Pages

Sunday, November 15, 2020

MIKOPO YA ASILIMIA KUMI YA HALMASHAURI: FURSA, CHANGAMOTO NA UFUMBUZI WAKE

Moja katika mambo yanayopaswa kupongezwa kwa serikali na wabunge ni kuwepo kwa Sheria ya Fedha za Serikali za mitaa (Chapter 290- The Local Government Finance Act 2019) na hususani kifungu 37 A ambacho kinasema kwamba (tafsiri ni yangu): 1. Mamlaka za serikali za ndani (district authority and urban authority) watateenga asilimia 10 ya mapato yake kwa ajili ya kuwezesha vikundi vilivyosajiliwa vya kina mama, vijana na watu wenye ulemavu. 2. Fedha zote zitakazotengwa kwa mujibu wa kifungu (1) zitatumika kwa ajili ya kutoa mikopo kwa vikundi vilivyosajiliwa vya wanawake, vijana na wau wenye ulemavu kwa mgao wa asilimia 40 kwa wanawake, asilimia 40 kwa vijana na asilimia 20 kwa wenye ulemavu. 3. Mikopo itakayotolewa kwa mujibu wa kifungu hiki haitakiwi kutozwa RIBA 4. Waziri, kwa kupitia kanuni anaweza kuweka utaratibu wa usimamizi na ugawaji wa mikopo hiyo kwa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu. FURSA. Kwa kuzingatia amri ya Sheria hii, fursa ya kupata mikopo ambayo haina riba kwa wananchi inapaswa kutumika ipasavyo kwa mujibu wa taratibu ambazo wilaya husika kwa kupitia mamlaka aliyopewa Waziri husika itaziweka. Ni wajibu wa serikali za wilaya kuweka wazi uwepo wa fedha hizi na taratibu zake zote katika tovuti, na machapisho ya wilaya husika ili wananchi waweze kujuwa kiwango cha fedha kilichotengwa kwa mwaka husika, mchakato wa maombi, muda wa kujibiwa maombi, shughuli za uzalishaji au biashara zinazopewa kipaumbele na kadhalika. Kadhalika ni wajibu wa madiwani, kuhakikisha wilaya husika inaweka wazi taarifa zote za mikopo hii kwa wananchi na yeye kuzifikisha taarifa hizo kwa makatibu watendaji wa kata, wenyeviti wa serikali za mitaa na kwa mabalozi wa nyumba kumi. Kadhalika ni wajibu wa watumishi hawa bila kujali mrengo wa kisiasa wa wananchi anao wawakilisha kuzifikisha taarifa hizo ili wananchi wote wanufaike kwa kukuza uzalishaji na kukuza biashara katika maeneo husika. Kama wananchi, ni wajibu wetu kujiunga katika vikundi kwa mujibu wa taratibu zilizowekwa na halmashauri husika kwa jili ya kuweza kupata mikopo hii na kujikomboa kiuchumi. CHANGAMOTO. Katika mkutano wa mwisho wa mwezi wa Oktoba, taasisi ya Policy Forum kwa kushirikiana na UNA Tanzania waliaandaa mjadala kuhusu mikopo hii ya asilimia kumi. Ndugu Maeda aliwasilisha mada nzuri juu uwepo wa fursa hii kwa wananchi na changamoto kadhaa zikiwemo 1. Kutotekelezwa kwa amri ya sheria hii kwa baadhi ya wilaya nchini. 2. Kukosekana kwa taarifa kwa wananchi wa wilaya husika juu ya uwepo wa mikopo hii kwa vikundi. Tafiti yangu ndogo kwa njia ya mtandao kwa wilaya zote za Dar es Salaam, tovuti zao hazina taarifa hii katika huduma zao kwa wananchi. Wilaya ya Kigamboni tu kwa kupitia jarida lao la mwaka huu lililopo katika tovuti ya Tamisemi inaonesha kuwa kuanzia mwaka 16/17 mpaka 19/20 jumla ya Bil 1.4 zimetumika kwa ajili ya mikopo hiyo. Hatahivyo hamna taarifa zozote kuhusu kanuni na taratibu za utoaji na upatikanaji wa mikopo hiyo ya vikundi katika jarida hilo na mengineyo katika tovuti zao. 3. Uhaba wa rasilimali watu katika halmashauri kwa ajili ya kusimamia kanuni, taratibu na urejeshaji wa mikopo hiyo. Maafisa maendeleo ya jamii ambao wamepewa jukumu hili pamoja na majukumu mengine wanahemewa na uzito wa kazi na hivyo kupelekea usimamizi legevu wa mikopo hiyo katika utoaji wake na ufuatiliaji wa urejeshwaji wake. Suala la utoaji mikopo na usimamizi wake (Credit Management Skills) ni la kitaalamu na lenye kuhitaji weledi mkubwa katika kulifanikisha. Ukosefu wa muda na mafunzo hayo ni kikwazo kikubwa sana. 4. Vikundi hewa vinavyohusishwa na wanasiasa waliopo madarakani katika wilaya husika ni tatizo kubwa. Hii inapelekea fedha zinazotolewa kutokurudishwa na hamna taarifa rasmi ya urejeshwaji wa mikopo hiyo. Halmashauri nyingi zinaeleza kiwango cha utoaji wa mikopo husika na hawaelezi makusanyo ya madeni hayo. Kwa nini? 5. Utowaji wa mikopo kwa mrego wa kisiasa ni tatizo kubwa. Baadhi ya wanasiasa, kama wabunge na madiwani, wanaweza kugeuza kuwa mtaji wa kisiasa katika utoaji wa taarifa za uwepo wa mikopo hii, kutowa ushawishi wa vikundi vya kupewa na visivyofaa kupewa, kujitafutia umaarufu wa kisiasa kwa kupitia mikopo hiyo na hata kushawishi kuundwa vikundi hewa ili walengwa wao wanufaike. 6. Muda mfupi wa kuanza marejesho ya mikopo husika. Kwa kukosekana weledi katika fani ya mikopo, mikopo hutolewa bila kuzingatia mzunguko wa biashara husika. 7. Muda mrefu wa kujibiwa maombi ya mikopo. 8. Uwezo mdogo wa kiungozi wa kuendesha miradi ya vikundi husika. Vikundi husika kwa kukosa maarifa ya somo la biashara na ujasiriamali na uongozi, wanashindwa kuendesha biashara na vikundi vyao kufikia malengo ya miradi ya vikundi. Watendaji wa vikundi hawana ujuzi wa usimamizi wa fedha, undeshaji wa miradi ya kiuchumi na masuala ya uongozi. 9. Urasimu katika mchakato wa kupata mikopo. Hili ni changamoto kongwe katika shughuli za halmashauri ambao unatokana na kuwepo kwa masharti ambayo hayanatija zaidi ya upotevu wa muda. Kwa mfano, maombi ya mikopo yatakiwa iambatane na barua ya utambulisho wa mtendaji wa kijiji au mtaa na mtendaji wa kata. Mara nyingi ofisi za watendaji hao zipo maeneo tofauti na kila mtendaji kabla ya kutoa utambulisho huo anachukuwa siku kadhaa na hata kupelekeya hisia za kutaka rushwa ili kuandika barua hiyo. 10. Upo uwezekanao wa halmashauri kutoza riba katika mikopo hii kinyume na sheria iliyotajwa hapo juu. SULUHISHO. 1.Taarifa kwa wananchi. Halmashauri zote zinapaswa kuweka taarifa za uwepo wa mikopo hii katika tovuti zao, mabango ya halmashauri na machapisho ya halmashauri. Taarifa za kina zenye kueleza kanuni na taratibu zote za upatikanaji na utoaji wa mikopo hiyo kwa njia ya uwazi na uwajibikaji. Tovuti za Halamshauri nyingi nchini hazina taarifa zozote katika "Huduma Zetu" kuhusu mikopo hii. Kipekee niitaje Halmashauri ya Jii la Tanga ambao katika huduma zetu wameweka "Uwezeshaji wananchi." Hatahivyo, taarifa zao zinahitaji kuboreshwa zaidi ili kuwe na uwazi. 2. Mrengo wa Kisiasa. Wizara na Wakuu wa Mikoa yote husika wanapaswa kuhakikisha ya kuwa Halmashauri hazitowi huduma hii kwa mrengo wa kisiasa. Kama ambavyo benki hutakiwa kuanisha mikopo kwa wanasaisa, kadhalika mikopo inayotolewa kwa vikundi vinavyohusiana na wanasiasa yapaswa taarifa hizo kuwekwa wazi na umakini katika kuongeza uchambuzi wa tathmini ya miradi husika ili kuepusha tatizo la vikundi hewa au vikundi vya kisiasa ambayo mikopo hiyo huwa ni kama zawadi badala ya kufanyia shughuli za kiuchumi. 3. Elimu ya Biashara na Uongozi. Kitaifa elimu ya biashara na ujasiriamali ni muhimu sana haswa ukizingatia kuwa sekta binafsi na ujasiriamali ni injini ya uchumi wa kisasa kama alivyosema Mh. Rais katika ufunguzi wa bunge la 12. Kadhalika elimu ya uongozi wa vikundi ni nguzo muhimu katika kufanikiwa kwa kikundi cha kiuchumi. Mkakati wa muda mrefu unahitaji kuwepo somo la biashara lianze kufunzwa katika elimu ya msingi na iwe lazima mpaka kidato cha nne. Somola General Studies katika A' level lazima liwe na maudhui ya Ujasiriamali wenye mafanikio na uongozi wa vikundi vya kiuchumi. Kadhalika, mkakati wa muda mfupi unahitaji kuzilazimisha Halmashauri kwa kushirikiana na taasisi binafsi na za umma za kutowa mafunzo ya ujasiriamali na uongozi kwa vikundi vya kiuchumi vinavyosajiliwa katika halmashauri na wahusika wafaulu vizuri kabla ya kupewa mikopo hiyo. 4. Usimamizi wenye weledi. Maafisa maendeleo ya jamii wapate wasaidizi au waajiriwe maafisa wa mikopo ya vikundi vya kiuchumi kwa ajili ya kushughulikia kata maalumu. Maofisa hao wawe wamesomea masuala ya usimamizi makini wa mikopo ya vikundi, wawe na mafunzo ya mara kwa mara, wapewe malengo ya kila mwaka katika kutoa mikopo iliyo safi, wafuatilie mikopo, wale watakaobainika kushindwa kusimamia urejeshwaji wa mikopo hiyo waachishwe kazi na waajiriwe watendaji wengine watakaomudu majukumu yao ipasavyo. Pendekezo hili linatoa fursa kwa vijana wetu waliosoma fani za kibenki, fedha, n.k kupata ajira na fedha hizi zilizotengwa katika kutowa mikopo hii zinaweza kutumika kwa kiwango cha asilimia 30 kulipa mishahara yao na asilimia 70 kutoka katika mapato mengine ya halmashauri. 5. Kushirikiana na sekta binafsi. Ili kuepuka mikopo hewa na watu wasiokuwa waaminifu, Halmashauri na ofisi za mkoa ziwe na mashirikiano na mashirika binafsi ya kukagua taarifa za vikundi, kufuatilia mikopo sugu na kuwapeleka wahusika mahakamani. Kadhalika, kuwa na mashirikiano na vyuo vya mafunzo. 6. Tehama. Ili kuwe na ufanisi wa usimamizi mzuri, ni vyema halmashauri kutumia tehama ya usimamizi wa mikopo (credit management software) ili taarifa zote za mikopo yote iwepo katika mtandao ili kuhakikisha ya kwamba taarifa za vikundi hazipotei na utunzaji wa kumbukumbu zote unaimarishwa. 7. Adhabu na Pongezi. Wizara yapaswa kuziadhibu Halmashauri zote ambazo zitashidwa kutoa mikopo hii kwa asilimia 80% ya fedha zilizokusanywa katika mwaka husika na zile zote ambazo mikopo mibaya ni zaidi ya asilimia 10% ya fedha zilizotolewa. Wizara iwe inafanya uchunguzi wake kabla ya kutoa adhabu hizo ili kubaini changamoto ambazo zipo nje ya uwezo wa Halmashauri na kubuni namna bora ya kuzisaidia au kushirikisha sekta binafsi katika utatuzi wake. Kadhalika, wahusika wa utoaji mikopo inayotolewa nje ya taratibu na kanuni yapaswa kuadhibiwa. Na halmashauri zinazotekeleza vyema usimamizi wa mikopo hii kupongezwa na kutambuliwa. 8. Kuondoa Urasimu na kuharakisha uoaji wa huduma. Utarataribu wa wajumbe wa vikundi upunguzwe kutoka watu 10 mpaka 5, muda wa kutoa mikopo ndani ya miezi mitatu upunguzi mpaka ndani ya mwezi mmoja, na mianya ya rushwa izibwe kwa kuwa na dirisha katika halmashauri la malalamiko yote yanayohusiana na mikopo ya vikundi. Malalamiko hayo, yashughulikiwe kwa haraka na kwa uadilifu pale inapothibiti ukiukwaji wa taratibu na kanuni zilizowekwa. Hitimisho. Kwa dhati nirejee kupongeza kwa kuwepo kwa sheria hiina kwa kuwaletea wananchi fursa muhimu ya kujiwezesha kiuchumi kwa kupitia halmashauri zao nchi nzima. Kwa miaka mingi wananchi wanalalamikia riba kubwa katika taasisi za fedha na kwa hatua hii ni wazi kuwa serikali imeleta ufumbuzi mzuri ambao yatupasa kuuimarisha na kuudumisha kwa vizazi vya leo na kesho. Nitoe wito kwa taasisi nyingine kama za SIDO na mifuko mbalimbali ya uwezeshaji, kuachana na fikra mgando za mikopo ya riba bali wajikite katika kufanya biashara kwa njia ya kugawana faida au hasara (profit and loss sharing) ambayo ni yenye uadilifu, haki na jumuishi kwa wananchi wote. Mwisho, niwakumbushe maneno ya Mh.Raisi JPM akifungua bunge la 12 aliposema "Penye kukosoa kosoeni kwa hoja na kutoa mapendekezo ya namna ya kushughulikia. Tunahitaji constructive criticism na sio kukosoa kwa lengo la kukosoa tu." Haya ni maneno mazito ambayo yanatukumbusha wajibu wa kila mmoja wetu kama wananchi na sio kwa wabunge pekee. Hii ni kazi ya kila raia mwema kwa nchi yake kuhakikisha mikopo ya 10% inafanya kazi iliyokusudiwa ya kuleta mapinduzi ya kiuchumi kwa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.