Pages

Wednesday, May 14, 2025

SERIKALI INAPOKOPA KWA RIBA, UBAGUZI WA FURSA NA HALI YA WAISLAM.

Serikali zote hukopa. Tofauti yao ni madhumun, viwango na namna ya ukopaji. Serikali ya Jamhuri ya Tanzania inakopa kwa njia mbalimbali moja wapo ni kupitia Hati funganiza muda mrefu, au mfupi au mikopo kutoka taasisi za fedha za kibishara na kimataifa. Hivi karibuni serikali ilitangaza Treasury Bond Auction Number 528. Serikali ikikusudia kukopa kuanzia TZS 1mil na itakuwa inalipa riba ya 15.49% kwa mwaka kwa wale watakaoikopesha (neno uwekezaji au investment lisikupe tabu, ni mkopo).

UBAGUZI WA FURSA.

Katika fani ya masuala ya fedha, serikali inapokopa kupitia hati fungani ni fursa kwa wananchi katika kutengeza vipato pale ambapo mwananchi anaikopesha serikali na kuhakikishiwa kuwa atalipwa fedha zake na riba au faida nono ya 15.45% kila mwaka katika mkopo wake kwa muda wa miaka 10 au 20 ijayo.


Je fursa hii ni kwa wananchi wote - waislam, wakristo, wahindu na wengineo? Jawabu jepesi ni kuwa NDIO - watu wote bila kujali dini zao wanaweza kuikopesha serikali. Hatahivyo, jawabu hiyo ni kama mtu anayejifanya kipofu wa uhalisia wa jamii ambayo serikali inaiongoza na kuihudumia. Ni kupe mfano mdogo, unaonaje iwapo Serikali itatangaza kuwa inatoa fursa kuwa sasa Mwanamme au mwanamke atakayeingia katika NDOA YA MKE ZAIDI YA MMOJA atapewa zawadi kila mwaka ya laki mmoja maadamu yupo katika ndoa hiyo, je fursa hii ni kwa watu wote? Waislam na wakristo na wengineo? Jawabu jepesi litakuwa NDIO. Hatahivyo, uhalisia ni kuwa fursa hii ya kuoa na kupewa laki moja kila mwaka (kodi za wananchi wote) itakuwa ni kuwabagua wakristo ambao kwa mafunzo ya Imani yao ndoa ni ya mke mmoja tu. Ama kwa Waislam na wengine, wanaweza kuoa zaidi ya mke mmoja na hivyo ni fursa kwao lakini sio kwa ndugu zao wakristo.



Hivyo, linapokuja suala la KUIKOPESHA Serikali kwa riba, ni wazi kuwa fursa hiyo kwa uhalisia ni kwa WAKRISTO na wengineo na sio kwa Waislam kwa sababu kwa Waislam mikopo yenye kutoza au kutoa RIBA ni Haramu, ni dhambi kubwa! Lakini kwa Wakristo, riba sio dhambi bali kipato halali.


Hivyo kupitia ukopaji wa hati fungani, Muislam anaambiwa fanya dhambi ili upate fedha. Hivyo, muislam anayeshiriki kukopesha kwa riba inaweza kuwa hajui dini yake au ameamua kupata dhambi ilia pate fedha. Je serikali inayoheshimu dini za watu wake na haki yao ya kuabudu, inajisikije kuwafikisha Waislam katika kuwaweka katika hali ya kuchagua baina ya kutengeza fedha na kuchuma dhambi ya kula Riba? Serikali inaonaje pale ambapo Waislam wanakosa fursa hii kwa kujiepusha kwa hiari kwa HOFU YA MUNGU lakini KODI zao zinatumika kulipa riba kwa wananchi wenzao na hivyo wenzao kutajirika bila jasho wakati wao wanalazimika kuchuma fedha kwa kuvuja jasho na kubeba hatari (risk mbalimbali za kibishara n.k)?

NJIA MBADALA.

Kwa kuwa serikali lazima zikope ili kuwezesha miradi mbalimbali ya kimaendeleo na kijamii, hivyo ni jambo la msingi kuwe na njia mbadala ili kufikia lengo hilo. Je mbadala ni upi? Njia mbadala ambayo ni jumuishi kwa wananchi wote -Waislam na wengineo ni kutoa hati fungani ya Kiislam inayojulikana kama SUKUK.


Utaratibu wa Sukuk ni maarufu duniani na kwa mataifa mbalimbali. Nchi kama Nigeria, Afrika Kusini, Sudan, Gambia, Senegali, Malaysia, Indonesia na kadhalika zimekuwa zikitumia utaratibu wa Sukuk kwa ajili ya kupata fedha za maendeleo kwa njia ya miamala isiyohusisha Riba na hivyo kuwajumuisha katika fursa ya uwekezaji wananchi wote. Hivi karibuni, serikali ya mapinduzi ya Zanzibar imezindua ZANZIBAR SUKUK kwa mafanikio makubwa.

Naamini na nafahamu kuwa Serikali yetu inatambua utaratibu huu wa Sukuk (imetajwa katika Mpango wa tatu wa Miaka Mitan -FYDP III) na hivyo niwakumbushe Wizara ya Fedha, kuwa Waislam wanasubiri kwa hamu kuona serikali yao inawajumuisha katika fursa za uwekezaji Halali kupitia Sukuk na wanachukizwa kuona kuwa fursa hiyo imeendelea kufinywa kwao kwa muda mrefu bila ya sababu zinazofahamika.