeka na wewe miaka nenda rudi umejifunga katika kipato cha miaka ya nyuma! Kila siku zinavyoenda unatakiwa ujenge uchumi wako au hali ya kiuchumi itakuwa na changamoto ya kutegemeya wengine. Weka malengo na kisha tekeleza peke yako au pamoja na wengine!

Wednesday, August 19, 2020

MATATIZO YA KIUCHUMI (ECONOMIC PROBLEM)

Nchi zote duniani hufanya juhudi kubwa katika kujenga uchumi imara na maendeleo kwa watu wake. Nimeeleza katika makala iliyopita mitazamo miwili tofauti kuhusu suala la maendeleo. Kujenga uchumi imara na kuleta maendeleo iwe kwa misingi ya kiislam au vinginevyo ni kazi ngumu na yenye kuhitaji umakini mkubwa kwa upande wa viongozi na wanaoongozwa. Si jambo la viongozi pekee kusema hiki na hiki tunachofanya ndio maendeleo au ndio ukuaji wa uchumi. Ikitokeya hivyo, wananchi wana kila sababu ya kuhoji aina hiyo ya maendeleo inayosemwa na viongozi wao. Na jambo hili limekuwa likijitokeza mara kadhaa kwa sababu mbili; Ya kwanza, kukosekana ushirikishwaji wa wananchi katika majadiliano ya maendeleo wayatakayo na uchumi imara wanaoutaka (lack of public participation). Je watendaji wa serikali wanakusanya maoni yetu na kuyafanyia kazi? Ya pili, tabiya ya viongozi na wanasiasa kuhodhi maamuzi ya matumizi ya rasilimali mbalimbali katika maeneo yao (dominance of political elite in decision making on resource utilization). Mambo haya yanahitaji kusahihishwa. Ili kufanikiwa katika usahihishaji wa mambo haya, tunahitaji kujiuliza tatizo au matatizo ya kiuchumi yanayowakabili watu wetu ni ya sampuli gani? Wachumi kama Lionel Robins waona kuwa tatizo la kiuchumi la watu wetu chanzo chake ni uhaba wa rasilimali (scarcity of resources). Wanamahitaji mengi lakini rasilimali ni chache ili kukidhi mahitaji hayo. Kwa upande wa wachumi wa Kiislam, tatizo la kiuchumi linalowakabili watu wetu linachukuwa sura zifuatazo: 1. KUKOSEKANA KWA FURSA SAWA (EQUAL OPPORTUNITIES). Binadamu ni viumbe vya Allah na wote wanahadhi kwa ubinadamu wao. Wote wana mahitaji sawa ya msingi katika kuendesha maisha yao ya kila siku. Wanahitaji kula, kunywa, kupata elimu, kupata ajira, kupata matibabu, kupata fursa za kujiongezeya mapato, kugombeya nafasi za uongozi, kutowa maoni na ushauri, kudai haki katika vyombo vya sheria n.k. Tatizo la kiuchumi kwa watu wetu hujitokeza pale mamlaka fulani haitowi fursa sawa kwa watu wote kujipatia mahitaji yao. Tulieleza wiki iliyopita mifano kadhaa kuhusu fursa za mikopo kutoka Baraza la Uwezeshaji Kiuchumi ambazo haziwapi fursa waislam kunufaika kutokana na uwepo wa Riba katika mikopo hiyo pamoja na kuwa sehemu ya fedha zao ndio zinazoendesha mifuko hiyo kwa kupitiya kodi mbalimbali. Katika fursa za ajira serikalini, sauti za waislam wamekuwa zinalalamika kuwa ni waislam wachache mno wanaopewa fursa hizo. Kadhalika katika fursa za elimu ya juu, kuna malalamiko kuwa waislam ni mdogo kuliko wa dini nyingine. Kwa ujumla inapotokeya kuwa watu hawana fursa sawa za kujipatiya mahitaji yao, hili ni tatizo ambalo linahitaji umakini mkubwa kulitatuwa na inawezekana. Sio mambo ya kupuuza bali kuyafanyia kazi kwa umakini mkubwa. 2. UBORA WA MAISHA ( QUALITY OF LIFE). Binadamu kwa uhalisia wake ni mjumuiko wa kiwiliwili na roho. Hivyo, ubora wa maisha ya binadamu upo katika kujengewa uwezo wa kiimani (spiritual) na uwezo wa kuyamudu mazingira yake (materials). Tatizo la kiuchumi lipo katika kutafuta njia maridhawa zenye kuweka uwiano baina ya mambo haya mawili ili binadamu huyu aweze kufikiya kilele cha kuwa na utu na vitu. Sera za kiuchumi zenye kujenga fursa za kuwa na vitu zinapelekeya watu kuwa mtu-vitu (materialist). Athari yake ni kuwa na ongezeko la wizi, ongezeko la rushwa, ongezeko la dhuluma n.k Na sera zenye kujenga fursa za kuwa na imani zinapelekeya kuwa na watu waliojitenga na ulimwengu wao (spiritualist). Athari yake ni kuwa na watu wanaojitenga na kufanya kazi n.k Mambo haya mawili yanahitajika kwa binadamu ili kuwa kamilifu kama alivyoumbwa na Mola wake, awe na utu na vitu kwa ustawi wa ubinadamu na mahitaji yake. 3. UADILIFU NA HAKI. Tatizo la mwisho la kiuchumi kwa mtazamo wa Kiislamu ni namna gani ya kumlinda mtu mwenye rasilimali yake iwe kipawa, maarifa au kitu dhidi ya wale ambao wanataka kumnyonya au kumpokonya au kumdhulumu jambo ambalo mwisho wako litaathiri ubora wa maisha yake na kukosekana kwa fursa baina ya wananchi. Kwa mfano, kuna wananchi wengi mno ambao wanamiliki ardhi lakini hawana hati miliki za viwanja hivyo. Wapo katika hali ya hatari inayoweza kupelekeya kupoteza mali zao kwa kudhulumiwa na wananchi wenzao au hata na watumishi wa serikali wasiokuwa waadilifu. Mfano wa pili ni utaratibu wa kuwa ardhi yote ni ya serikali na mwenye hati amekodi tu (leasehold) unaweza kuwaweka wananchi wengi katika hatari ya kupoteza mali zao baada ya muda wa kukodi kuisha (lease) na ikawa yule aliyekodishwa au mwenye hati hiyo hakuomba kuendeleya kuikodisha ardhi hiyo (lease renewal) ndani ya muda uliowekwa. Jambo hili sio la kufikirika bali yametokeya kwa baadhi ya wananchi wa Kenya ambao walijikuta nyumba zao zikibomolewa katika mji wa Nairobi na wamiliki wapya kwa kuwa hawakurenew hati zao! Wakati huo huo baadhi ya wananchi wenzao hati zao ni za kudumu na sio kukodishwa (freehold). Kwa upande wa pili, ni tatizo la kiuchumi na kijamii iwapo sheria zetu hazikidhi aina mbalimbali za miamala au ufanyaji wa biashara. Kwa mfano biashara ya bima ya Kiislam, sheria na kanuni zilizopo hazikidhi matakwa ya biashara hiyo na kuwa kanuni mpya zinahitajika. Ukosefu wa kanunni hizo mpya zimepelekeya kukosekana bima ya kiislam nchini Tanzania. Hivyo baadhi ya wananchi wananufaika na huduma za bima na kulipwa fidia wakati wa majanga na sehemu ya wananchi wanakoseshwa kupata huduma hiyo kwa sababu ya msingi-nayo ni kuwa bima zilizopo zinaenda kinyume na mafunzo ya dini yao! Kwa upande mwingine, sheria zenye kuingiliya haki ya umiliki mali zinahitaji mabadiliko. Kwa upande wa vyombo vya mahakama lazima viwe uwezo mkubwa wa kusikiliza kesi kwa wakati na haraka ili kila mwenye haki yake aweze kuipata na kunufaika. Hivyo, ni suala la msingi kuwa sera, sheria na vyombo vya mahakama vinasimama katika uadilifu na haki. Mwenyezi Mungu anasema "Enyi mlio amini! Kuweni wenye kusimamisha uadilifu...(4:135). Kwa kuhitimisha, matatizo yetu ya kiuchumi si uhaba wa rasilimali peke na wingi wa mahitaji peke yake bali pia ukosefu wa fursa sawa, ubora wa maisha yenye uwiano baina ya utu na vitu na ukosefu wa uadilifu na haki.

Wednesday, August 12, 2020

UCHUMI JUMUISHI NA MCHANGO WA CIFCA

Wiki iliyopita tulitowa mfano mmoja unaonesha upungufu wetu katika kujenga uchumi jumuishi. Makala haya yataeleza mifano mingine michache na kueleza mchango wa CIFCA katika masuala ya fedha na kuwa na uchumi jumuishi. Mikopo wa wafanyakazi serikalini. Serikali kama taasisi nyingine hutowa mikopo nafuu kwa watumishi wake. Mikopo hiyo huelezwa kuwa haina riba lakini kwa jicho la Uislam ipo riba iliyojificha au kufichwa chini ya kile kinachoitwa tozo mbalimbali za mkopo huo. Wanachuoni wanaona kuwa mkopo wowote ambao unatozo au unamnufaisha mkopeshaji isipokuwa tozo halisi tu ambazo hulipwa kwa watowa huduma wengine. Kwa mfano tozo ya kutuma mkopo kwenye simu au kwenye bank yako inaweza kukusanywa na mkopeshaji kama gharama halisi ya mkopo unaotolewa. Gharama au tozo ambazo hazifungamani moja kwa moja na gharama halisi za mkopo. Baraza la Taifa la uwezeshaji wananachi Kiuchumi (NEEC). Baraza la taifa ambalo limeundwa na kuanza shughuli zake mwaka 2005 lina dhima ifuatayo "Kuongoza Watanzania kuelekea katika uchumi thabiti wa taifa kwa kutengeneza mazingira rafiki ya biashara na ushiriki sawa katika kiuchumi." Ni dhima inayoleta matumaini na baraza lina program nzuri za kuwawezesha watanzania kujiimarisha kiuchumi. Hatahivyo, yapo maeneo machache yanayopaswa kufanyiwa kazi ili kuwapa waislamu fursa sawa na wananchi wengine. Tovuti ya baraza inaeleza kuwa kuna mifuko ya Serikali na Programu za uwezeshaji wananchi kiuchumi 45 ambazo zinaratibiwa na Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi. Makala haya haitoweza kuangalia mifuko yote hiyo bali tutatazama mifuko inayohusiana na utoaji mikopo moja kwa moja kwa wajasiriamali kwa mfano; 1. Mfuko wa Rais wa Kujitegemea (Presidetial Trust Fund –PTF). Mfuko unatowa mafunzo, mikopo na kufanya tafiti. Ni wazo zuri sana kuwa na mfuko namna hii hata hivyo huduma yake ya mikopo inaweza ikawa sio jumuishi au rafiki kwa waislam iwapo kuna riba ndani yake. Tovuti ya mfuko kwa sasa inaonesha aina za mikopo, masharti na kiwango cha mikopo lakini ipo kimya kuhusu tozo au riba yoyote inayotozwa na mfuko. Suali muhimu ni je mfuko huu unatozza riba kwa mikopo yake au la? Ikiwa inatoza basi ni wazi kuwa sio rafiki kwa waislam kwa kuwa kwa waislam riba imekatazwa. Ikiwa hamna riba, hii itakuwa ni mfano mmoja unaodhihirisha kuwa inawezekana kutowa mikopo bila riba na hivyo harakati za mfuko zinahitaji kupongezwa kwa kuwa jumuishi. 2. Mfuko wa Maendeleo ya Vijana (Youth Development Fund –YDF), Mfuko wa Maendeleo ya Wanawake (Women Development Fund –WDF) na Mfuko wa Taifa wa Kuendeleza Wajasiriamali Wananchi(National Entrepreneurship Development Fund –NEDF). Kimsingi fikra ya kuwa na mifuko hii ni nzuri mno. Hatahivyo, mikopo yake hutolewa bila riba? Ikiwa ni mikopo yenye riba au tozo, hiyo ni mushkeli mkubwa kwa waislam na hivyo kutonufaika ipasavyo na mifuko hiyo. Changamoto na tatizo la riba lipo katika mifuko mingine inayoratibiwa na baraza. Kadhalika, baraza katika utekelezaji wa majukumu yake linaweza kutowa mkopo kwa mtu au shirika kwa mujibu wa masharti waliyojiwekeya. Je mikopo hiyo ina riba au la? Kimsingi, baraza katika kutekeleza majukumu yake ni muhimu mno kuzingatia ujumuishi wa taratibu za mikopo ili baraza hili liwe na manufaa wa watu wote. MCHANGO WA CIFCA Waislam baada ya kutambuwa changamoto zilizopo katika sekta ya fedha na uchumi, waliaamuwa kuanzisha chombo chao chenye lengo la kushauri na kufunza yoyote yule ambaye angependeleya kufuata mfumo wa fedha na uchumi usiohusisha suala la riba. Kadhalika, chombo hicho kinaendeleya kutowa elimu kwa waislam juu ya tatizo la riba katika mikopo mbalimbali ikiwa na lengo la kuhadharisha na kuonesha njia mbadala. Hivyo, ni muhimu sana hususani sekta ya umma kushirikiana na chombo hiki nchini ili mikopo inayotolewa na taasisi za serikali na mifuko ya baraza la taifa iweze kunufaika na wataalamu bobezi wa masuala ya fedha na uchumi waliopo katika chombo hicho na hivyo kuongeza kasi juhudi za baraza. Itambulike ya kwamba, taratibu zisizo na riba ni jumuishi kwa kila mtanzania na sio kwa manufaa ya waislam peke yao. Kadhalika nitoe wito kwa taasisi binafsi za fedha na utoaji mikopo, kutambuwa kuwa lipo kundi kubwa la watanzania ambao hawafurahishwi na hawaridhii miamala ya riba kabisa na sio suala la riba kubwa au ndogo. Riba yote iwe ndogo au kubwa, haifai. Kwa rehema zake Mola ametuwekeya njia nyingi ambazo zinaiwezesha taasisi kufanya biashara na kupata faida isiyokuwa riba. Hivyo, wachukuwe fursa inayopatikana kwa kuwepo kwa CIFCA nchini ili kuweza kushauriwa namna ya kufanya ili waweze miamala sahahi na kutowa huduma zisizokuwa na riba kwa manufaa ya watanzania wote. Jambo hili linawezekana iwapo taasisi husika itakuwa na utashi thabiti na kufuata maelekezo ya wataalamu wa CIFCA katika kuepukana na Riba pamoja na vipengele vingine ambavyo ni vya kinyonyaji.

Wednesday, August 5, 2020

UCHUMI JUMUISHI

Maendeleo ya kiuchumi ni eneo muhimu baada ya yale ambayo tuliyaeleza wiki iliyopita. Katika hotuba ya bajeti ya wizara ya fedha mwaka huu, Waziri wa Fedha alibainisha dhamira ya serikali kuwaleteya wananchi maendeleo ya kiuchumi na kuwajumuisha wananchi katika maendeleo ya kiuchumi. Mikakati kadhaa kila mwaka huwekwa ili kufikiya azma hii. Katika yale ambayo Waziri alibainisha kwa mfano ni kufutwa kwa ada na tozo za kero ili kuboresha mazingira ya kufanya biashara na kuwekeza hapa nchini. Uwekezaji katika miundombinu wezeshi kwa shughuli za uzalishaji mali na biashara ili kukuza uchumi, kuendelea kuorodhesha Hatifungani zake katika Soko la Hisa la Dar es Salaam; na kutoa elimu kwa umma ili kuhamasisha ushiriki wao katika kuwekeza kwenye Hatifungani na Dhamana za Serikali, kusimamia na kuboresha sekta ya fedha; kuongeza upatikanaji wa huduma za msingi kama vile afya, elimu, maji na umeme hususan maeneo ya vijijini; na kuendelea kutekeleza Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini kupitia Mfuko wa Maendeleo ya jamii (TASAF) ili kuongeza kipato chao na kuwawezesha kupata mahitaji ya msingi na kadhalika. Je mikakati hii inawapa fursa sawa wananchi kujumuika kwa katika kuziendea fursa za uchumi? Jawabu ni ndio na hapana! Ili kufahamu hoja za jawabu hii kwanza tujiulize ni nini uchumi jumuishi ambao wachumi katika karne hii wanaona kuwa ni njia muwafaka ya kuhakikisha uchumi unakuwa vizuri na kuwa imara. UCHUMI JUMUISHI (INCLUSIVE ECONOMY). Ukiwauliza watu wa kawaida nini uchumi jumuishi watakuwa na jawabu tofauti na hilo pia lipo kwa upande wa wachumi. Wapo wanaona kuwa uchumi jumuishi ni ule ambao watu wanafursa sawa ya kupata ajira yenye hadhi na kipato halali. Ni uchumi ambao kila mwananchi anahusishwa katika fursa zilizopo za kupata kipato na anaweza kuziendeya fursa hizo bila kikwazo chochote iwe dini au kabila au eneo alilopo na kadhilika. Ni uchumi ambao fursa haziwapendelei watu fulani tu iwe kwa utajiri wao au kwa dini zao au kwa uanachama wao nakadhalika bali kila mtu anaweza kunufaika kikamilifu na fursa zilizopo. Tafsiri moja wapo ambayo inanivutiya zaidi ni ile inayosema kuwa uchumi jumuishi ni ule ambao unawajali watu wote kwa mujibu wa mitazamo yao ya kiuchumi ( inclusive economy as the one that support all people from their economic standpoint). Baada ya kufahamu maana ya uchumi jumuishi, je hatuwa hizi zilizoainishwa na Waziri ni hatuwa zenye kujenga uchumi jumuishi? SIFA YA UCHUMI JUMUISHI NA HALI YETU. Wachumi wamebainisha vigezo au sifa kadhaa za uchumi jumuishi kama vile; ushiriki wa wananchi (participation), usawa wa fursa mbalimbali (equity), kuongezeka kwa mapato (growth), endelevu (sustainable) na imara (stability). Ukitazama sifa hizi na ukilinganisha na hatuwa ambazo waziri amezibainisha utaona kuwa zipo ambazo zimekidhi sifa hizo kama vile kufuta ada na tozo zenye kero, kuwekeza katika miundombinu, upatikanaji wa huduma za msingi,kunusuru kaya masikini na kadhalika. Na kwa upande mwingine, kwa mtazamo wa kiuchumi wa kiislamu, baadhi ya hatuwa zilizotajwa sio jumuishi kikamilifu na hazitowi fursa sawa kwa wote. Kwa mfano, kuoridhesha hatifungani na dhamana za serikali zinazolipa riba. HATIFUNGANI NA DHAMANA ZA SERIKALI. Waziri amesisitiza kuwa serikali itatowa elimu kwa umma ili kuhamasisha ushiriki wao katika au kununuwa au kuwekeza kwenye Hatifungani na Dhamana za Serikali. Kimsingi, serikali huhitaji fedha kwa ajili ya shughuli zake mbalimbali za kuwatumikiya wananchi. Na njia moja maridhawa ni kufanya biashara na wananchi wao, kwa maana ya kuwataka wawekeze katika hatifungani na dhamana zake ili wapate faida na kuongeza kipato chao na huku fedha hizo zinaenda katika kuimarisha miundombinu au huduma muhimu kwa wananchi. Hivyo wananchi wananufaika pande zote mbili. Dosari iliyopo kwa mtazamo wa Uchumi wa Kiislamu ni kuwa hatifungani na dhamana za serikali zimetengezwa katika muundo ambao serikali wanauza hela kwa hela au kitaalamu inakopa kwa wananchi wake na kuwalipa na riba (interest). Hapa kuna tatizo la muundo (structural fault). Nini tatizo? Muundo huu unawanyima na kuwakosesha fursa sawa sehemu ya wananchi hususani waislamu katika kushiriki katika kufanya uwekezaji kwa kupitiya serikali yao kwa kuwa wao, HAWARUHUSIWI kukopa au kukopesha kwa riba au kuuza hela au kukodisha hela kwa hela! Riba ni dhambi kubwa sana katika Uislamu. Ubaya wake umefananishwa na kutangaza vita na Mwenyezi Mungu au kufanya tendo la ndoa na mama yako mzazi. Anayekula riba ataingiya motoni isipokuwa atakapo tubiya na kuachana na riba. Kwa kutolifahamu jambo hili, serikali sio tu haitoweza kupata fedha za kutosha kutoka Waislam wanaofuata dini yao na Waislamu hawatoweza kupata kipato cha ziada. Hivyo, serikali inaumiya na wananchi hawa wanakosa fursa ambayo wenzao wengine wanaipata! Lakini baya zaidi ni kuwa, serikali inapolipa riba kwa wale ambao watawekeza katika hatifungani na dhamana hizo kwa kuwa dini zao haziwazuii kukopesha kwa riba itakuwa inatumiya kodi zetu sote kuwanufaisha kwa malipo ya riba baadhi tu ya wananchi! Hali hii inadhihirisha wazi kuwa muundo wa serikali wa kukopa kwa riba kwa kuuza hatifungani na dhamana (Treasury bills and treasury bonds), sio jumuishi kwa wananchi wote. Ni muundo unaowabaguwa waislamu kwa kuwafanya wasishiriki katika kufanya 'biashara' serikali na kupata faida ya halali. Ni muundo ambao inahitaji kufikiriwa upya ili kutafuta muundo mwingine ambao utaiwezesha serikali kupata hela au kukidhi mahitaji yake na wananchi kuwekeza na kupata faida halali. je ipo njia mbadala? NINI CHA KUFANYA? Njia tulioieleza hapo awali ya kukopa kwa riba ni kongwe na imekuwa ni ya mazoeya lakini ukweli ni kuwa sio shirikishi kwa wananchi wote na ni yenye kubaguwa waislamu. Wachumi wa Kiislamu, wameshapendekeza miundo mengine ambayo serikali inaweza kupata hela au ukidhi mahitaji yake bila ya kutumiya mkataba wa kukopa kwa riba na badala yake kutumiya mikataba mingine kama vile ya mauziano (sales) au kukodisha (leasing) au kushirikiana katika faida na hasara (partnership). Jina maarufu la njia zenye kufuata mikataba hii ni Sukuk. Zipo Sukuk aina nyingi na zenye kuundwa kwa mikataba mbalimbali lakini sio mkataba wa kukopa (loans contract). Njia hii y Sukuk, imeshatumika nchi kadhaa ikiwemo Afrika Kusini, Nigeria, Gambia, Senegal, Sudan na nchi nyingine. Miundo hii (Sukuk) inayowafikiana na kanuni za kibiashara za Kiislamu hazibagui watu wa dini nyingine kwa kuwa hazipingani na mafunzo ya dini hizo. Waislamu na wasiokuwa waislamu wanaweza kushiriki kwa usawa. Je njia hizo zinawezesha wananchi kupata faida? Ndio. Kwa mfano, serikali inataka fedha kwa ajili ya kununuwa mitambo ya Umeme wa Stigler's Gorge ili kuzalisha umeme nchini. Ili kukidhi haja hii serikali kwa kupitiya bank kuu inakaribisha wananchi kuchanga fedha ambazo zitatumika kununuwa mitambo hiyo kwa bilioni 100 kwa mfano, na serikali itaahidi kununuwa mitambo hiyo kutoka kwa wananchi kwa Bil 105 na wananchi hao watalipwa ndani ya mwaka au miaka mitatu na kadhalika kulingana na kila mmoja alivyochangiya na gawio la faida. Kwa utaratibu huu, haya ni mauziano kwa faida na sio kukopeshana. Hii ni biashara halali ya mali kwa fedha na sio biashara haramu ya fedha kwa fedha. Hii ni njia moja tu katika njia nyingi zilizobuniwa na wachumi waislam katika kuiwezesha serikali kupata mahitaji yake (financing government deficit budget) ambayo waislam na wananchi wote kwa usawa wanaweza kushiriki na kuhimizana kushiriki kikamilifu na kuiondoleya serikali kazi ya ziada katika kuhamasisha. Hivyo, jambo hili linawezekana na wapo wataalamu wa kutosha duniani wa kuishauri serikali katika kuweka muundo ambao unaepukana na riba. Kinyume na hivi, waislam wanasikitika mno kuona matangazo ya serikali yanahamasisha kununuwa hatifungani na dhamana zake kwa njia ya riba ilhali zipo njia mbadala zisizo na riba ambazo na wao wanaweza kushiriki bila kuvunja kanuni za dini yao. Waislamu wanahuzunika kuona serikali itatumiya kodi zao kulipa riba kwa baadhi ya wananchi na kuwanufaisha watu wachache tu. Ili kutuondoleya masikitiko haya na huzuni hizi, tunaiomba kwa heshima kubwa serikali yetu sikivu ione kuwa kuna haja sasa ya kubuni njia mbadala ambazo zitawapa wananchi wote fursa sawa ya kushiriki katika kuiwezesha serikali kupata mahitaji yake na wananchi kupata fursa ya kupata kipato cha halali.