Pages

Wednesday, May 14, 2025

SERIKALI INAPOKOPA KWA RIBA, UBAGUZI WA FURSA NA HALI YA WAISLAM.

Serikali zote hukopa. Tofauti yao ni madhumun, viwango na namna ya ukopaji. Serikali ya Jamhuri ya Tanzania inakopa kwa njia mbalimbali moja wapo ni kupitia Hati funganiza muda mrefu, au mfupi au mikopo kutoka taasisi za fedha za kibishara na kimataifa. Hivi karibuni serikali ilitangaza Treasury Bond Auction Number 528. Serikali ikikusudia kukopa kuanzia TZS 1mil na itakuwa inalipa riba ya 15.49% kwa mwaka kwa wale watakaoikopesha (neno uwekezaji au investment lisikupe tabu, ni mkopo).

UBAGUZI WA FURSA.

Katika fani ya masuala ya fedha, serikali inapokopa kupitia hati fungani ni fursa kwa wananchi katika kutengeza vipato pale ambapo mwananchi anaikopesha serikali na kuhakikishiwa kuwa atalipwa fedha zake na riba au faida nono ya 15.45% kila mwaka katika mkopo wake kwa muda wa miaka 10 au 20 ijayo.


Je fursa hii ni kwa wananchi wote - waislam, wakristo, wahindu na wengineo? Jawabu jepesi ni kuwa NDIO - watu wote bila kujali dini zao wanaweza kuikopesha serikali. Hatahivyo, jawabu hiyo ni kama mtu anayejifanya kipofu wa uhalisia wa jamii ambayo serikali inaiongoza na kuihudumia. Ni kupe mfano mdogo, unaonaje iwapo Serikali itatangaza kuwa inatoa fursa kuwa sasa Mwanamme au mwanamke atakayeingia katika NDOA YA MKE ZAIDI YA MMOJA atapewa zawadi kila mwaka ya laki mmoja maadamu yupo katika ndoa hiyo, je fursa hii ni kwa watu wote? Waislam na wakristo na wengineo? Jawabu jepesi litakuwa NDIO. Hatahivyo, uhalisia ni kuwa fursa hii ya kuoa na kupewa laki moja kila mwaka (kodi za wananchi wote) itakuwa ni kuwabagua wakristo ambao kwa mafunzo ya Imani yao ndoa ni ya mke mmoja tu. Ama kwa Waislam na wengine, wanaweza kuoa zaidi ya mke mmoja na hivyo ni fursa kwao lakini sio kwa ndugu zao wakristo.



Hivyo, linapokuja suala la KUIKOPESHA Serikali kwa riba, ni wazi kuwa fursa hiyo kwa uhalisia ni kwa WAKRISTO na wengineo na sio kwa Waislam kwa sababu kwa Waislam mikopo yenye kutoza au kutoa RIBA ni Haramu, ni dhambi kubwa! Lakini kwa Wakristo, riba sio dhambi bali kipato halali.


Hivyo kupitia ukopaji wa hati fungani, Muislam anaambiwa fanya dhambi ili upate fedha. Hivyo, muislam anayeshiriki kukopesha kwa riba inaweza kuwa hajui dini yake au ameamua kupata dhambi ilia pate fedha. Je serikali inayoheshimu dini za watu wake na haki yao ya kuabudu, inajisikije kuwafikisha Waislam katika kuwaweka katika hali ya kuchagua baina ya kutengeza fedha na kuchuma dhambi ya kula Riba? Serikali inaonaje pale ambapo Waislam wanakosa fursa hii kwa kujiepusha kwa hiari kwa HOFU YA MUNGU lakini KODI zao zinatumika kulipa riba kwa wananchi wenzao na hivyo wenzao kutajirika bila jasho wakati wao wanalazimika kuchuma fedha kwa kuvuja jasho na kubeba hatari (risk mbalimbali za kibishara n.k)?

NJIA MBADALA.

Kwa kuwa serikali lazima zikope ili kuwezesha miradi mbalimbali ya kimaendeleo na kijamii, hivyo ni jambo la msingi kuwe na njia mbadala ili kufikia lengo hilo. Je mbadala ni upi? Njia mbadala ambayo ni jumuishi kwa wananchi wote -Waislam na wengineo ni kutoa hati fungani ya Kiislam inayojulikana kama SUKUK.


Utaratibu wa Sukuk ni maarufu duniani na kwa mataifa mbalimbali. Nchi kama Nigeria, Afrika Kusini, Sudan, Gambia, Senegali, Malaysia, Indonesia na kadhalika zimekuwa zikitumia utaratibu wa Sukuk kwa ajili ya kupata fedha za maendeleo kwa njia ya miamala isiyohusisha Riba na hivyo kuwajumuisha katika fursa ya uwekezaji wananchi wote. Hivi karibuni, serikali ya mapinduzi ya Zanzibar imezindua ZANZIBAR SUKUK kwa mafanikio makubwa.

Naamini na nafahamu kuwa Serikali yetu inatambua utaratibu huu wa Sukuk (imetajwa katika Mpango wa tatu wa Miaka Mitan -FYDP III) na hivyo niwakumbushe Wizara ya Fedha, kuwa Waislam wanasubiri kwa hamu kuona serikali yao inawajumuisha katika fursa za uwekezaji Halali kupitia Sukuk na wanachukizwa kuona kuwa fursa hiyo imeendelea kufinywa kwao kwa muda mrefu bila ya sababu zinazofahamika.

Tuesday, April 22, 2025

BARUA YA WAZI KWA MHESHIMIWA RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA - OMBI LA KUFUNGULIWA KWA DIRISHA LA HUDUMA ZA KIBENKI ZA KIISLAM KATIKA BENKI YA USHIRIKA



Mheshimiwa Rais,
Salaam Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh.
Kwa heshima na taadhima, napenda kuchukua fursa hii kukuandikia barua hii ya wazi, nikieleza maombi na mapendekezo kwa lengo la kuunga mkono juhudi zako za kuleta maendeleo jumuishi na ustawi wa Watanzania wote bila kujali hali zao za kiuchumi, kijamii wala kidini.

Mheshimiwa Rais,
Tanzania ni nchi ya watu wenye imani mbalimbali, na kwa miongo kadhaa tumeendelea kuishi kwa mshikamano, amani na kuvumiliana. Katika kuhakikisha maendeleo hayo yanamgusa kila Mtanzania, serikali yako imeweka msisitizo mkubwa katika utekelezaji wa *Sera ya Taifa ya Ujumuishi wa Kifedha(The National Financial inclusion framework)*, ambayo inalenga kuhakikisha kuwa wananchi wote wanapata fursa ya kushiriki kikamilifu katika mifumo rasmi ya kifedha kwa ustawi wao binafsi na wa taifa kwa ujumla.

Hata hivyo, kuna sehemu ya wananchi ambao kutokana na misingi ya imani yao ya dini, wanakosa huduma stahiki za kibenki zinazooana na misingi ya imani yao – hasa Waislamu wanaofuata mfumo wa fedha za Kiislam (*Islamic Banking*), unaokataza riba (*riba/usury*) na kuweka mkazo kwenye usawa, uwazi, na kushirikiana katika faida na hasara (*profit and loss sharing*).

Hivi karibuni kumekuwa na juhudi kubwa zikiongozwa na Waziri wa Kilimo Mh. Bashe juu kuanzisha Benki ya Ushirika nchini ambayo inatazamiwa kuwa Mheshimiwa Rais utakuwa ni mwenye kuifungua ifikapo April 28 mwaka huu. Kauli mbiu katika sherehe za ufunguzi wa benki hii ni kuhusu ujumuishi wa kifedha na ugawaji sawa wa fursa *Driving Financial Inclusion, shared prosperity.* Benki ya Ushirika ni chombo muhimu chenye dhamira ya kuwakwamua wananchi wa kipato cha chini na wa kati, hasa wale walioko vijijini na kwenye sekta isiyo rasmi. Kwa kuwa tayari benki hii inalenga kuwafikia wananchi waliotengwa kifedha, tunapendekeza kuwa dirisha maalum la huduma za Kibenki za Kiislam lifunguliwe ndani ya Benki ya Ushirika ili:
1. Kuongeza ujumuishi wa kifedha kwa Waislamu na wengine wanaotaka mfumo mbadala wa kibenki. Hii itawawezesha kushiriki kikamilifu katika shughuli za kiuchumi au kibenki bila hofu ya kwenda kinyume na misingi ya dini yao.

2. Kuchochea maendeleo ya kiuchumi kwa makundi yaliyo pembezoni. Huduma hizi zitawavutia wananchi wengi waliokuwa hawatumii huduma za kibenki, hivyo kukuza ujumuishi, mzunguko wa fedha na uwekezaji.

3. Kukuza ushindani wa haki miongoni mwa taasisi za fedha. Mfumo wa huduma za Benki za Kiislam huwekeza kwa kushirikiana na mteja (kwa mfano kupitia uwezeshaji kwa njia ya *murabaha*, *mudaraba*, au *Salam*), na hivyo kuchochea uwajibikaji, ushirikishwaji na ustawi wa kijamii.

4. Kutekeleza kwa vitendo sera ya Taifa ya Ujumuishi wa Kifedha. Dirisha hili litakuwa mfano hai wa utekelezaji wa sera hiyo, ikionyesha dhamira ya kweli ya serikali katika kuwajumuisha wananchi wote – bila ubaguzi.

Mheshimiwa Rais,
Dirisha hili la huduma za Kibenki za Kiislam linaweza kuanzishwa kwa mafanikio makubwa kwa kuwa benki kuu inayouzoefu wa kusimamia utolewaji wa huduma hizi nchi, tunao wataalamu wa kutosha tena vijana waliosomea shughuli za kibenki za Kiislam wenye uzoefu ambao wanaweza kusimamia huduma hii kwa mafanikio makubwa. Mimi binafsi ni mfano wa vijana hao ambao nimeshirikiana na wengine kuhakikisha tunasaidia benki zetu kuwa na huduma jumuishi nchini.

Tuna imani kubwa na uongozi wako unaojali maslahi ya watu wote, na tuna matumaini kuwa ombi hili litapewa uzito unaostahili kwa ajili ya kujenga taifa jumuishi, lenye haki, amani, ustawi na fursa sawa kwa wote. Kadhalika naomba ombi hili ambalo naamini utaridhia lifanyiwe kazi kwa kushirikiana na chombo chetu cha wataalamu cha CIFCA (Center of Islamic Finance and Advice) na kulifanyia kazi katika taasisi zote za Umma nchini kama vile TADB, Azania Bank, TCB, SELF Mirofinance na taasisi nyingine zinazohusika na uwezeshaji wananchi kiuchumi.

Kwa heshima na taadhima,

Nakutakia mafanikio mema katika kuongoza Taifa letu katika maendeleo, uongofu na njia ya sawa sawa.

Tuesday, March 25, 2025

ZAKATUL FITRI

Imeandika na Sheikh Tawakkal Juma.
1. ✨ MAANA YA ZAKATUL-FITRI
Ni zaka maalumu inayotolewa baada ya kumalizika mfungo wa mwezi wa ramadhan. - imeitwa hivyo kwa sababu inawajibika kwa kuingia siku ya idd-el-fitri. - Piah inaitwa zaka ya viwiliwili na kufungua miili kwa sababu inawajibika kwa kila nafsi na sio katika Mali. - Zama hii imefaradhishwa mwaka wa pili Hijiria baada ya kufaradhisha funga ya ramadhan.
2. HUKUMU YAKE
Ni wajibu kwa kila muislamu mwanaume na mwanamke, mdogo na mkubwa, aliyehuru au mtumwa anapaswa kuitoa baada ya funga ya Ramadhani kabla ya kuswali swala ya Iddil-Fitri. - Watoto, wanawake, wazee n.k wasio na uwezo wa kulipa Zakatul-Fitri watalipiwa na mawalii wao (wasimamizi wao). - Kwamfano katika familia baba atamtolea mkewe na watoto wake ikiwa hawawezi kujitolea, pia atawatolea wazazi wake kama nao pia hawana uwezo wa kujitolea, vilevile baba atalazimika kuwatolea Zakatul-Fitri wale wote wengine ambao ni waislamu walio chini ya uangalizi wake na hawawezi kutoa Zakatul-Fitri. - Hata mtoto mchanga aliyezaliwa dakika chache kabla ya kuandama kwa mwezi naye pia atatolewa Zakatul-Fitri.
3. WANAOPASWA KUTOA ZAKATUL FITRI
- Zakatul Fitri inamlazimu yeyote yule mwenye kupata chakula cha kumtosha yeye na wale waliochini ya uangalizi wake kwa mchana wa siku ya Iddi na usiku wake na akawa na ziada. - Ziada hiyo ataitoa Zakatul-Fitri kwa viwango vinavyostahiki.
4. KIWANGO CHA ZAKATUL FITRI
- (Imekuja katika mafundisho ya mtume kuwa kiwango ni Swaa’ moja) ambayo ni makadirio sawa na Kilo mbili na nusu au mchoto wa chakula wa ujazo wa viganja viwili vya mkono vya mtu wa wastani vilivyojaa mara nne. - Kinachotolewa ni chakula Kinachotumika na watu Katika nchi hiyo - (mfano mchele) au pia mtu anaweza kutoa kiasi cha pesa chenye thamani sawa na kiasi hicho cha chakula (kisichopungua,ni bora hata ikizidi kdg), - mfano kilo 2 na nusu ya mchele mzuri katika eneo fulani inaweza kuwa ni Tsh 7000/= (Itategemea na eneo)
5. JINSI YA KUTOA ZAKATUL FITRI
- kwa urahisi zaidi Zakatul Fitri hukusanywa pamoja katika sehemu zenye kuaminika kama misikitini au katika taasisi za kidini na kisha kuwafikishia wahusika hivyo pia ukipata ugumu wa kumfikia mhusika wa kupewa Zakatul Fitri unaweza ukaiwasilisha sehemu hizo.
NB: Kama ukiweza ni vizuri zaidi kutoa chakula na kumfikishia mhusika moja kwa moja kama ilivyokuja kiasili katika hadith ya mtume(s.a.w), licha ya watu kuona kuwa pesa ndiyo rahisi na inapendeza zaidi hata kwa mhusika mwenyewe anayepewa Zakatul Fitri ili kupata na mahitaji mengine lakini tambua pia unaweza kutoa chakula hicho kama Zakatul Fitri kisha na pesa hiyo ya mahitaji mengine kama Sadaqa ya kawaida ambayo ni bora pia.
- Kiasi chini ya kiwango cha Zakatul Fitri na au kutoa kitu kingine tofauti na lengo la Zakatul Fitri hiyo sio Zakatul Fitri ni Sadaqa ya kawaida.
6. UMUHIMU WA ZAKATUL-FITRI
Zakatul-Fitri ni kwa ajili ya kuitakasa funga ya muislamu kutokana na maneno machafu na mambo ya upuuzi wakati alipokuwa katika swaum kwa kuwalisha maskini chakula ili nao wapate chakula kizuri siku ya Iddi na ndio maana kutolewa kwake kunakuwa kabla ya kusali sala ya Iddil-Fitri ili kuendana na maandalizi.
7 . MUDA WA KUTOA ZAKATUL-FITRI
- Muda mzuri zaidi ni wakati kuanzia Magharibi ya siku ya mwisho ya Ramadhani hadi asubuhi kabla ya Sala ya Iddil-Fitri. - Inaweza pia kutolewa siku mbili au tatu hivi kabla (Chamsingi iwe kabla ya sala ya Iddil-Fitri). - Kulipa Zakatul-Fitri mapema kabla ya kusali lddi au mapema zaidi ya hapo kutawawezesha maskini na mafakiri kufurahia lddi pamoja na waislamu wengine. - Ikitokea sababu ya msingi kama vile kusahau na mtu akachelewa kutoa Zakatul-Fitri mpaka lddi ikasaliwa, basi hana budi kuitoa baada ya sala lakini jambo la kuzingatia ni kwamba amri ya kutoa Zakatul-Fitri kabla ya sala imetolewa na mtume (s.a.w) hivyo mtu akiivunja amri hii kwa makusudi au kwa uzembe ajue kuwa atakuwa amefanya makosa.
8 . WANAOSTAHILI KUPEWA ZAKATUL-FITRI
- Wanaostahiki ni maskini na wale wote wasioweza kujipatia chakula pamoja na wale walio chini ya uangalizi wa hao maskini na wasiojiweza ili nao wafurahie Iddi pamoja na waislamu wenzao wenye uwezo. - Kama pia ilivyo katika Zakatul-Mal akipewa Zakatul-Fitri mtu asiyestahiki itakuwa ni kudhulumu haki ya wale wanaostahiki, - hivyo mtoaji na mpokeaji wa Zakatul-Fitri hiyo wote watakuwa ni madhalimu. - Ili kuhakikisha kuwa katika jamii au katika mtaa wa waislamu kila anayestahiki kupewa Zakatul-Fitri anapata na kuzuia uwezekano wa mtu mmoja kulundikiwa Zakatul-Fitri kiasi kikubwa sana na mwingine kukosa au kupata kiasi kidogo sana kisichotosheleza mahitaji yake ya siku ya Iddi, - basi ni vyema waislamu wa sehemu hiyo waikusanye Zakatul-Fitri kwa pamoja na kisha waigawanye kwa wote wanaostahiki katika mtaa au sehemu hiyo wakizingatia mahitajio yao kulingana nao majukumu ya kifamilia waliyonayo. - Piah inajuzu kumpa mtu mmoja zaidi ya pishi moja - Muislamu inampasa achukue juhudi ya kuwatafuta wanaostahiki kupewa zaka hii.
NB:Watu unaowajibika kuwatolea Zakatul-Fitri haihesabiki kuwa unawapa Zakatul Fitri, mfano kuwapa wazazi wako sio Zakatul-Fitri kwani wao ni wajibu wako kuwahudumia.

SUKUK NI WIZI NA UTAPELI?

Nimeona katika mitandao ya kijamii maneno ambayo hayapaswi kukaliwa kimya hususani na wadau wa sekta ya fedha ya Kiislam. Maneno hayo anuani yake ni "SUKUK NI WIZI NA UTAPELI, BENKI KUU TOENI TAHADHARI" ukiwa "unaonekana" kuingiza Sukuk katika kinyang'anyiro cha mashindano ya Kisiasa visiwani Zanzibar lakini pia huenda waandaaji wake wana malengo ya kutia hofu wananchi dhidi ya hatua kubwa iliyofikiwa nchini ya kuwa na Sukuk iliyotolewa na SMZ. Tunajiuliza dhamira gani waliyonayo wale walioandaa ujumbe huo? Kwa nini katika mikopo yote ya serikali ya Zanzibar hatujasikia kunasibishwa na Wizi na Utapeli isipokuwa Sukuk?


Waingereza wanamsemo wao "If you want to kill a dog, give it a bad name (ukitaka kumuua mbwa, mpe jina baya)." Kuinasibisha sukuk na wizi na utapeli ni katika mkakati mbaya sana na haunabudi kukemewa vikali na wadau wote wa maendeleo jumuishi katika nchi yetu. Nakemea kitendo hicho ambacho sio cha kistaarabu wala uungwana, huku nikiwa na matumaini kuwa vyombo vya usalama vitakuwa mbioni kuwatafuta watu waliopo nyuma ya ujumbe huo na kuwachukulia hatua stahiki.


Sitoingia katika ujumbe wa kisiasa uliovikwa tu ndani ya ujumbe huo, bali ninachokiona ni mashambulizi dhidi ya Sukuk kama njia mbadala na jumuishi kwa maendeleo ya nchi yetu. Hivyo, niseme kuwa kwa mujibu wa mpango wa maendeleo wa miaka mitano (FYDP), Sukuk inatambulika na mamlaka za nchi kama njia mbadala wa kuwezesha maendeleo ya nchi yetu. Zanzibar Sukuk ni hatua kubwa katika kutekeleza mpango huo na inatambulika na Benki Kuu na Mamlaka ya Masoko ya Fedha na Mitaji nchini. Hivi karibuni, tumeona Gavana wa Benki Kuu akiwa na Waziri wa Fedha wa Zanzibar akipendekeza wananchi wawekeze katika Sukuk hiyo. Hivyo, ni hujuma mbaya sana kutumia upotoshaji kwa lengo si tu la kupata kiki ya kisiasa bali kuichafua Sukuk kama njia jumuishi na inayotambulika nchini. Wale walionyuma ya ujumbe huo, waache mwenendo huo ambao unaathari mbaya sana katika kujenga jamii ya watu wastaarabu, maendeleo endelevu na utoaji wa huduma jumuishi za kifedha nchini.


Kwa upande mwingine, ujumbe huo umedhihirisha na kutukumbusha kiasi gani Siasa inavyoweza kuathiri huduma za kifedha za Kiislam ktk nchi zetu. Binafsi, imenikumbusha kitabu cha Prof Rodney Wilson, The Politics of Islamic Finance akionesha namna gani Siasa za nchi zinaweza kuathiri vizuri au vibaya maendeleo ya Islamic Finance. Kwa muktadha huo, hatupaswi kukaa kimya pale tunapoona watu wachahe wanataka "kutumia siasa chafu" katika jambo muhimu kama hili lenye kujumuisha na kuwapa watu fursa kushiriki katika maendeleo ya nchi yao na kukuza vipato vyao kwa njia Halali bila Riba!


Kwa kuhitimisha, mara zote tumeona athari chanya ya utashi mzuri wa kisiasa kupitia ilani za vyama vya Siasa na utekelezaji wake katika kuwezesha huduma za kifedha za Kiislam nchini kustawi na kunufaisha wananchi. Wote walionyuma ya utashi huo mzuri, tunawapongeza na kuwataka wasikatishwe tamaa kwa hali yoyote iwayo. Hii ni mara ya kwanza natumai itakuwa ya mwisho, kuona watu kupitia "mlango wa kisiasa", wakihusisha Sukuk na wizi au utapeli. Waislam na hususani wataalamu wa masuala ya kifedha ya Kiislam, hatuwezi kukaa kimya na kukubali upotoshaji huo kwa kupitia mlango wa Kisiasa ambao unahujumu au kurejesha nyuma juhudi za miongo kadhaa zenye dhamira ya kutoa fursa kwa Waislam na wananchi wengine kushirikiana na Mamlaka za nchi yao katika upatikanaji wa huduma jumuishi za kifedha nchini.