Pages

Sunday, June 28, 2020

BAJETI YA TANO NA MZIGO WA RIBA




Kama ilivyo kawaida, mwezi huu Mh. Waziri wa Fedha alisoma bajeti ya tano ya serikali. Bajeti hiyo imesifiwa na wadau mbalimbali kuwa ni bajeti nzuri na yenye ahueni kwa wananchi. Kwa hakika, uzuri wa kitu hujidhihirisha katika midomo ya watu na ahueni huhisiwa na watu. Pamoja na hayo, hakuna kazi binadamu ambayo yenye ukamilifu katika uzuri wake hata ikiwa tutataka na hakika hii inajidhihirisha katika maeneo mengi ya shughuli na kazi za binadamu.

Hivyo, bajeti ni nzuri lakini yapo maeneo ambayo kwa mtazamo wangu naona yatazamwe sana na kurekebishwa siku za mbele.

Eneo la kwanza, mzigo wa riba! Bajeti hii ni ya Trilioni 34.88. Katika matumizi ya bajeti hii, trilioni 22.10 au 63% ni za matumizi ya kawaida na asilimia 37% ni za matumizi ya maendeleo. Katika hii trilioni 22, trilioni 2.8 au 12% ni malipo ya riba peke yake, ukiongeza za mtaji utakaolipwa inafika trilioni 8.5 au asilimia 38% ya bajeti ya matumizi inaenda kulipa deni na riba zake.

Na mwaka huu serikali inatarajiya kukopa trilioni 4.9 kutoka katika soko la ndani. Hii itaongeza deni na itaongeza riba. Katika kiasi hicho, trilioni 3.32 sawa na 67% ya mkopo huu wa tril 4.9 ni kwa ajili ya kulipa madeni ya nyuma yalioyoiva (you borrow from John to pay Tom) na kiasi kilichobaki ni kwa ajili ya shughuli za maendeleo. Tukirudi katika nukta ya msingi ni kuwa tuna riba ya tril 2.8 ya kulipa mwaka huu peke yake. Tril 2.8 ni pesa nyingi kwa taifa letu kulipa kama Riba. Kwa mfano, bajeti yote ya elimu ni trilioni 1.3, Wizara ya Afya peke yake ni Bilion 933. Hivyo riba tunayolipa ingeweza kuongeza bajeti yetu ya elimu na Afya, na kubakiwa na chenji!

Nilifanya hesabu ndogo kuona kila mwananchi analipa riba ya kiasi gani. Hivyo tril 2.8 ukigawa kwa watu takribani milioni 57, ni kiasi cha riba ya Shilingi elf 49 ambayo kila mmoja wetu anachangia katika riba hiyo itakayolipwa. Hivyo, kila mmoja wetu anataka au la, japokuwa baadhi yetu ni dhambi kubwa sana kukopa na kulipa mikopo ya riba hata iwe ni kwa sh 10, tunalipa kiasi hicho kwa kupitia kodi zetu mbalimbali. Hivyo ni dhahiri, ubunifu unahitajika katika sera zetu za fedha katika suala la ukopaji na tukiongozwa na kumuogopa Mungu aliyeharamisha riba, basi tutapata njia.

Wenzetu wa Sudan na Irani, wameiepuka riba kabisa katika uendeshaji wa nchi zao. Hivyo,inawezekana! Naiomba serikali ijitahidi kubuni njia zisizo za riba kwa kujifunza kutoka katika nchi hizo na Malaysia n.k, ili kugharamia miradi ya maendeleo nchini. Rais Obasanjo amepata kusema "If you ask me what is the worst thing in the world, I will say it is compound interest.(Ukiniuliza mimi, kitu kibaya zaidi ulimwenguni, nitasema kuwa ni riba juu ya riba!)” Pope Francis amesema "“Usury humiliates and kills (Riba inadhalilisha na kuuwa).” Pia amesema, “Usury is a grave sin. It kills life, stomps on human dignity, promotes corruption, and sets up obstacles to the common good. (Riba ni dhambi kubwa, inaua maisha, inachafuwa heshima ya mwanadamu, inashawishi ufisadi na ni kizuizi cha kufanya mambo mema.” (https://www.vaticannews.va/en/pope/news/2018-02/pope-francis-usury-financial-exploitation.html).

Katika Uislam, riba ni dhambi yenye kuangamiza. Anayejihusisha na riba ametangaza vita na Mungu! Ni wazi vita hivyo sio rahisi mwanadamu kuishinda. Tuachane na njia hii ya kukopa kwa Riba kama serikali, kama biashara na kama wananchi!

Eneo la pili, ni katika suala la kuondosha kampuni za mawasiliano zinazomilikiwa na serikali kwa 25% na ziada katika takwa la kuorodheshwa katika soko la hisa. Pia kuziondoa kampuni zenye kumiliki minara ya mawasiliano zisiwe sehemu ya makampuni yanayotakiwa kuorodheshwa katika soko la hisa la Dar es salaam. Pendekezo hili waziri ameeleza mantiki yake ni kuhakikisha serikali inabaki na hisa hizo na kupata faida zaidi badala ya kuzipunguza iwapo kampuni hizo zitaorodheshwa katika soko la hisa. Tukifuata mantiki hii, hatutoweza kulikuza soko la hisa ipasavyo kwa kuwa inaonesha kuwa serikali ni mchoyo (state is greed) katika hisa zake katika makampuni ya mawasiliano na hivyo wenye makampuni ya binafsi hawatashawishika kuuza hisa za makampuni yao hapo. Kama serikali ni yenye uchoyo, watu binafsi ni wachoyo zaidi. Kampuni zinazofanya vizuri hazitaona haja ya kuwashirikisha watanzania katika umiliki wa makampuni yao.

Kwa upande mwingine kwa sasa makampuni yaliyopo katika soko la hisa ni machache (27 hivi) wakati Kenya wana zaidi ya makampuni 60. Tunahitaji kutengeza vishawishi (incentives) kwa makampuni mazuri wajiorodheshe katika soko letu hili. Na Mh. Waziri alisema katika bajeti hii kuwa serikali inalenga kutowa elimu ya umma ili kuhamasisha ushiriki wa wananchi katika soko la hisa. Ili lengo hili litimie panahitajika kuwa na uwanja mpana wa makampuni ya kuwekeza. Hebu tafakari iwapo tu watu milion 20, watazikimbilia hisa za kampuni 27 wangapi watapata na wangapi watakosa? Kwa hivyo tunahitaji kuongeza makampuni katika soko la hisa na sio kuzizuia kisheria baadhi zisifanye hivyo. Sasa jambo hili la kuziondoa baadhi ya kampuni, linahitaji kufikiriwa vizuri zaidi na haswa kuweka mikakati yenye kushawishi kampuni nzuri binafsi za ndani na nje ya nchi zijiorodheshe katika soko la hisa.

Kwa leo ningependa kuishia hapa. Ni matumaini yangu kuwa nasaha hizi zinaweza kusaidia nchi yangu na watu wake.