Pages

Sunday, September 22, 2019

WAISLAMU NA BIDHAA ZA KIFEDHA-SEHEMU YA KWANZA.



Uislam ni mfumo kamili wa maisha ya mwanadamu. Mfumo huu kwa miaka zaidi ya 1441 umekuwa ikifuatwa na waislam duniani kote. Katika mfumo wa Uislamu, suala la fedha limefunzwa ipasavyo kiasi ambacho muislam hahitaji kujifunza nafasi, umuhimu na namna ya kutafuta au kuitumiya fedha kutoka kwa wasiokuwa waislam. Uislam katika fiqh yake una mlango mpana wa Fiqh Muamalat ambao ndani yake kuna mlango wa Fiqh al Masrafi Al Islam (Fiqh ya mambo ya fedha ya Kiislam).

Waislam wanaongozwa na misingi imara ya dini yao inayowataka waepukane na riba, gharar (udanganyifu, hatari isiyokuwa na ulazima), na maisir (bahati nasibu-upande mmoja upate na mwingine ukose) katika miamala ya biashara na fedha. Mambo matatu hayo yamekuwa ni doa kubwa au shimo la moto katika huduma za kifedha zilizozagaa ulimwenguni hivi leo. Na mambo hayo pamoja na kudorora kwa maadili mema, yamesababishiya ulimwengu kila baada ya miaka kumi au zaidi, kudorora kwa mfumo wa fedha na uchumi (financial crisis) au kuingiya katika shimo hilo la moto. Hivyo bidhaa nyingi za kibenki, bima, na masoko ya mitaji kwa kuwa na madoa hayo-yaani riba, gharar na maisir-muislamu hulazimika kuepuka bidhaa hizo kama ukoma au zaidi. Kutofanya hivyo ni kuchuma madhambi makubwa! Muislamu halisi anakumbuka kuwa kujihusisha na riba ni kutangaza vita na Muumba wake. Muislam halisi hatothubutu.

Waislam hao wanapojitenga na bidhaa hizo za kifedha, wao wanaathirika duniani kwa kiasi fulani lakini nchi husika piya inaathirika. Tutatowa mifano michache.

1. Huduma za kibenki. Benki nyingi huduma zake kwa kiasi kikubwa isipokuwa huduma chache tu zimezungukwa na riba ya kutisha. Huduma ya kufungua akaunti ya akiba, ukiweka pesa zako ili ziwe salama, benki hizo zinafanya mkataba na wewe wa kukupa riba ya kiasi fulani. Ukifungua akaunti ya hundi, bank hizo zinatumiya pesa hizo na za akiba kukopesha wengine na kuwatoza riba. Hivyo, inakuwa ni kupokeya riba au/na kuisaidiya bank kwa kupitiya hela zako kukopesha wengine kwa mikopo ya riba. Muislam katu hawezi kuhatarisha akhera yake kwa maslahi ya ulimwengu tu kwa kuziwezesha bank hizo kuendeleza uovu wa riba!

Je vipi muislam anaathirika? Muislam anaathirika kwa njia tatu, moja kukosa mahala salama pa kuweka fedha zake. Pili, anakosa mahala pa kuwekeza pesa zake ili kuzilinda fedha hizo dhidi ya mfumuko wa bei unaoshusha thamani ya pesa. Tatu, kukosa mahala pa kupatiya mtaji au rasimali (financing) ambayo itamuwezesha kukidhi mahitaji yake binafsi au ya biashara zake. Sidhani kama kuna serikali ambayo ingependa kuwawacha sehemu ya wananchi wake wapate shida hizo wakati ipo njia nzuri ya kuwasaidiya!

Je vipi nchi inaathirika? Nchi inaathirika mno. Kwanza, inakosa uwezo wa kukusanya akiba (weak saving mobilization) ambazo zinaweza kuwekezwa katika vitega uchumi mbalimbali. Tafiti mbalimbali zinaonesha kuwa ukosefu wa akiba huchangiya nchi kuwa na maendeleo madogo. Kwa mfano ikiwa kunatakiwa uwekezaji mkubwa kwa ajili ya maendeleo ya nchi, mfumo wa kibenki unakuwa hauna hela za uwekezaji katika miradi hiyo. Matokeo yake, nchi inalazimika kukopa nje na kwa masharti ya ajabu ajabu ambayo haitonufaisha nchi ipasavyo. Vilevile wananchi wanakosa mitaji kwa gharama nafuu kwa sababu pesa nyingi zinakuwa nje ya mzunguko wa mabenki. Pili, sera za kifedha (monetary policy) zinashindwa kuwa na athari nzuri katika kuimarisha uchumi wa nchi kwa kuwa mzunguko mkubwa wa fedha upo nje ya taasisi za fedha. Tatu na mbaya zaidi ni kushindwa kuondowa umasikini kwa kupitiya mikopo. Waislam katu hawatachukuwa mikopo ya riba hata ikiwa riba hiyo ni 1%. Sasa mikakati ya kupambana na Umasikini inakuwa ni kwa maeneo ya wasiokuwa waislam lakini maeneo ya Zanzibar, Dar, Tanga, Lindi, Mtwara, Bagamoyo, Mwanza, Songea, Morogoro, Pwani, n.k utakuta hawachukuwi mikopo ya riba na hivyo harakati za kuondowa umasikini zinakuwa ngumu.

Tafiti kadhaa zinaonesha kuwa huduma za fedha zisizozingatiya imani na tamaduni za watu wake, hususiwa na watu hao. Kwa kuliona hili, nchi kadhaa ulimwenguni hata zenye waislam wachache, wameruhusu mfumo wa kibenki wa Kiislamu ambao hautozi au kupokeya riba na badala yake unasimama katika misingi ya kufanya biashara, uwekezaji na ushirikiano kwa kupitiya mikataba ambayo inakidhi kanuni na sheria za kifedha za kiislamu. Matunda mazuri ya mfumo wa kibenki wa Kiislamu unawavutiya hata wasiokuwa waislam kwa kuwa pamoja na kutotoza riba, unazingatia maadili mema katika kuchaguwa maeneo ya kuwekeza. Bank hizi zimejipambanuwa katika kujiepusha na uwekezaji katika biashara za ulevi, uasherati, kamari, silaha, utakatishaji fedha haramu, uzalishaji wa sigara na uharibifu wa mazingira pamoja na mambo mengine. Kwa kupiya huduma hizi na iwapo serikali husika itaweka mazingira rafiki, wananchi wengi watanufaika na nchi pia itanufaika sana. Kwa mfano nchi kama Uingereza, leo ni kitovu cha huduma za fedha za Kiislam! Wanajali maslahi ya kiuchumi kwa nchi yao na wananchi wao. Nchi hiyo imeweza kuvutiya wawekezaji na mitaji mikubwa kutoka nchi mbalimbali kuwekeza Uingereza japokuwa waislam ni sehemu ndogo. Katika afrika yetu, nchi kama Afrika kusini, Kenya, Nigeria zenye uchumi mkubwa zimejizatiti katika kuweka mazingira mazuri. Nchi na wananchi wote bila kujali dini zao wananufaika na huduma hizo.

Nchini Tanzania, Kenya na Uganda, tunazishukuru serikali kuruhusu uwepo wa benki ya Kiislam na huduma za kifedha za Kiislamu ambazo zimekuwa zikifanya vizuri japokuwa kwa kasi ndogo kutokana na changamoto mbalimbali. Ni wakati muwafaka kwa serikali kuwa na utaratibu mzuri na uliokuwa wazi na sheria zilizowazi (Legal, supervisory and regulatory framework), elimu ya bishara yenye kuwajuza wananchi kuhusu mabenki haya n.k. Hatuwa hizi na nyinginezo, zenye kutambuwa mfumo huu zitavutiya wawekezaji, kuongeza kukuza akiba (mobilize national savings through financial inclusion), kuzipa nguvu sera za kifedha katika kuimarisha uchumi na hivyo uchumi wa nchi na wananchi wetu.

Kwa kumaliziya nukta hii, nitowe wito kwa waislamu na wananchi wa imani zote kuweka fedha zao katika benki zenye huduma za kifedha za Kiislam. Na kwa Waislam hususani sehemu ambazo huduma hizo zinapatikana duniani, hawana sababu ya kuweka hela zao majumbani au katika taasisi nyingine au kuendeleya na miamala ya kibenki yenye kujihusisha na riba!

Itaendeleya...

Kwa maarifa zaidi, soma:
Ijuwe ubaya na hatari ya Riba, Gharar na Maisir kwa kusoma hapa:https://mpra.ub.uni-muenchen.de/67711/1/MPRA_paper_67711.pdf
Ijuwe Gharar kwa kusoma hapa : https://islamicmarkets.com/education/gharar.

No comments:

Post a Comment