Pages

Wednesday, July 29, 2020

MAENDELEO TUYATAKAYO


Tupo katika mwaka wa uchaguzi mkuu wa nchi nzima. Vyama mbalimbali vitarudi kwa wananchi kunadi sera zao na mipango yao ya kuwaleteya wananchi maendeleo. Je ni maendeleo gani tuyatakayo watanzania na waislamu?

Dhana ya Maendeleo.

Neno hili "Maendeleo" (Development), hupendwa sana kutumiwa na wanasiasa wanapojinadi kwa wananchi. Wataalamu wa lugha ya Kiingereza wanasema kuwa neno hili "development" lilianza kutumika katika kuelezeya hatua za ukuaji wa viumbe katika miaka ya 1756. Na limekuja kutumiwa na wachumi katika miaka ya 1902 na kuendeleya likimaanisha kuwa ni hali ya kupiga hatuwa za kiuchumi (state of economic advancement). Dhana hii ya maendeleo ya kiuchumi ilishika kasi zaidi baada ya vita vya pili vya dunia na mijadala kadhaa ikifanyika mpaka kuja kuibuka kwa somo maalum liitwao "development economics." ambalo hufunzwa katika vyuo vikuu mbali mbali ulimwenguni.

Kimsingi kuna tafsiri nyingi sana kutoka kwa wachumi kuhusiana na swali hili, "maendeleo" ni kitu gani? Wengi wetu neno maendeleo tunalihusisha tu na weingi wa fedha, hali nzuri ya maisha inayomwezesha mtu kuweza kujikimu bila hofu, kuwa na miundombinu imara kama vile barabara, maji, shule, umeme, vituo vya afya, kukuza uchumi ili kutowa ajira nyingi nakadhalika. Mara nyingi viongozi na wanasiasa hukusudiya maana hii wanaposimama kujinadi majukwaani kuomba kura. Haya ni sehemu moja tu ya maendeleo.

Maendeleo katika Uislam.

Wachumi wa Kiislamu wamefanya kazi kubwa katika kubainisha mtazamo wa Uislamu kuhusu maendeleo. Pamoja na kuwepo mitazamo mbalimbali, wanachuoni hawa wanaona kuwa maendelo ni lazima yajumuishe na yahusishe maeneo matatu muhimu na makubwa. La kwanza, uwepo wa fursa kwa wote na uhuru wa mtu binafsi kujiendeleza mwenyewe bila hofu wala upendeleo (individual human self-development without fear or favour).Pili, uwepo wa mazingira rafiki na bora yenye kumwezesha mtu kufikiya malengo yake kipindi chote (physical and material development of the earth). Na la tatu, kuwepo kwa haya mawili kwa watu wote katika jamii husika (development of society as whole). Uislam unaona kuwa eneo la kwanza ni muhimu zaidi na ndio chachu ya kupatikana maendeleo katika maeneo haya mengine. Anasema Mchumi mmoa wa Kiislam Profesa Abdul Hamid Abdul Aziz "Mazingira ya mwanadamu yaandaliwe kutowa fursa na uhuru wa kubadilika kutoka hatuwa moja kwenda hatuwa iliyobora zaidi sio kimali tu na bali na kiimani na muruwa mwema (material and spiritual development)."

Uislam unaona maendeleo yoyote yale lazima yamwezeshe Mtu ambaye ni Khalifa wa Mwenyezi Mungu, aweze kutoka katika umasikini wa kipato, fikra, imani na utamaduni na kueleya katika mabadiliko ambayo yatamwezesha kuwa na utajiri wa maarifa, wingi wa Imani kwa Muumba wake, muruwa mwema au tabia njema, fikra madhubuti za kielimu na kuyamudu mazingira yake muda wote. Mtu huyu awe anajitambuwa mwenyewe, anatambuwa lengo la kuumbwa kwake, anamtambuwa Muumba wake, na majukumu aliyopewa kama Khalifa wa Mwenyezi Mungu ambayo yanalengo la kumtowa katika upotofu na giza na kumwingiza katika nuru na uongofu. Kwa lugha ya Qur'an hawa ndio Ar Rashidun (walioongoka na walioendeleya)

Maendeleo katika sura hii ndio ambayo Quran inayaona kuwa ni fadhila na neema kubwa pale Mola aliposema "Lakini Mwenyezi Mungu amekupendezeeni Imani, na akaipamba katika nyoyo zenu, na amekufanyeni muuchukie ukafiri, na upotovu, na uasi. Hao ndio walio ongoka (walioendeleya).Kwa fadhila za Mwenyezi Mungu na neema zake. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kujua, Mwenye hikima (49:7-8). Mtume salallahu alayhi wasallam amesema " Amefaulu (katika kila jambo) yule ambaye ni Muislam wa kweli aliyejisalimisha katika uongofu wa Mola wake, akaruzukiwa rizki yenye kumtosheleza mahitaji yake katika maisha ya Ulimwengu na Moyo wake ukawa wenye kushukuru na kukinai (usiokuwa na pupa na vitu au anasa za kilimwengu)." Vile Mtume s.a.w amesema " Sifa nne mwenye kuwa nazo, basi asiwe na hofu juu ya lolote alilolikosa ulimwenguni. Ya kwanza, Uaminifu (trustworthy) (dhana pana sana yenye kujumuisha kuwa Mwaminifu juu ya amri za Mola wako na juu ya yale uliyoaminiwa na viumbe wenzio iwe siri, kazi, au mali n.k). Ya pili, Ukweli (truthful) katika kauli zako na matendo yako ya kila siku, humdanganyi mtu wala huthubutu kumdanganya Muumba wako. Ya tatu, kuwa na tabiya njema zenye kupendeza hata watu wakawa hawaudhiki kwa kuwepo kwako pamoja nao, ikawa mfano wako ni sawa na mtende wenye kutowa mazuri zaidi kuliko unayochukuwa kutoka katika ardhi na kwa watu na ya mwisho, mwenye kutosheka na chakula chako cha kila siku." [Imepokewa na Imam Ahmad katika Musnad Ahmad].

Pamoja na hayo, Uislam umempa jukumu mwanadamu aindeleze ardhi au ulimwengu na mazingira yanayomzunguka kwa kumtaka awe Mus-liheeena (mwenye kufanya wema) na sio Mufsideena (mwenye kuharibu). Mola anasema "Na utafute, kwa aliyo kupa Mwenyezi Mungu, makaazi ya Akhera. Wala usisahau fungu lako la dunia. Nawe fanya wema kama Mwenyezi Mungu alivyo kufanyia wema wewe. Wala usitafute kufanya ufisadi katika ardhi. Hakika Mwenyezi Mungu hawapendi mafisadi." (28:77).

Maendeleo Tuyatakayo.

Kwa kuzingatiya kuwa dhana ya maendeleo ni mada pana mno Kiuchumi na katika Uislam na ambayo makala haya haitoshi kuijadili kwa urefu wake bali kukumbusha tu Waislam na wasomaji wafahamu Uislam una mtazamo wake na mafundisho yake yanalenga kumleteya maendeleo mwanadamu katika maeneo yake yote muhimu; kiimani, kiakili, kitabiya, kimali, kiafya na kimaisha kwa ujumla wake na sio kama nadharia za kimagharibi ambazo zimechukuwa baadhi ya mambo haya na kuyaacha mengine. Hivyo maendeleo tuyakayo ni lazima yajikite katika ujumuifu mambo haya yote na katika kuelezea nukta hii nitatowa mifano miwili tu.

Maendeleo ya Kiimani.

Mwanadamu anahitajio la kuamini katika maisha yake. Kwa kuwa hili halimwepuki, anaweza kuishiya kuamini ipasavyo au kupoteya katika imani yake hiyo. Na haiwezekani bali ni ujuha uliofurutu ada kuwa mwanadamu anaweza kudai yeye hana anachoamini. Hivyo binadamu anahitaji maendeleo ya kiroho na kiimani (spiritual development). Je kama taifa tunamjengeya imani gani mwananchi wa Tanzania? Ukitazama vyama mbalimbali, utaona kuwa vyama hivyo vina ambayo vinayaamini kwa mfano kipo chama kinachoamini kuwa "Binadamu wote ni Sawa, Kila mtu anastahili heshima ya kutambuliwa na kuthaminiwa utu wake.Ujamaa na kujitegemea ndiyo njia pekee ya kujenga jamii ya watu walio sawa na huru." Kwa hiyo, vyama vina imani zake mbalimbali.

Je ni maendeleo gani ya kiimani tuyatakayo? Kama Waislamu, maendeleo ya kiimani tuyakayo ni kuwa na taifa linaloamini uwepo wa Mwenyezi Mungu Mmoja na sifa zake tukufu na kadhalika. Hivyo kwa kuzingatia imani hii, wale wanaodai kutaka kutuleteya maendeleo hawatopuuza mchango wa wale ambao wanatukumbusha uwepo wa Mwenyezi Mungu na muongozo wake kama ambayo hali ilivyo sasa hivi. Kwa mfano, kwa nini hamna walimu walioajiriwa kufundisha somo la dini mashuleni kama ilivyo masomo mengine? Je kwa nini serikali haitowi msaada katika kuchapa na kusambaza vitabu vya elimu ya dini mashuleni? Majibu mepesi tunayoweza kuyapata ni kuwa serikali haijihusishi na mambo ya dini au serikali haina dini. Ikiwa kuyafanya haya ni kujihusisha na mambo ya dini kana kwamba dini ni jambo baya kabisa basi ni wazi kuwa eneo hili la kimaendeleo limewachwa makusudi. Sisi tunaona kuwa serikali kama ambavyo inasimamia taasisi zote za dini bili kuziingiliya uendeshaji wake hivyo hivyo inayo nafasi ya kutowa machango wake katika eneo hili muhimu na nyeti la kimaendeleo. Hivyo, iwapo wanasiasa wetu wanadai na kuamini Mungu yupo, hatuna budi kuendeleza imani hiyo kwa kiwango cha kuthamini walimu wa masomo ya dini katika nchi yetu.

Maendeleo ya Kitabia

Mwanadamu anatabia zake za kimaumbile na zile anazojifunza kila siku na kuamuwa za kuchukuwa na kuziacha. Maendeleo yenye kubadilisha tabiya mbovu kuelekeya katika tabia nzuri (moral development) ni kipaumbele kinachostahiki . Je kama taifa tunafunza, kusimamiya na kuhimiza tabiya gani kwa wananchi wetu bila kujali mwanachama wa chama au la? Nchi yetu imeshuhudiya na inaendeleya kushuhudiya mmomonyoko wa maadili mema kwa vijana na wazee wetu. Haya ni matokeo ya kutofunza na kusimamia maadili ipasavyo katika ngazo zote. Watu wafunzwe tabia ya ukweli, uaminifu, uchapakazi, kufanya mambo kwa ajili Mungu n.k. Kama taifa tumewaachia watu fulani kufunza maadili kama vile viongozi wa dini, wazazi au mtu binafsi. Je inatosha? Jawabu ni haitoshi. Kama ambavyo tunafunza masomo ya uraia (civic education), mazoezi (physical education) n.k tunahitaji uwekezaji katika kufunza maadili mema kama taifa na kuyasimamia. Haitoshi kuwa na watu ambao wanasema "Nitasema kweli daima, fitina kwangu mwiko" na kisha wanapoenda kinyume chake kwa kusema uongo hadharani na kuleta fitina ikawa taifa halichukuwi hatuwa zozote. Wamesema wanchuoni wa tabia kuwa "Taifa / Umma wowote ule kuwepo kwake na kubaki kwake kunategemeya uwepo wa maadili yake. Iwapo maadili yake yataondoka, basi na umma huo utakuwa umeondoka hata kama vizazi vingalipo."

Hivyo maendeleo tuyatakayo yawe jumuishi kwa watu wote, yenye mtazamo mpana na mtambuka ambayo yatajikita kumbadilisha mwanadamu mwenyewe kuwa kiumbe bora kama Mungu anavyotaka awe na kuimarisha mazingira yake na kustawisha jamii yote kwa ujumla. Maendeleo ambayo yanatowa fursa kwa wote kujiendeleza kwa uhuru bila uonevu wala kupendelewa au kukandamizwa. Maendeleo ambayo utu wetu unaheshimiwa, unalindwa, unaimarishwa na kuendelezwa na sio kudunishwa, kupuuzwa au kudumazwa.


Monday, July 20, 2020

HATARI YA MOTO NA HAJA YA BIMA YA KIISLAMU (TAKAFUL)



Mwaka wa 2019 na mwanzoni mwa mwaka huu, nchini Australia walipatwa na janga kubwa la moto katika misitu (bushfires) na mpaka katika makazi ya watu. Zaidi ya ekari 46 milioni ziliteketeya kwa moto, nyumba zaidi ya 3500 ziliunguwa na watu 34 walipoteza maisha.

Kwa masikitiko makubwa, mwezi huu baadhi ya shule za Kiislam kama vile Ilala Islamic, Mtambani, Kinondoni na kituo cha mayatima zilikumbwa na maafa ya kuunguwa kwa moto. Kwanza niwape pole wafiwa wa janga hili na waathirika wote wa moto huu na mingine iliyopita. Ni jambo la kusikitisha uhai na mali inapopoteya kwa mkasa wa moto au kwa janga lolote jingine. Kwa kuwa yameshatokeya, hatuna budi kuwa na subira na tunamuomba Mola atuepushe yasiendelee kutokeya maafa haya.

Binafsi nimekumbana na mtihani wa moto mara mbili katika maisha yangu. Mara ya kwanza, nikiwa shule ya msingi, nyumba yetu ilipatwa na mkasa wa kuunguwa na sehemu ya chumba kimoja iliathirika sana kisha moto huo ulizimwa kwa taufiki ya Allah kupitiya msaada ya majirani wema. Nakumbuka zahma na taharuki zake siku hiyo hazikuwa za kawaida. Mara ya pili, nikiwa chuo kikuu cha Kiislamu nchini Uganda, bweni letu lote lilichomeka kwa moto. Sikuweza kuokoa chochote zaidi ya nguo nilizokuwa nazo siku hiyo na ilikuwa karibu na muda wa mitihani ya kumaliza muhula. Ni mtihani mzito, uliotulazimu tulale msikitini kwa muda, tuazimwe nguo za kuvaa, kupewa nasaha (counselling) na mengi ya kueleza lakini hapa sio sehemu yake. Makala haya yatajaribu kusisitiza juu ya hatari ya janga la moto katika maisha yetu, athari yake kiuchumi na hatuwa za kuchukuwa ili kujihadhari na athari hizo.

Hatari na maafa ya Moto.

Maafa ya moto huenda yameanzia pale moto uliposhushwa na kutumika na binadamu ulimwenguni. Moto umetajwa katika vitabu vitukufu kama adhabu waliondaliwa waovu katika maisha ya Akhera kwa kuasi kwao maelekezo ya Mola wao. Ikiwa moto ni adhabu akhera kwa waovu, basi hili ni afa na janga kubwa na baya mno linaloweza kumpata binadamu duniani au akhera.

Siku moja wakati wa Mtume Muhammad s.a.w nyumba iliunguwa na kuunguza wakazi wake katika mji wa Madina. Mtume s.a.w akasema " Moto huu kwa hakika ni adui yenu. Mnapoenda kulala, hakikisheni mnazima sehemu zenye moto." (Sahih Bukhari). Katika hadithi nyingine kasema " Msiuwache moto unawaka katika nyumba zenu." Katika Qur'an, Allah s.w.t ametuagiza " Enyi Mlioamini, jiepusheni nyinyi na familia zenu kutokana na Moto." (66:6).

Vyanzo vya maafa ya kuunguliwa na moto ni anuai. Inaweza sababu ikawa ni hitilafu ya umeme (electrical), matumizi yasiyo sahihi ya majiko ya kuni, mkaa au gas (Cooking), sigara ambayo haikuzimwa, mishumaa na vifaa vya kutiya joto hasa katika maeneo ye baridi (heaters)na kadhalika. Kadhalika moto unaweza kusababishwa na watu wanaotaka kuhujumu wengine. Kimsingi, moto unapoleta maafa ni lazima vyombo vya uzimaji moto vifanye uchunguzi wa kina juu ya sababu yake na iwafahamishe wahusika sababu hizo. Katika nchi zilizoendeleya, matukio yote ya moto hurekeodiwa na sababu zake ili taarifa hizo ziwafae wananachi katika kuchukuwa tahadhari zaidi.

Athari za Kiuchumi.

Kuna nchi chache ambazo huweka taarifa ya gharama ya moto katika nchi zao kiuchumi. Nchini Uingereza na Wales, taarifa yao ya mwaka 2003 (Economic cost of fire report) imekisia kuwa gharama ya moto katika nchi hizo ni paundi 7.7 bilioni (sawa na Tzs 22 trilioni).

Katika moto uliotokeya Australia mwanzoni mwa mwaka huu, Wataalamu wa masuala ya bima walikisiya kuwa baina ya Nov 2019 mpaka kati ya Feb, 2020 moto huo ulisababaisha hasara inayokaribiya bilioni za marekani 1.3 kutokana na madai yaliyowasilishwa(insured claims) kwa makampuni ya bima. Mwaka 2015 katika nchi ya Indonesia, moto katika misitu yake na mazao yake yaliigharimu nchi hiyo dola za marekani bilioni 16.

Kiwanda kinapopata moto, wafanyakazi wenye ujuzi wanaweza kupoteza maisha yao, mashine na zama muhimu kuharibika, ajira kupoteya, uzalishaji kupunguwa n.k ni athari kubwa japokuwa sio rahisi kutathmini athari yake kifedha katika uchumi. Nyumba ya mtu inapatwa na janga hili, niwazi kuwa inamuathiri mtu kiuchumi kwa kukosa makazi yake salama na uwezekano wa kutumiya nyumba yake kama dhamana ya mikopo benki. Mbaya zaidi inamweka katika gharama ya kukodisha nyumba kila mwezi na kulipiya pesa kadhaa. Mifano hii michache itutosheleze kutambuwa kuwa moto iwe wa nyumbani au shuleni au kiwandani au ofisini unaathari kubwa kwa watu na mali zao na uchumi kwa ujumla.

Tathmini za awali za shule ya Ilala Islamic, Mvumoni na Kinondoni Muslim zinaonesha karibu nusu bilioni au zaidi zitahitajika ili kurekebisha hasara iliyojitokeza ya mali zilizopoteya lakini uhai hauwezi kurudi tena. Ikiwa taasisi hizo zinamkopo benki, wanaweza kuathirika katika kulipa mikopo na kusababaisha benki kuwa na mikopo mibaya (non-performing loans)


Hatuwa za kuchukuwa.

Kimsingi kuna hatuwa tatu za kukabiliana na tishio la moto katika nyumba au ofisi au kiwandani. Ya kwanza, ni kuchukuwa tahadhari ya kuepuka kuwa na matumizi ya moto kabisa katika nyumba au ofisi. Kusiwe na umeme, kusiwashwe kandili au mshumaa au matumizi ya kitu chochote cha moto, hii inaitwa ni ni kuepuka vyanzo vya hatari ya moto kabisa (risk avoidance). Hii ni njia ngumu kabisa kutekelezeka katika

Njia ya pili, ni kuendeleya na matumizi ya vitu vya moto na huku kuweka mitambo mbalimbali ya kugunduwa moto ukiwaka (fire sensors and alarms), njia za kuzimia maji za uhakika (fire water pipes), kamati za kuangalia na kutathmini majanga (crisis au disasters committees) ambazo zinaweza kuchukuwa hatuwa ya haraka janga linapotokeya n.k. Njia hii inalenga kupunguza athari ya uharibifu wa moto (risk reduction measure). Bado moto unaweza kutokeya na kuleta athari kiuchumi.

Njia ya tatu, ni kuhamisha athari ya kiuchumi ya janga la moto kwa kukata bima (Insurance -risk transfer). Kwa kupitiya bima ya moto, linapotokeya janga la moto katika nyumba au kiwandani au ofisini, kampuni ya bima itakuja kulipa gharama ya hasara iliyotokana na moto huo. Hivyo, bima inapunguza au kuondosha mzigo wa gharama ambazo zingehitajika kurekebisha nyumba au ofisi au kiwanda ili mwenyewe asikose makazi au asipatwe na gharama za kuijenga ofisi au nyumba kutoka mfukoni mwake. Lakini maisha ya watu hayawezi kurejeshwa kwa bima yoyote ile.

Kwa bahati mbaya na masikitiko makubwa, bima ya moto na zote zilizopo nchini ni HARAMU kwa waislamu kwa kuwa zinakwenda kinyume na sheria za mikataba ya biashara ya Kiislamu. Mikataba wa bima zilizopo unahusisha riba na kukosa uadilifu baina ya pande mbili. Jambo hili linawakera mno waislam na hasa ukizingatiya kuwa ipo njia mbadala nayo ni bima ya Kiislam (Takaful).

Harakati za kuomba kuwepo bima hii nchini zimeanza kitambo. Tangu mwaka wa 2012, mamlaka ya Bima (TIRA) ilifanya utafiti juu ya uwepo wa haja ya bima hii na utafiti huo ulionesha kuwa bima ya Kiislamu inahitajika nchini. Miaka iliyofuata mamlaka iliandaa taratibu za kutoa leseni na usimamizi wa bima aina hii (Takaful regulations) ambazo zilijadiliwa kwa kina na wadau na wataaalamu mbalimbali nchini hadi kuhitimishwa kwa ajili ya kusainiwa na kupelekwa Wizara ya Fedha. Mwaka 2018, katika mkutano wa kila mwaka wa Bima nchini uliofanyika Tanga, Waziri wa Fedha Mh. Mpango alikiri kuwa taratibu za bima hii zimechukuwa muda mrefu kukamilika na kuwa Waziri ataingilia kati (ministerial interventions) ili ziweze kusainiwa na kutumika.

Mwaka na miezi sasa tangu kauli hiyo itolewe, hatuna taratibu hizo na ilhali zipo kampuni ambazo zipo tayari jana kabla ya leo kuwekeza katika uendeshaji na utoaji wa bima hii nchini. Fursa za ajira zinapoteya na Mali za waislamu zinakosa bima ya Kiislamu mpaka kuangamiya kwa moto bila fidia kutokana na Waziri kushindwa au kulegalega katika kuidhinishwa kwa taratibu za bima hii. Hatutaki kuamini kuwa Waziri anashawishiwa na makampuni shindani yanayoona yatakosa biashara iwapo bima hii itaruhusiwa. Pia hatutaki kuamini kuwa Waziri hatambui haja na hamu kubwa ya Waislam na wananchi wote kuwa na bima yenye kusimama katika uadilifu.

Hivyo, tunamkumbusha kwa unyenyekevu mkubwa Waziri na wafanya maamuzi katika Wizara ya fedha, kuharakisha kupitishwa kwa taratibu hizo ili tuweze kupata wawekezaji zaidi katika huduma za bima nchini, kutengeza ajira, kuongeza matumizi ya bima kwa wananchi, kueleta ushindani na muhimu zaidi kuwawezesha waislamu kutumiya bima ambayo itawaezesha kupata fidia ya hasara za maafa ya moto na mengineyo.



Tuesday, July 14, 2020

UCHUMI WA KATI NA JAMBO LILILO MUHIMU ZAIDI


Siku chache zilizopita nchi yetu ilitangazwa kuwa sasa ni nchi yenye uchumi wa kati (middle income country). Wanasiasa wanaongoza serikali walitumiya fursa hiyo kudhihirisha furaha yao kwa kuona juhudi za muda mrefu zimezaa matunda. Wachumi wanaona hatuwa hii inafaida zake na hasara au changamoto zake. Na hili ni jambo la kawaida, iwe furaha kwa wanasiasa au iwe uchambuzi wa pande mbili -faida na hasara- kwa upande wa wachumi

Makala haya hayalengi kuwa upande wa wanasiasa wala wachumi wenye kupima maendeleo katika mizani ya pato la taifa. Makala haya inataka kubainisha kuwa pamoja na lengo hili la kuwa uchumi wa kati kufikiwa, tusisahau yaliyo muhimu zaidi na ambayo wenzetu waliondeleya (developed countries) wanalenga kulifikiya badala ya kuongezeka pato la taifa tu. Hii haimaanishi kuwa ongezeko la pato la taifa sio muhimu, la hasha. Lakini tufahamu kuwa ustawi wa nchi na watu wake haupo katika kuongeza kipato peke yake. Iwe kipato halisi au kama washindani waliokuwa nje ya serikali wanavyoona kuwa ni kipato cha katika makaratasi!

Wachumi wa Kiislamu kwa miaka mingi wamefikiria na kulenga katika kuelekeza sera za nchi katika kukuza kipato cha mwananchi kwa upande mmoja na kuhakikisha kuwa wananchi wanafuraha (Happiness). Hili la kipato linalenga kuhakikisha wananchi wanaondoka katika mtihani wa ufukara jambo ambalo
Mtume s.a.w alikuwa akimuomba Mola wetu amuepushe na ufukara. Na suala la kuwafanya watu wawe na furaha ni katika mafunzo ya Mtume s.a.w pale aliposema; amali au kitendo kizuri ni kufanya jambo kwa ndugu yako akafurahi au kuingiza furaha kwa ndugu yako!

Katika miaka ya 2010, wanasiasa na wachumi wa nchi zilizoendeleya wamezinduka kuona kuwa kile ambacho kwa miaka mingi wamekishughulikiya nacho ni kuongeza kipato cha watu wao,kuwa matajiri zaidi wakitarajiya kuwa kwa utajiri huo matatizo yote yatakwisha lakini la kustaajabisha ni kuwa pamoja na kuongezeka kipato katika nchi ya Amerika na Ulaya, lakini tafiti zinaonesha furaha haikuongezeka! Profesa Richard Layard na wenzake katika kitabu chao "The Origins of Happiness (2019)", wanauliza swali hili "jambo gani muhimu zaidi kwa mwanandamu (what matters most?) na kujenga hoja kadhaa kuwa fedha zilionekana kuwa ni muhimu mpaka hivi karibuni watu wakiipa fedha nafasi ya heshima. Lakini sasa hivi watu wengi duniani wameona na wanataka kutazamwa upya dhana ya maendeleo. Watu hawa wanakataa kuwa utajiri na kipato kuwa sera za maendeleo ya nchi na mtu binafsi yasiweke mbele zaidi kipato kikubwa kama ishara ya maendeleo na badala yake maendeleo yapimwe kwa kutazama watu wangapi wana furaha na maisha yao. Hivyo watunga sera wanapaswa kuzielekeza sera zao katika kuweka mazingira ambayo watu watakuwa na ustawi na furaha.

Kwa kulitambuwa jambo hili na umuhimu wake, nchi ambazo ni sehemu ya OECD wameazimiya kuwa sera za nchi zao zijielekeze katika ustawi na watu wao wawe na furaha. Hivi sasa kuna nchi kadhaa ambazo zimefikiya kuwa na mawaziri wa kuhakikisha watu wanaishi kwa furaha (Ministers for Happiness) kama vile UAE na sehemu nyingine. Umoja wa Mataifa umeifanya Machi 20 kila mwaka ni siku ya kimataifa ya furaha (International Day of Happiness).

Kadhalika tafiti na ripoti zimekuwa zikifanywa na kuchapwa kila mwaka ili kupima kiwango cha furaha cha wananchi wa nchi mbalimbali duniani. Kwa mfano ripoti ya mwanzo ilichapwa mwaka 2012 na ripoti ya mwaka huu -World Happiness Report 2020, inaonesha kuwa Tanzania ipo chini katika kuwa na watu wenye furaha! Bila shaka, ripoti hizo zinaweza kubishaniwa na hoja kutolewa za kuunga mkono au kuzipinga ripoti hizo. Ikiwa tutaziunga mkono au kinyume chake, jambo moja tunapaswa kukubaliana kama watanzania katika kuendeleza uchumi wa watu wetu nalo ni tusisahau yale ambayo yanawapa ustawi na furaha wananchi wetu! Jambo hili hatuna budi kulitazama kwa kina na kulipima wenyewe kila mwaka au baada ya miaka ili tuhakikishe kuwa kukuwa kwa kipato kunaenda sambamba na kuongezeka furaha na sio karaha au kuongezeka matatizo ya akili au watu kujitowa uhai bila sababu kama ilivyo leo katika nchi nyingi zilizoendeleya.

Katika kufikiya azma hii, Mtume s.a.w anatukumbusha na kutufunza aliposema "Katika mambo yenye kumpatiya mtu furaha ni kuwa na jirani mwema, kuwa na chombo kizuri cha usafiri na kuwa na makazi yenye nafasi."Wale ambao wamejaaliwa mambo hayo matatu basi wakithirishe kushukuru, na wale ambao wamekosa hayo, ni wajibu wa watunga sera kuweka mazingira mazuri ili vitu hivi avipate kila mwananchi wa Tanzania pamoja na kuwa na elimu bora na huduma bora za afya, maji safi, umeme wa uhakika, haki za binadamu zenye kuheshimiwa n.k. Tuanzie katika familiya zetu, mitaani, kata, vitongoji, vijijini, wilayani, mkoani na taifa lote kwa ujumla. Sote twenye dhima ya uongozi katika maeneo hayo, tutekeleze wajibu wetu wa kuweka mazingira mazuri ya ustawi na furaha!

Tuesday, July 7, 2020

UCHUMI WA KIISLAM NA UCHUMI WA KIBEPARI


Ulimwengu umeshuhudia aina kuu mbili za mifumo ya uchumi. Mifumo ya uchumi ya wanadamu na mfumo wa uchumi wa Mwenyezi Mungu. Watu walipojieka mbali na muongozo wa dini zao, waliunda dini mpya na mifumo mipya ya kuendesha maisha yao kwa kutarajiya kupata maendeleo au furaha au ustawi wa jamii zao. Je wameyapata maendeleo, furaha na ustawi wa jamii zao? Na je maendeleo au furaha au ustawi huo unaishia maisha ya dunia pekee au na maisha baada ya kifo? Yoyote yule anayejishughulisha na uchumi binafsi, wa jamii au wa nchi, yampasa ajiulize iwapo njia au mikakati anayofuata itampa utulivu duniani na malipo akhera. Hili ni suali muhimu ambalo yataka turudi katika kulinganisha baina ya mfumo wa uchumi wa Kiislamu na mfumo ya wanadamu kwa mfano ubepari (capitalism).

1. Itikadi.

Mfumo wa uchumi wa Kiislamu umejengwa na kusimama katika kuamini uwepo wa Muumba wa ulimwengu na walimwengu, Mwenye kuruzuku neema mbalimbali ni Mola mmoja asiyekuwa na mshirika. Ameumba ulimwengu kwa ajili ya matumizi ya mwanadamu na shughuli zake za kiuchumi hazina budi kutambuwa mchango wa Mola katika natija anayoipata. Je umeona moto ambao mnautumia? Je ni nyinyi ambao mlioanzisha au ni yeye? Je mmeona maji mnayokunywa? Ni nyinyi mlioyateremsha katika hazina zake au ni yeye? Je mmeona mbegu mnazozipanda ardhini? Je ni nyinyi mnaootesha mazao mbalimbali kwa mbegu hizo au ni yeye? (Surat Waqiah). Kiitikadi, mfumo huu unatambuwa kuwa yupo ambaye bila yeye hamna linalowezekana kwa juhudi ya mwanadamu peke yake. Hii haimaanishi kuwa mtu asijishughulishe, hapana afanye harakati mbalimbali za kujileteya maendeleo huku akijuwa kuwa hizo ni sababu tu na yeye Mola ndio anayesababisha sababu hizo zilete matokeo fulani. Hivyo, kwa kwa itikadi hii, yeyote anayejishughulisha katika kukuza uchumi wake na wa watu wake, hana budi vilevile kutambuwa mipaka iliyowekwa na yule ambaye ulimwengu ni milki yake. Kuna shughuli ambazo amezihalalisha na nyingine ameziharamisha. Hivyo uchumi wa Kiislam, unaona rasilimali zilizopo ni fadhila za Mola kwa wanadamu, zinatakiwa kutumika kwa njia ya halali, kuimarisha ustawi wa mtu na jamii yake na matokeo ya matumizi hayo daima yaambatane na shukrani kwa Muumba.

Mifumo ya uchumi wa kibinadamu inasimama katika kuamini kuwa ulimwengu umejitokeza tu bila kuumbwa na Mola. Nadharia mbalimbali za kuibuka kwa ulimwengu zimearifu kuwa Ulimwengu ulitokeya tu. Rasilimali hizi ni chache na hivyo hamna budi kufanya juhudi ya kila namna ili kuweza kuzimiliki rasilimali hizo kwa maslahi binafsi(ubepari) au maslahi ya jamii yote (ujamaa). Mfumo wa kibepari umeyaweka maendeleo na furaha na ustawi katika matashi na juhudi za mtu mwenyewe. Ni wewe mwenyewe unayeweza kujiendeleza au kujididimiza. Ukitumia rasilimali vizuri utapata natija nzuri au ukitumia rasilimali vibaya utapata matokeo mabaya, suala la uzuri na ubaya ni kwa mizani ya mwanadamu mwenyewe. Apataye ni mwerevu na aliyekosa ni mlegevu! Hamna la halali au haramu isipokuwa lile ambalo sheria za nchi imebainisha kuwa ni halali au haramu hata kama sheria hiyo inaenda kinyume na Sheria ya Mwenyezi Mungu. Hivyo, rasilimali zilizopo ni chache, ni zawadi ya asili, anayezimiliki ni mwerevu na kuzitumia rasilimali hizo ni kwa matashi binafsi ya kujipatiya furaha na ustawi kwa mtu binafsi bila kujali ustawi wa jamii nzima.

2. Uzalishaji Mali.

Mfumo wa uchumi wa Kiislamu unahimiza katika kuzalisha mali. Mali hiyo ni kila kitu chenye manufaa kwa watu katika maisha yao. Mali hiyo iwe ni zao la kazi ya halali na sio wizi au kwa hila mbalimbali. Mali inazalishwa kwa kulima, kuvua, kuzalisha, kutengeneza, kununuwa na kuuza n.k. Binadamu katika kuzalisha mali hana budi kuchunga asizalishe mali kwa njia za haramu au asizalishe mali haramu.

Mfumo wa kibepari pia unahimiza kuzalisha mali mbalimbali ili kupata utajiri ambao utatumiwa kwa maslahi ya mwenye mali mwenyewe. Mali hiyo ni kitu chochote kinachoweza kumilikiwa. Uzalishaji ni jambo huru kwa mtu kuamuwa mwenyewe anataka kuzalisha nini. Haidhuru kitu hicho kiwe ni kwa manufaa au chenye madhara kwa watu kwa mfano wa sigara, dawa za kulevya, ulevi, mirungi, filamu za ufuska, biashara ya bidhaa feki nakadhalika. Uhuru wa mtu ni kitu kitakatifu katika ubepari kiasi ambacho dola inawajibu wa kuulinda uhuru huo hata kama unamleteya madhara huyo mwenye kupewa uhuru huo. Hivi karibuni, huko amerika imekuwa halali kulima na kuvuta bangi katika baadhi ya majimbo ya nchi hiyo. Baada ya uzalishaji sigara, pombe na picha za ufuska, sasa bangi pia ni rukhsa na pengine wakaruhusu dawa za kulevya siku za usoni.

3. Matumizi ya Mali.

Mfumo wa Uchumi wa Kiislamu unahimiza matumizi ya wastani ya mali na matumizi yenye kujali wengine. Mali uliyonayo ni amana kwa matumizi yako ya msingi na pia kuwatazama wengine. Uislam unakataza matumizi ya anasa na israfu na uharibifu wa mali. Kama ilivyokuwa katika kuchuma kwa kufuata amri za Mungu, na katika kuitumia pia ni lazima kufuta maelekezo ya Mungu. Mungu ameelekeza kuwa mali itumiwe kwa wastani kwa ustawi wa mwenye mali na familia yake, na jirani zake na jamii yake.

Mfumo wa kibepari unaona suala la matumizi ni eneo la uhuru wa mtu lisilokuwa na mipaka. Kama alivyotafuta kwa nguvu zake na matumizi ni kwa matashi yake. Hamna kizuizi katika matumizi isipokuwa sheria za nchi ambazo hata hivyo baadhi yake zinaonekana kuwa ni kandamizi dhidi ya uhuru wa binadamu. Mfumo huu kwa uhalisia unahimiza matumizi ya anasa na israfu na kununuwa vitu mara kwa mara (consumerism) kama njia ya kuthibitishia wengine kuwa wewe ni mwenye uwezo wa kumudu chochote ukitakacho. Mfumo huu unahimiza mashindano ya vitu badala ya utu. Wajibu wa mtumiaji mali unaishia katika kujistawisha na kujifurahisha yeye mwenyewe hata kama umezungukwa na majirani wanaolala na njaa au wanauguwa maradhi mbalimbali kwa kushindwa kumudu gharama za matibabau au kuishi katika ujinga kwa kushindwa kumudu gharama za elimu.

4. Usambazaji wa Mali.

Mfumo wa uchumi wa Kiislamu umeweka njia mbalimbali za kuigawa mali miongoni mwa wanajamii ili wote wawe na ustawi unaohifadhi heshima ya binadamu kama kiumbe bora ulimwenguni. Njia ya Zakat ni moja wapo. Kila mwenye mali analazimika kila mwaka kugawa sehemu ndogo ya mali yake kwa ajili ya wale ambao hawana kitu ili na wao waweze kufurahi na kustawi katika jamii yao. Mali inapaswa kuzunguka na sio kuhodhiwa na wachache! Njia nyingine ni sadaka na waqfu ambazo zinapelekeya mali kugawiwa kwa watu mbalimbai katika jamii ili kuinuwa hali zao.Serikali yenye kufuata mfumo huu, inajali raia wake kwa kuhakikisha wale ambao hawana uwezo wa kujikimu wanasaidiwa na serikali kupata mahitaji ya msingi yenye kuhifadhi utu wao na heshima yao.

Imesemwa kuwa Ubepari hauna roho. Kila kinachopatikana baada ya kutowa kodi stahiki (na mara nyingi kodi hiyo huepukwa kwa udanganyifu), mwenye mali hana wajibu wa kumsaidiya yoyote. Yoyote mwenye shida arudi kwa serikali yake, kwa msaada. Sio wajibu wa mfanyabiashara au mwenye mali kuhakikisha mali hiyo inawasaidia wengine katika jamii yake na hata kwa familia yake. Mzazi katika mfumo wa kibepari hana wajibu hata wa kumsaidia mwanawe aliyebaleghe kwa kumpa mtaji wa bure, mtoto katika umri huo ni wa serikali kumtazama na kujitafutia mwenyewe. Ni mimi mimi! (Man eat man society). Hakuna cha bure katika ubepari. Imesemwa ukipewa cha bure ujuwe wewe ndio bidhaa yenyewe ambayo inauzwa kwa wengine! Tunayaona haya katika mitandao ya kijamii. Ni bure kujiunga lakini kumbe taarifa zetu za kimtandao zinauzwa kwa pesa nyingi kwa wengine!


5. Fedha (Capital).

Mfumo wa uchumi wa Kiislam unaona kuwa fedha au mtaji unanafasi yake lakini sio mama wala msingi mkuu wa uzalishaji. Bali binadamu, mwenye nguvu kazi na maarifa akisuhubiana na mtaji unaohitajika hupelekeya katika uzalishaji na hivyo viwili hivyo havitengani katika uzalishaji. Fedha inahitajika kujumuika na binadamu mwenye maarifa na ujuzi katika uzalishaji wenye tija. Hivyo, vyote viwili vinatakiwa kuthaminiwa kwa uadilifu na bila kimoja kumuelemeya mwenzake kuwa ni eti ni bora zaidi. Hivyo ni marufuku katika uchumi wa Kiislam, mwenye fedha kutowa fedha kwa mkopo na kudai nyongeza bila kuwa tayari kubeba hasara inayotakana na shughuli inayofanyika na fedha hizo.

Ubepari (Capitalism) unaona kuwa fedha na mtaji ndio mama na msingi mkuu wa uzalishaji. Hivyo fedha pekee inaweza kuzalisha fedha nyingi zaidi kwa kokopeshwa kwa riba mara dufu na kumpatiya mwenye mtaji huo fedha zaidi bila kujali mchango wa binadamu katika kuzalisha. Watu ni watumishi wa mtaji na hivyo mtaji unastahiki kupata faida zaidi kuliko binadamu anayeufanya mtaji huo uzalishe zaidi. Kwa fikra hizi, ulimwengu leo unashuhudia mpasuko mkubwa sana baina ya matajiri na masikini. Kwa kuwa matajiri hao wanatumia mitaji yao katika kujipatiya faida kubwa kwa mfano wa riba hali ya kuwa wao wenyewe hawafanyi kazi yoyote. Mfumo huu hauzingatii uadilifu baina ya wenye mitaji na wenye kufanya kazi! Si ajabu Bilionea Ray Dalio, amesema kuwa "Capitalism is failing us (Ubepari unatufelisha katika maisha)."

Hitimisho.

Pamoja na kuwa uchumi wa Kiislamu ulishamiri katika wakati wa Mtume s.a.w na makhalifa zake waongofu na athari zake zikiwepo katika dola zilizokuwepo chini ya himaya ya Ukhalifa, leo ni nchi chache ambazo zina mwelekeo wa kushikamana na uchumi wa Kiislam. Habri nzuri ni kuwa mfumo wa uchumi wa Kiislam umekuwa ukifanyiwa utafiti kwa muda sasa ili uweze kufuatwa katika zama hizi baada ya kuwa ulipigwa vita baada ya kuanguka dola za Kiislam na kuingia ukoloni wa nchi za magharibi ambao ulifanya juhudi ili kufuta athari ya uchumi huu.

La kusukitisha zaidi ni kuwa binadamu katika zama hizi, wengi wetu tumekuwa mabepari na mifumo ya uchumi wetu imekuwa ikielekeya katika mfumo huo zaidi kuliko mifumo mingine. Hata hivyo, zipo tofauti katika mfumo huu wenyewe, kuna ubepari wa dola (State / political capitalism) ukiongozwa na China na ule wa nchi za kimagharibi (Liberal capitalism). Mwandishi wa Capitalism Alone, bwana Branko ameeeleza kwa undani kushamiri kwa aina hizi za ubepari na dosari zake akisisitiza kuwa mabadiliko lazima yafanyike haswa katika ubepari wa nchi za magharibi. Katika maependekezo yake, ameshauri dola zifanye yafuatayo:
1. Kuhamisha mitaji na umiliki wa mitaji hiyo kwa kuwapa nafuu ya kodi watu wenye vipato vya kati na kuwatoza kodi kubwa kabisa matajiri na kuweka kodi katika mali za mirathi. (deconcentrating capital and wealth ownership through tax advantages that give the middle class a bigger stake in financial capital and a corresponding increase in the taxation of the rich, coupled with higher taxes on inheritance).
2. Serikali zifanye uwekezaji mkubwa katika kuboresha elimu na kutowa fursa sawa kwa wazalishaji na wawekezaji. Hii inajumuisha serikali kufanya biashara na wawekezaji wa kati kwa kuwapatia tenda mbalimbali. (He also calls for a significant boost in public investment to broaden access to high-quality education and enhance equality of opportunity.)
3. Serikali kuweka kikomo cha michango ya matajiri kwa wanasiasa au vyama vyao na watunga sera mbalimbali ili matajiri hao wasihodhi mfumo wa kisiasa na kujinufaisha zaidi kupitiya wanasiasa ambao watakuwa wanawafungulia njia zaidi za kumiliki mitaji na kuwekeza pasi na ushindani ulio wa haki. (Strictly limited and exclusively public funding of political campaigns to reduce the ability of the rich to control the political process is another necessary reform).

Hizi ni hatuwa za mwanzo na mengi zaidi yanapaswa kufanywa ili kuiepusha nchi kama Tanzania, isije kujikwaa katika dosari za ubepari wa kimagharibi.