Pages

Friday, September 27, 2019

WAISLAMU NA BIDHAA ZA KIFEDHA-SEHEMU YA PILI.


Karibu! Katika sehemu ya kwanza ya makala haya tulionyesha kuwa mambo matatu-Riba, Gharar na Maisir-kuwa ni mambo yenye kutiya doa mfumo wa kifedha wa ulimwengu. Tukatoa mfano wa njia mbadala ili kuepukana na madoa hayo katika sekta ya benki. Leo tutaingalia sekta ya bima.

Sekta ya Bima. Bima kwa ufupi ni utaratibu ambao unaomuwezesha mtu au biashara kujikinga na athari mbaya za matukio ya hatari (insurable risk) kwa kukuwezesha kifedha kurudi katika hali yako ya awali. Kwa mfano, hatari za kuunguliwa nyumba yako inaweza kupunguzwa kwa kupitiya bima ya moto ambapo kampuni ya bima hukulipa kiwango cha fedha ambacho utaweza kujenga nyumba yako kama ile ya mwanzo na kuendeleya na maisha. Hatari ya kuumwa na magonjwa na ikawa hauna hela ya kulipiya matibabu pia bima ya afya inakuwezesha kupata fedha ambazo hulipwa katika kituo cha afya ili upate huduma ya matibabu. Hizo ni baadhi ya hatari, hatahivyo hatari zipo aina nyingi, baadhi yake kuhatiwa bima na nyingine hazina bima kama vile vita (war), fujo (riots) n.k.

Uislamu unatambuwa haja ya kuwa na utaratibu ambao unawawezesha wananchi kujikwamuwa au kusaidiana wanapopatwa na hatari mbalimbali katika maisha yao na shughuli zao. Hivyo Uislam hauna pingamizi na dhana ya bima iwapo utaratibu wa shughuli za bima hizo utaachana na madoa yale matatu-RIBA, GHARAR, MAISIR na Uwekezaji ktk sekta ambazo ni kinyume na maadili. Kwa bahati mbaya, katika nchi zetu na duniani kote, bima zote zinamadoa hayo isipokuwa zile zinazoitwa za TAKAFUL (Bima inayofuta kanuni na maadili ya kiislamu). Bima aina hii (TAKAFUL), mkataba wake sio wa mauzo ya kuhamisha hatari ( not a sales contract to transfer risk) kutoka kwa mnunuzi wa bima kwenda kwa muuzaji bali mkataba wake ni wa kujumuika pamoja kusaidiana na kushirikiana katika kuondoa athari za hatari ( contract of partnership / co-operation in sharing the risk). Wanaojiunga na utaratibu wa takaful, wanakubaliana kushirikiana kumsaidiya mwenzao pale anapopatwa na janga au hatari fulani kwa kuchangia fedha kiwango maalum (contribution) na kuwekwa katika mfuko (pooled fund) ambazo zitawekezwa katika vitega uchumi halali (visivyokuwa na riba) ili michango hiyo na mapato yake yaongeze uwezo wa mfuko kukabiliana na athari za majanga yanayoweza kuwakumba wachangiaji wake na kuwalipa mara kwa mara (claims). Mfuko huo wa fedha utasimamiwa na kampuni (Takaful operator) ambayo itahakikisha kila mchangiaji anapewa kiwango stahili cha kuchangia (underwriting) na pia kuwekeza (investing) kwa niaba ya wachangiaji ambao ndio wamiliki wa mfuko huo. Msimamizi (Takaful operator) hulipwa kwa mujibu wa makubaliano maalumu. Kwa kupitiya utaratibu huu, doa la riba, gharar na maisir huwa limetatuliwa!

Inafahamika nchini Tanzania na sehemu nyinginezo kuwa baadhi ya wananchi hususani waislamu kamwe hawaridhii kushiriki katika BIMA hizi za kawaida isipokuwa kwa sababu ya KULAZIMISHWA tu na Sheria ambazo hazizingatii tamaduni na maadili yao. Kwa maneno mengine, wananchi hawa wanavumiliya tu sheria hizo ambazo zinawafanya wafanye kitendo haramu kwa mujibu wa dini yao. Ni wazi kuwa utaratibu wa kulazimisha watu kwa kuweka Sheria nje ya tamaduni za watu. Kadhalika Sheria hizo zinaenda kinyume na misingi ya somo la Legal anthropology ambalo mtaalamu wa sheria Profesa Palamagamba Kabudi amelifundisha na kuwahimiza wabunge na hususani wanasheria kulizingatiya wamapotunga sheria! Ni kwa kuzingatiya misingi ya somo hilo, kwa mfano nchi nyingi ikiwemo Tanzania katika Sheria yake ya ndoa inatambuwa matakwa ya dini mbalimbali katika suala la ndoa na hivyo Sheria inatambuwa ndoa ya mila, ndoa ya kiislamu na ndoa ya kiserikali. Kwa bahati mbaya, sera na sheria zinazohusu uchumi wa fedha (financial economy) hazijazingatiya tamaduni na maadili ya watu wake na hivyo watu wote kuwekwa katika mfumo mmoja tu wa kiserikali (government way and no other way!). Haya ni mapungufu makubwa na wahusika wanapaswa kuyatazama kwa kushirikiana na wahusika ili kuwa na sera na sheria jumuishi (inclusive financial policies and legislation).

Matokeo ya kukosekana TAKAFUL ni kuwa wananchi huathirika na nchi huathirika mno. Wananchi huathirika na matokeo ya majanga mbalimbali ambayo kimsingi yangeweza kuwa na BIMA ya TAKAFUL lakini kwa kuwa bima zilizopo ni HARAMU wanashindwa kujiunga nazo. Hivyo juhudi ya miaka ya mwananchi kujenga nyumba yake au kulima chamba lake n.k, inaweza kupoteya kwa janga moja tu la moto na kumpelekeya kuwa masikini omba omba mtaani. Au ugonjwa unaotibika unapelekeya matatizo makubwa kiafya pale familiya inaposhindwa kumudu gharama wakati BIMA ya TAKAFUL ingemuwezesha kumudu gharama za matibabu na kuokowa maisha yake. Wananchi wanavumiliya lakini ni njia njema ni wananchi waishi kwa kuvumiliya au kufurahiya?

Serikali piya huathirika mno. Serikali inakosa uwezo wa kukusanya akiba (saving mobilization) ipasavyo kuwa kupitiya taasisi za BIMA kwa ajili ya uwekezaji katika miradi ya maendeleo nchini kwa kuwa wananchi hawajiungi na bima hizo zanazokinzana na utamaduni / imani yao. Serikali inakosa mapato ya kodi kutoka katika faida ya makampuni ambayo yapo tayari kuendesha shughuli za bima kwa njia ya TAKAFUL na pia kukosa kodi ya mshahara (PAYE) ambayo ingelipwa na wafanyakazi wa makampuni hayo. Vile vile mzigo mkubwa kwa serikali katika kutowa huduma mbalimbali kama ya afya kwa kuwa wananchi hawamudu kuchangiya gharama zake. Vile vile, serikali kukosa uwekezaji katika sekta ya BIMA kwa kuwa sekta hiyo inatambuwa utaratibu mmoja tu na haitambui TAKAFUL. Mbaya zaidi, huduma za bima hazileti manufaa yanayotarajiwa kwa kuwa wananchi wahazipokei huduma hizo zenye kukinzana na tamaduni / imani zao.

Kwa kutambuwa hasara hizo, nchi mbalimbali duniani kama vile Uingereza, Malaysia, Indonesia, Afrika Kusini, Nijeria, Kenya, Misri, Sudani n.k wameruhusu utaratibu wa TAKAFUL katika nchi zao. Huduma hizo zinawanufaisha wananchi wote bila kubaguwa imani zao. Nchini Tanzania, wananchi walishaeleza haja yao ya kutaka huduma za TAKAFUL katika tafiti iliyofanywa na TIRA mwaka 2012. Tafiti hiyo ilianza kufanyiwa kazi kwa kutengenezwa kanuni (regulations) ambazo zitaiongoza TIRA katika utoaji wa leseni, usimamizi n.k. Wadau mbalimbali walishiriki katika kuzitengeneza na kuzipitisha. Lakini miaka zaidi ya minne, kanuni hizo hazitangazwa rasmi, Kulikoni?

Kwa kutambuwa ucheleweshaji wa jambo hili, Waziri wa Fedha Mh. Mpango katika hotuba yake kwa wadau iliyofanyika mkoa wa Tanga tarehe 27 Oktoba 2018 aliahidi kuwa mambo matatu wizara yake itayaingilia (ministerial intervention) na kuyatatuwa kwa haraka; la kwanza suala la kuwa na sera mpya ya shughuli za BIMA (National Insurance Policy), kanuni (regulation) za uendeshaji huduma mseto wa benki na bima (bancassurance) na kanuni za shughuli za Takaful. Mwaka mmoja ukiwa unakaribiya kitimiya tangu ahadi hiyo itolewe, bado kanuni za Takaful hazijatangazwa ilhali kuna makampuni kadhaa yasemekana yameshaomba kutowa huduma hizo katika mamlaka ya bima nchini (TIRA) lakini bado hayajaruhusiwa!

Wakati nchi na wananchi wanaathirika kutokana na kwa mapokezi hafifu ya huduma za bima (low insurance penetration rate), tunaiomba serikali yetu sikivu ilifuatilie suala hili na kumkumbusha Waziri wa Fedha kulimaliza suala hili ambalo ni kero kwa wadau na wananchi. Naamini TAKAFUL ikiruhusiwa na kuwekewa mazingira mazuri itaongeza kiwango cha wanaotumia huduma hizo mara dufu, kuwanufaisha wananchi na nchi nzima.

Kwa maelezo ya kina kuhusu TAKAFUL, soma;

https://www.findevgateway.org/sites/default/files/mfg-en-paper-takaful-and-poverty-alleviation-2004.pdf










No comments:

Post a Comment