Pages

Wednesday, September 23, 2020

ILANI ZA VYAMA KWA JICHO LA UCHUMI WA KIISLAMU- SEHEMU YA PILI

Wiki iliyopita tulifafanuwa ilani ya chama cha mapinduzi kuhusu sekta ya fedha kwa jicho la uchumi wa Kiislamu. Katika makala haya tutatazama vyama mbadala au maarufu kama vyama vya upinzani. Kwa kuwa vyama hivi vipo vingi tutatazama vile ambavyo ni vyenye wabunge katika bunge la Jamhuri ya Muungano. Tutaanza na CHADEMA. VIPAUMBELE VYA CHADEMA. Ilani ya Chadema ukurasa wa tani imaainisha vipaumbele 20. Kati ya vipaumbele ishirini, zaidi ya vipaumbele kumi vinahusu masuala ya uchumi na biashara. Baadhi ya vipaumbele hivyo ni:Kwa kushirikiana na sekta binafsi Kujenga uchumi imara wa kidigitali na shirikishi, Kuweka mazingira wezeshi kwa wawekezaji wa ndani na nje, Kuwajengea uwezo wanawake kusimamia na kumiliki uchumi, Kuwezesha Wananchi kumiliki ardhi kwa matumizi endelevu,Kuboresha sekta ya madini na kuwezesha wachimbaji wadogo wanashiriki na kumiliki uchumi wa madini. SEKTA YA FEDHA. Kama ilivyo kwa ilani ya CCM, ilani ya chadema inatambuwa umhimu wa sekta ya fedha. Ilani inasema katika ukurasa 23 "Sekta ya fedha iliyo imara katika nchi, ni nguzo imara katika kuhakikisha uchumi wa nchi unashamiri na unakuwa endelevu. Sekta binafsi iliyo imara inajengwa na sekta fedha, hivyo basi sekta hii ni muhimu sana katika kujenga uchumi." Ilani hiyo pia imebainisha kuwa pamoja na kuwa na mabenki mengi nchini lakini changamoto kubwa ni " kwa wananchi kupata mikopo kwa ajili ya kuanzisha na kuendeleza biashara." Vile vile ilani imebainisha kuwa "kumekuwa na vikwazo vingi na vikubwa kwa wajasiriamali wapya kwenye soko katika kupata mitaji. Jambo hili kwa upande mmoja ndio kisababishi kikubwa cha uwepo wa kundi kubwa la vijana wasiokuwa na ajira hapa nchini." Kadhalika ilani inabainisha kuwa "Changamoto hizo zinatokana na sera za fedha zinazotolewa na benki kuu kwa taasisi za fedha na hivyo kuwa ni kikwazo kikuu kwa mabenki kuweza kukopesha wajasiriamali wapya JE NINI CHADEMA ITAFANYA? Ilani imeahidi mambo kadhaa ambayo ni mazuri lakini yapo ambayo kwa jicho la uchumi wa Kiislamu hazifai kabisa hususani kwa jamii ya Waislam nchini. Hatuwa nzuri zilizobainishwa na ilani ni kama vile; Mosi, Serikali ya Chadema kwa kushirikiana na sekta binafsi itatunga sera za kuwawezesha wananchi kushiriki na kunufaika na biashara ya masoko ya fedha inayotumia mitandao(ushiriki wa masoko ya hisa ya kimataifa kwa kutumia mitandao). Pili, Serikali ya Chadema itahakikisha kwamba kipaumbele cha kwanza kwa taasisi za fedha kiwe ni kuhudumia wananchi kabla ya kuhudumia Serikali. Tatu, Chadema itahakikisha kuwa kunakuwa na urahisi wa upatikanaji wa huduma za benki na fedha kwa ajili ya kusaidia wananchi kukuza biashara zao na kadhalika. Hata hivyo, hatuwa ambayo haifai ni ile isemayo "Kutenga kiasi kikubwa cha fedha kwa ajili ya mikopo yenye masharti na riba nafuu, itakayoshindaniwa na vijana kwa ajili ya kupata mitaji na kuweza kujiajiri na kutoa ajira." Kutenga kiasi kikubwa cha fedha kwa ajili ya mikopo yenye masharti nafuu na kupatikana kwa njia ya ushindani, hii ni sawa lakini mikopo yenye riba nafuu, hili la kutoza riba ni dosari inayoashiria kuwa watunga ilani hawajatambuwa tatizo la riba na ukubwa wake kiuchumi, hawajatambuwa uwepo wa njia mbadala isiyotoza riba na kubwa zaidi hawajatambuwa kuwa kijamii ipo sehemu kubwa ya wananchi ambao HAWAIKUBALI mikopo yenye riba nafuu au ghali. Ni dhambi kubwa kukopa kwa riba! MAPENDEKEZO. Pamoja na ilani kuonesha kuguswa na tatizo la umasikini na ukosefu wa mitaji ya kutosha kwa wananchi, ni wazi kuwa iwapo biashara ya kibenki na bidhaa zile zile za kibenki zitawachwa kama zilivyo sasa za kutoa mikopo ya riba (compunded interest) hatutatatuwa changamoto zilizopo katika sekta ya fedha kwa ukamilifu wake kwa sababu sehemu ya jamii haitokubali kushiriki katika mikopo ya aina hiyo. Inapendekezwa sekta ya fedha katika shughuli zake za uwekezaji kufungamanishwa na sekta ya vitu halisi (real economy) kwa kuwa na sera inayoitaka sekta ya fedha kama vile benki na taasisi za mikopo midogo (microfinance institution), masoko ya mitaji kugawana faida na hasara (risk sharing) na wateja wake kutokana na uwekezaji ambao benki au taasisi husika inafanya na sio kama ilivyo sasa ambapo benki inamwachia mkopeshaji kubeba hatari zote za biashara husika (risk transfer). Vile vile, kuzitaka benki zifanye biashara halisi ya vitu au utoaji wa huduma kwa kwa njia ya mauziano ya vitu kwa faida au kukodisha rasilimali kwa faida na sio biashara ya fedha kwa fedha ambayo ni jambo lisilokubaliwa katika uchumi wa Kiislam. Jambo la mwisho, inapendekezwa kuwa hatuwa mbalimbali zilizoanishwa kuwa na muda maalum wa utekelezaji na sio ahadi zisizokuwa na ukomo wa muda wa utekelezaji. Ahadi za namna hiyo zinafunguwa mlango wa kutowajibika ipasavyo na Serikali kuona inayo muda mwingi. Kwa mfano, ilani inaahidi kuwa "Serikali ya Chadema itaanzisha maeneo maalum (Kisiwa cha Mafia na Pemba) ya mitaji isiyotozwa kodi (tax heaven) ili kupanua wigo wa kupata mitaji kwa ajili ya miradi mikubwa na wajasiriamali wadogo." Je ndani ya muda gani hili litatekelezwa? Muda wa utekelezaji unapaswa kubainishwa kwa uwazi kwa wananchi.

No comments:

Post a Comment