Pages

Friday, June 18, 2021

USHAURI KUHUSU BENKI YA WAJASIRIAMALI

Mheshimiwa Raisi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania akihutubia mkutano wa hadhara na vijana uliofanyika June 2021 mkoani Mwanza aliwaahidi vijana wa Tanzania kuanzisha benki ya wajasiriamali ili kuweza kupata mitaji ya kuanzisha na kuendesha biashara.
Raisi alisema "...Kwa pamoja serikali na mfuko huu (AfDB), tutaanzisha benki ya ujasiriamali kwa ajili ya vijana. Benki hiyo itaanzishwa hapa nchini .. kutatuwa tatizo la mitaji kwa vijana." Ahadi hii imepokewa vyema hususani na vijana kwa sababu inaonesha utambuzi wa mojawapo ya vikwazo kwa vijana katika kujiajiri na kukuza mitaji yao katika shughuli zao za kiuchumi. Ni matumaini yetu kuwa ahadi hii itatekelezwa na katika kutekeleza ahadi hii, napenda nishauri mambo yafuatayo ambayo yataiwezesha benki hii kukidhi kiu ya vijana wote nchini na kufikia lengo la kutatuwa tatizo la mitaji bila kuathiri mtaji wa benki yenyewe. Ushauri. 1. Mtaji wa Banki hii (Source of Capital). Imeelezwa kuwa mtaji wa benki hii utatokana na ushirikiano baina ya serikali na mfuko wa AfDB. Napendekeza benki hii mtaji wake utokane na mapato ya halmashauri ima katika ile 10% au iwepo 10% nyingine. Mapato hayo kutoka halmashauri zote na kuongeza kidogo kutoka katika mfuko mkuu wa serikali kutaepusha haja ya kuwa na ushirikiano na AfDB ambao uendeshaji wake ni kutazama faida ya haraka na kubwa. Umuhimu wa wazo hili la kutumia 10 za hlamashauri unatokana na taarifa za usimamizi wa fedha za 10% kutoka katika halmashauri una changamoto zinazohitaji kuboreshwa nchi nzima. Hivyo, chini ya taasisi ya kibenki iliyo chini ya benki kuu, kunaweza kwa kiasi kikubwa kuondoa baadhi ya dosari zilizopo katika utaratibu wa sasa wa ukopeshaji katika halmashauri na hivyo kuboresha usimamizi wa fedha hizi za wananchi ili zikikopwa zirudi na kukopesha wengine. Muhimu zaidi ni kwamba fedha hizi kutoka halmashauri zote zitawezesha kuendelea kutoa mikopo bila riba kama ilivyo sasa na hivyo kutawawezesha vijana kupata usaidizi mzuri katika miaka ya mwanzo ya uendeshaji wa biashara (start ups) ambao huwa na changamoto nyingi. Mwisho, fedha hizi chini ya utaratibu wa kibenki utapunguza kama sio kuondosha ushawishi wa kisiasa katika utaoji wa mikopo hiyo na pia kuwawezesha vijana waliopo ktk halmashauri zenye makusanyo hafifu kuendelea kupata mitaji zaidi tofauti na ilivyo sasa ambapo 10% ya halmashauri ikiisha, mikopo inakwama kutolewa mpaka mwaka ujao. 2. Bidhaa jumuishi (inclusive and appropriate solutions). Mkakati wa nchi kuhusu mfumo wa fedha jumuishi (NFIF) unataka watoa huduma za fedha kuwa na bidhaa na huduma jumuishi, huduma muwafaka, zenye gharama nzuri, zinazopatikana kwa urahisi nakadhalika. Hitajio hili linailazimu serikali kuwa mfano wa kuigwa kwa kuwa na bidhaa jumuishi zenye kukidhi mahitaji mbali mbali ya vijana katika benki zake na taasisi za uwezeshaji. Kwa mfano, ikiwepo mikopo yenye tozo au riba, vilevile inapaswa kuwepo mikopo isiyotoza riba (interest free) na mikopo ya mali kwa pesa i.e unauuziwa bidhaa kwa faida mnayokubaliana badala ya kupewa hela. Ikumbukwe kuwa tunayo sehemu kubwa ya wananchi na vijana wetu, visiwani na bara ambao kwa utamaduni na imani zao ni haramu kujihusisha na riba. Badala yake wanaweza kukopa mali na kulipa hela au kufanya mashirikiano katika mradi wa biashara na kisha kugawana faida au hasara. Hili ni muhimu kuzingatiwa. Kwa bahati mbaya, taasisi nyingi za usaidizi wa wajasiriamali za kiserikali zilizopo kama vile SIDO, SELF MFI, PASS n.k zinatoza riba na kuwakosesha fursa baadhi ya vijana na wananchi. Dosari hii hainabudi kurekebishwa kwa taasisi zote za serikali nchini kwa kuiga aina mbalimbali za ukopeshaji na uwezeshaji kama vile kutoka katika benki ya zinazotoa huduma bila riba nchini kama vile PBZ Ikhlas, Amana Bank, KCB Sahl, CRDB Al Barakah, NBC La Riba. Aina hizo hujumuisha kununua na kuuza vitu kukidhi mahitaji ya wateja, kukodisha rasilimali na kushirikiana kimtaji na kugawana faida au hasara katika mradi husika. 3. Zaidi ya mafunzo kwa wajasiriamali yanahitajika (More than entrepreneurship trainings). Ni rahisi kuona kuwa tatizo la vijana kutokuwa na ajira ni uhaba wa upatikanaji wa mitaji kwa vijana ili kujiajiri. Hatahivyo, uhaba wa elimu na nidhamu ya ujasiriamali ni kikwazo kikubwa. Hivyo, benki hii hainabudi kuanzisha au kuwa na ushirikiano wa karibu mno na wa kimkakati ili kuziba mapengo hayo. Njia mojawapo ni kutoa mafunzo ya ujasiriamali kutoka kwa wajasiriamali wenyewe sio walimu wa darasani au vyuoni tu (theoretical), kwa kuwa na incubators na accelerators sehemu mbali mbali nchini ili kuziwezesha biashara za vijana na wananchi kuanza, kukuwa na kupanuka zaidi. Nini incubator na nini accelerators? Incubators huwa ni sehemu maalum ambazo hutowa mafunzo mbalimbali ya biashara, nafasi za ofisi kwa bei nafuu na kupata huduma mbalimbali zinazoweza kuisaidia biashara ndogo kuanza na kustawi. Hamna muda maalum wa kuwa katika sehemu hii. Accelerator huwa ni sehemu ambayo waanzilishi wa biashara mpya hukaa na wataalamu wa masuala mbalimbali ya biashara kwa wiki na miezi maalumu ili kuzijenga biashara hizo kifikra, mikakati na mitaji ili kuziepusha biashara kufannya makosa ambayo huweza kujitokeza katika uendeshaji wa biashara zao. Ni lazima mafunzo mazuri na usaidizi wa kitaalamu utolewe zaidi ya upatikanaji au utoaji wa mitaji fedha za kuwakopesha tu vijana wetu. 4. Mabadiliko ya Sheria na kanuni za kibenki (Change of laws and regulations). Tuna mabenki zaidi ya 50 lakini bado mitaji kwa wajasiriamali imekuwa ni kikwazo kikubwa. Moja ya sababu ni kuwa kanuni na sheria za kibenki zilizopo na zinazosimamia uendeshaji wa benki sio rafiki kwa wajasiriamali wadogo ambao hawana dhamana na bado hawajaanza kutekeleza mawazo yao ya biashara. Ili kufanikiwa kwa benki hii ni lazima kuwa na kanuni au sheria nyingine zinahusiana na mitaji, uendeshaji na usimamizi wa benki hii. Huko nyuma tumekuwa na benki ya wanawake chini ya sheria na kanuni zilezile za kibenki, leo haipo tena. Hivyo tutahadhari na ule msemo kuwa "Uchizi ni kufanya yale yale huku ukitarajia motokeo tofauti. "Insanity is doing the same thing and expecting a different results." Pamoja na hili, ushindani wa sekta ya umma na sekta binafsi katika suala la mitaji linapaswa kuepukwa, kwa kuwekwa zuio maalum la kiwango ambacho benki hii itaruhusiwa kuikopesha serikali ili benki ijikite kukopesha na kuwezesha wajisiriamali kwa kuwa hilo ni ndio jukumu lake la msingi. Sambamba na hili umakini mkubwa uchukuliwe kuwa na viongozi na menejimenti nzima ambayo ipo tayari na imejielimisha kwa upana katika kuendesha biashara ya kibenki kwa mtazamo mpya na kwa kuweka mbele ubunifu na ujasiri katika kuwa na bidhaa na suluhisho muwafaka kwa mahitaji ya biashara katika hatua zake zote. 5. Nyongeza katika ahadi. Huduma za kibenki ni njia moja ya kuwezesha wajasiriamali lakini sio njia pekee. Zipo aina nyingine ya taasisi ambazo ni muhimu kuanzishwa kama vile taasisi au mifuko ya kimitaji (Venture Capital firms au funds). Taasisi hizi huwekeza kwa kuwa wanahisa (equity or shareholding) kwa biashara zenye kuonesha uwezo wa kufanikiwa kibiashara, kuwa na mchango mkubwa katika jamii kwa kupitia huduma zake na kufungua fursa zinazokuja kwa uwepo wake. Ni muda muwafaka sasa, serikali kuwa na taasisi yake (government-backed venture capital fund) ya kuwekeza katika mashirika binafsi yanayoonesha uwezo wa kuendeshwa kwa faida badala ya kusubiria na kutegemea mifuko binafsi ya mitaji. Hii iwe ndio njia mbadala au inayoenda sambamba na serikali kushiriki katika umiliki wa mashirika binafsi ndani ya nchi na nje ya nchi. Hitimisho. Ni matumaini yangu kuwa mapendekezo haya yanaweza kuleta tija tunayoitarajia. Muhimu ni kuziandaa fikra na mawazo yetu hususani wale ambao watapewa jukumu hili na Rais kuendesha benki kwa njia ambayo haikuzoeleka lakini iliyojaribiwa na kufanikiwa iwe nchini au nje ya nchi. N ainapobidi kujaribu njia mpya ambazo hazikujaribiwa kabisa kwa uangalifu na umakini.