The primary purpose of this blog is to share latest information, opinions, exchange knowledge and expertise on the field of Islamic Finance from different perspectives. The secondary purpose is to share opinions and key development of Islamic Banking and Islamic insurance in Tanzania.
Tuesday, April 22, 2025
BARUA YA WAZI KWA MHESHIMIWA RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA - OMBI LA KUFUNGULIWA KWA DIRISHA LA HUDUMA ZA KIBENKI ZA KIISLAM KATIKA BENKI YA USHIRIKA
Mheshimiwa Rais,
Salaam Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh.
Kwa heshima na taadhima, napenda kuchukua fursa hii kukuandikia barua hii ya wazi, nikieleza maombi na mapendekezo kwa lengo la kuunga mkono juhudi zako za kuleta maendeleo jumuishi na ustawi wa Watanzania wote bila kujali hali zao za kiuchumi, kijamii wala kidini.
Mheshimiwa Rais,
Tanzania ni nchi ya watu wenye imani mbalimbali, na kwa miongo kadhaa tumeendelea kuishi kwa mshikamano, amani na kuvumiliana. Katika kuhakikisha maendeleo hayo yanamgusa kila Mtanzania, serikali yako imeweka msisitizo mkubwa katika utekelezaji wa *Sera ya Taifa ya Ujumuishi wa Kifedha(The National Financial inclusion framework)*, ambayo inalenga kuhakikisha kuwa wananchi wote wanapata fursa ya kushiriki kikamilifu katika mifumo rasmi ya kifedha kwa ustawi wao binafsi na wa taifa kwa ujumla.
Hata hivyo, kuna sehemu ya wananchi ambao kutokana na misingi ya imani yao ya dini, wanakosa huduma stahiki za kibenki zinazooana na misingi ya imani yao – hasa Waislamu wanaofuata mfumo wa fedha za Kiislam (*Islamic Banking*), unaokataza riba (*riba/usury*) na kuweka mkazo kwenye usawa, uwazi, na kushirikiana katika faida na hasara (*profit and loss sharing*).
Hivi karibuni kumekuwa na juhudi kubwa zikiongozwa na Waziri wa Kilimo Mh. Bashe juu kuanzisha Benki ya Ushirika nchini ambayo inatazamiwa kuwa Mheshimiwa Rais utakuwa ni mwenye kuifungua ifikapo April 28 mwaka huu. Kauli mbiu katika sherehe za ufunguzi wa benki hii ni kuhusu ujumuishi wa kifedha na ugawaji sawa wa fursa *Driving Financial Inclusion, shared prosperity.* Benki ya Ushirika ni chombo muhimu chenye dhamira ya kuwakwamua wananchi wa kipato cha chini na wa kati, hasa wale walioko vijijini na kwenye sekta isiyo rasmi. Kwa kuwa tayari benki hii inalenga kuwafikia wananchi waliotengwa kifedha, tunapendekeza kuwa dirisha maalum la huduma za Kibenki za Kiislam lifunguliwe ndani ya Benki ya Ushirika ili:
1. Kuongeza ujumuishi wa kifedha kwa Waislamu na wengine wanaotaka mfumo mbadala wa kibenki. Hii itawawezesha kushiriki kikamilifu katika shughuli za kiuchumi au kibenki bila hofu ya kwenda kinyume na misingi ya dini yao.
2. Kuchochea maendeleo ya kiuchumi kwa makundi yaliyo pembezoni. Huduma hizi zitawavutia wananchi wengi waliokuwa hawatumii huduma za kibenki, hivyo kukuza ujumuishi, mzunguko wa fedha na uwekezaji.
3. Kukuza ushindani wa haki miongoni mwa taasisi za fedha. Mfumo wa huduma za Benki za Kiislam huwekeza kwa kushirikiana na mteja (kwa mfano kupitia uwezeshaji kwa njia ya *murabaha*, *mudaraba*, au *Salam*), na hivyo kuchochea uwajibikaji, ushirikishwaji na ustawi wa kijamii.
4. Kutekeleza kwa vitendo sera ya Taifa ya Ujumuishi wa Kifedha. Dirisha hili litakuwa mfano hai wa utekelezaji wa sera hiyo, ikionyesha dhamira ya kweli ya serikali katika kuwajumuisha wananchi wote – bila ubaguzi.
Mheshimiwa Rais,
Dirisha hili la huduma za Kibenki za Kiislam linaweza kuanzishwa kwa mafanikio makubwa kwa kuwa benki kuu inayouzoefu wa kusimamia utolewaji wa huduma hizi nchi, tunao wataalamu wa kutosha tena vijana waliosomea shughuli za kibenki za Kiislam wenye uzoefu ambao wanaweza kusimamia huduma hii kwa mafanikio makubwa. Mimi binafsi ni mfano wa vijana hao ambao nimeshirikiana na wengine kuhakikisha tunasaidia benki zetu kuwa na huduma jumuishi nchini.
Tuna imani kubwa na uongozi wako unaojali maslahi ya watu wote, na tuna matumaini kuwa ombi hili litapewa uzito unaostahili kwa ajili ya kujenga taifa jumuishi, lenye haki, amani, ustawi na fursa sawa kwa wote. Kadhalika naomba ombi hili ambalo naamini utaridhia lifanyiwe kazi kwa kushirikiana na chombo chetu cha wataalamu cha CIFCA (Center of Islamic Finance and Advice) na kulifanyia kazi katika taasisi zote za Umma nchini kama vile TADB, Azania Bank, TCB, SELF Mirofinance na taasisi nyingine zinazohusika na uwezeshaji wananchi kiuchumi.
Kwa heshima na taadhima,
Nakutakia mafanikio mema katika kuongoza Taifa letu katika maendeleo, uongofu na njia ya sawa sawa.
Subscribe to:
Posts (Atom)